Go to full page →

Katika Baraza ya Hukumu VK 134

Walimwengu waovu wote watasimama mbele ya hukumu ya Mungu, wakihukumiwa kwa ajili ya kuihalifu amri ya mamlaka ya mbinguni. Hawana mwombezi ye yote awezaye kuwatetea; hawana udhuru wo wote; nao watahukumiwa kufa kwa milele. VK 134.1

Siku ile, itaonekana dhahiri ya kwamba mshahara wa dhambi siyo hali ya kujiwezea mwenyewe na kupata uzima wa milele, bali ni utumwa, uharibifu na mauti. Waovu wataona malipo ya maisha yao ya uasi. Walipopewa utukufu wa milele wakaudharau; lakini wakati ule wataona kwamba unafaa sana. Kila mtu aliyepotea atalia hivi, “Haya yote yangekuwa yangu, lakini nalichagua kuyazuia yasiingie katika maisha yangu. Loo, nilipumbazika ajabu! Nalikubali kuchagua maumivu, aibu na kushindwa, badala ya amani, furaha na heshima.” Wote wataona ya kwamba wamekatazwa mbinguni kwa haki kabisa. Katika maisha yao walisema, Hatumtaki huyu Yesu atutawale. Kana kwamba wamepumbazwa, naliwaona waovu wakilitazama tamasha la kutawazwa kwa Mwana wa Mungu. Mikononi mwake kuna mbau mbili za amri za Mungu, amri zile ambazo waovu walikuwa wakizidharau na kuziharibu. Watawaona waliookolewa wakiwa na furaha na shangwe wakimsujudu Mungu; na sauti ya wimbo itakaposikiwa na makutano yale ya watu wasimamao nje ya mji, wote watapaaza sauti zao pamoja wakisema, “Ni makuu, na ya ajabu, matendo yako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi; ni za haki, na za kweli, njia zako, Ee mfalme wa mataifa,” (Ufunuo 15:3), hao nao wataanguka kifudifudi, wakimwabudu Mfalme wa uzima. VK 134.2