Jioni ilikuwa imesogea wakati Yesu alipowaita Petro, Yakobo na Yohana, akapanda nao juu mlimani. Mchana kutwa walikuwa wakisafiri na kufundisha watu, kwa hiyo kupanda mlimani kulizidi kuwaongezea uchovu wao. Muda kitambo jua likachwa; wakaingia gizani. Hali ya giza na ukiwa ikafanana na jinsi maisha yao yalivyo. Mawingu yalikuwa yakikusanyika. TVV 238.1
Wanafunzi hawakuthubutu kumwuliza Kristo mahali alipokuwa akienda, au kwa nini wamepanda mlimani. Kila mara alikuwa akienda mlimani kuomba, wakati mwingine akikesha huko usiku kucha. Huko mlimani na msituni alifurahishwa sana na hali ya utulivu huo. Lakini wanafunzi walishangaa kuwa kwa nini wanasumbuka kupanda mlimani na hali walikuwa wamechoka katika safari. TVV 238.2
Mara Yesu aliwaambia kuwa safari yao imefika mwisho wake. Akijitenga kidogo nao; mtu wa huzuni akajibwaga katika maombi. Aliomba sana kwa machozi, akiomba uwezo wa kuvumilia katika hali yake ya kibinadamu. Ilimpasa aambatane na Mwenyezi, ndipo aweze kukabiliana na mambo ya siku za usoni. Aliwaombea Sana wanafunzi wake, ili imani yao isitikisike. Alipata umande mwingi usoni mwake, lakini hakujali. Hivyo saa zilipita taratibu. TVV 238.3
Mara ya kwanza wanafunzi wake walishirikiana naye maombini, lakini baada ya kupita muda kidogo walilala. Yesu alikuwa amewaeleza kuhusu mateso yanayomkabili, naye aliwatia moyo kwamba imani yao siyo ya bure. Sio wote hata kati ya wanafunzi wake kumi na wawili, watakaopata njozi ya hakika kuhusu mambo yake. Ni wale walioona na kushuhudia huzuni yake katika Gethsemane tu, ndio aliopanda nao mlimani. Na sasa maombi yake yalikuwa kwamba washuhudie maonekano yake ya baadaye kabla ya matatizo makuu yanayomjia, ili wajue kwamba yeye kweli ni Mwana wa Mungu, na kwamba kifo cha aibu atakachokufa ni mpango wa wokovu. TVV 238.4
Sala yake ilisikiwa. Ghafla mbingu zilifunguka, na mng’ao mtukufu uling’aa mlimani. Mwokozi akazungukwa na utukufu uliong’aa kwa ajabu. Uso wake ukang’aa. Uungu ukaangaza katika ubinadamu, na utukufu wa mbinguni ukaangaza kwake. Alipoondoka kutoka katika hali ya kuomba, Kristo alisirnama katika hali ya Uungu kamili katika fahari yake. Uso wake ulifanana kama jua, na mavazi yake yakawa kama nuru kwa weupe wake. TVV 239.1
Wanafunzi walipoamka, na kumtazama Bwana wao anavyong’aa waliogopa. Walishikwa na mshangao usiosemeka. Walipozoeana na utukufu huo na nuru hiyo ya ajabu, waliona watu wawili wa mbinguni, yaani Musa na Eliya. Musa aliyezungumza na Mungu katika mlima wa Sinai. Eliya aliyepewa hadhi ya kutoonja mauti, akachukuliwa mbinguni bila kufa. TVV 239.2
Musa hakuweza kuingia Kanani kwa ajili ya dhambi aliyofanya huko Meriba. Safari ya kuwaongoza Waisraeli kwenda katika nchi ya urithi wa baba zao, haikuwa yake. Kufia jangwani kulikuwa ni shabaha ya miaka arobaini ya safari ya matatizo, na uangalizi. Musa alipitia mauti, lakini hakubakia ndani ya kaburi, Kristo mwenyewe ndiye aliyemwita kutoka kaburini. Tazama Yuda 9. TVV 239.3
Musa katika mlima ule waliomtokea Yesu, aliwakilisha watu wenye haki, watakaofufuka katika ufufuo wa kwanza. Eliya aliyechukuliwa kwenda mbinguni bila kuonja mauti, anawakilisha watakatifu watakaotwaliwa wakati wa kurudi kwake Yesu mara ya pili bila kuonja mauti; watakaobadililishwa kufumba na kufumbua, wakati wa tarumbeta ya mwisho. I Wakorintho 15:51, 52. Yesu alikuwa na utukufu ule atakaokuwa nao atakapokuja mara ya pili. Utukufu wa Baba yake na wa malaika watakatifu. Marko 8:38; Waebrania 9:28. Katika mlima, kulionyeshwa mfano wa ufalme utakaokuja, lakini kwa kifupi, Kristo Mfalme, Musa, mfano wa watakatifu watakaofufuliwa, na Eliya badala ya watakaochukuhwa bila kuonja mauti. TVV 239.4