Pasaka ilikuwa inakaribia, na Yesu alikuwa akielekea kwenda Yerusalemu tena. Moyoni mwake alikuwa na utulivu kamili wa kuwa na umoja na Baba yake. Alikuwa akielekea kwenda mahali pa kujitolea kuwa kafara. Lakini wanafunzi wake walikuwa na hali ya hofu, mashaka, wasiwasi na giza. Mwokozi alitangulia, nao walistaajabu, wakamfuata kwa hofu. Tena Kristo akawafunulia wale kumi na wawili habari za kusulubiwa kwake na kuteswa kwake, akasema: TVV 305.1
“Angalieni tunapanda kwenda Yerusalemu, na mambo yote Mwana wa Adamu aliyoandikiwa yatatimizwa. Kwa maana atatiwa mikononi mwa mataifa, nao watamdhihaki, na kumpiga. Watamtemea mate na kumwua, na siku ya tatu atafufuka. Nao hawakufahamu na usemi huu. TVV 305.2
Je, hawakuwa wakitangaza kuwa: “Ufalme wa mbinguni umekaribia?” Kristo mwenyewe hakuwapa wanafunzi wake ahadi ya cheo kikuu katika ufalme wake? Je, manabii hawakutabiri kuhusu utukufu wa ufalme wa Masihi? Katika nuru ya mawazo hayo, maneno yake kuhusu kusalitiwa kwake yalikuwa tatanisho, na kivuli. TVV 305.3
Vyovyote vile vingetokea waliamini kuwa ufalme utasimamishwa karibuni. TVV 305.4
Yohana naYakobo nduguye walikuwa katika kundi la kwanza la walioacha vyote wakamfuata Kristo. Mioyo yao iliunganika na moyo wake, hivyo walitamani kupata wakati wa kuwa katika ufalme wake mara moja. Kila mara Yohana alikaa karibu na Mwokozi, na Yakobo alitazamia kupata heshima hiyo. TVV 305.5
Mama yao alikuwa akimhudumia Kristo kwa moyo wote. Kwa moyo wa upendo wa mama alitamani kuona watoto wake wakipata heshima katika ufalme huo. Siku moja walimjia Yesu, wote; mama na wanawe. Akasema, “Mnataka niwatendee nini?” Mama akasema: “Wape wanangu kuketi, mmoja mkono wako wa kulia, na mwingine mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako.” TVV 305.6
Yesu alisoma mioyo yao. Aliona ushirika walio nao kwake. Upendo wao kwake ulikuwa kama upendo wake wa kuokoa. Alisema: “Mnaweza kukinywea kikombe nitakachonywea na kubatizwa ubatizo nitakaobatizwa?” Walitafakari maneno yake ya fumbo, kisha wakasema: “Tunaweza”. Maana yake taabu na majaribu yake. Yesu akasema: “Ndiyo, nmaweza kunywea kikombe changu, na kubatizwa ubatizo wangu. Yohana na Yakobo walikuwa tayari kushiriki katika mateso ya Kristo. Mmoja alikuwa wa kwanza kuuawa kwa upanga, na mwingine alikuwa wa kwanza kuteseka kwa muda mrefu kuliko wote. TVV 306.1
Yesu akasema: “Lakini upande wangu wa kulia au upande wangu wa kushoto, sina amri, ila watapewa na Baba yangu wale walioandaliwa.” Katika ufalme wa Mungu, vyeo havipewi kwa upendeleo au kwa sheria. Hupokewa kwa tabia ilivyokuwa. Taji na kiti cha enzi ni ishara ya hali ya ushikamano uliokuwapo baina ya mtu na Kristo. Atakayesimama karibu sana na Kristo, ni mtu yule aliyepata kukinywea kikombe kichungu zaidi duniani, yaani aliyejinyima sana na kuishi maisha ya kujikana nafsi yake, na kuwa na upendo kama ule uliofanya wanafunzi kuacha vyote, na kuishi na kufanya kazi kwa njia ya kujikana nafsi ili kuokoa wapotevu. TVV 306.2
Wale kumi hawakufurahi. Kwao cheo cha juu katika ufalme ni kuishi kwa ubinafsi. Wakakasirika kwamba wale wawili wamewapita. TVV 306.3
Yesu alisema kwa wenye kukasirika: Mnajua ya kuwa wakuu wao huwatawala na kuwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu.” TVV 306.4
Katika ufalme wa ulimwengu vyeo ni kujitwalia kila kitu watu huishi kwa kutawala watu wa chini. Utajiri wa elimu ndivyo vinavyowapa madaraka, ya kutawala watu wengine, na kuwakandamiza walio chini. Dini nayo ilikuwa namna hiyo. TVV 306.5