Badala ya kuwashikilia watu katika utii pasipo kujua juu ya mafundisho yake, kazi ya Kanisa la Roma iliwafanya watu hao kuwa makafiri na waasi. Walikuwa wameudharau utawala wa Papa na kuuita ujanja wa mapadre. Walikuwa wanamfahamu mungu mmoja tu, yaani mungu wa Roma. Walikuwa wanaitazama tamaa na ukatili wa Kanisa la Roma kama tunda la Biblia, na hivyo hawakuwa wanavihitaji vyote viwili. TK 182.2
Kanisa la Roma lilimwakilisha Mungu vibaya, kwa hiyo watu walitupilia mbali Neno la Mungu na Mwandishi wake. Kinyume chake, Voltaire na washirika wake waliliweka kando Neno la Mungu na kuanza kusambaza ukanamungu. Kanisa la Roma lilikuwa linawakanyaga chini watu kwa kisigino cha chuma; sasa watu walitupilia mbali vizuizi vyote. Kwa hasira waliukataa ukweli na uongo pamoja. TK 182.3
Mwanzoni mwa Mapinduzi ya Ufaransa, kwa kibali cha mfalme, watu walikuwa wamepewa nafasi nyingi za uwakilishi kuliko idadi ya watawala na mapadre kwa pamoja. Na kwa namna hiyo, tayari madaraka yalikuwa mikononi mwa walio wengi; na hawakutaka kuyatumia kwa busara na nidhamu. Watu waliokuwa wamekasirishwa waliamua kulipa kisasi. Wenye kudhulumiwa walikuwa wamejifunza somo kutoka kwenye utawala wa kidiktcta na waligeuka kuwa wagandamizaji wa wale waliokuwa wanawadhulumu hapo kabla. TK 182.4
Ufaransa ilivuna katika damu kwa kukubali kulitii Kanisa la Roma. Mahali ambapo Ufaransa ilikuwa imesimamisha nguzo ya kwanza ya kuchomea “waasi wa kidini” chini ya utawala wa Kanisa la Roma mwanzoni mwa imani ya Matengenezo, hapo ndipo wanamapinduzi walipoweka mashine ya kukatia watu vichwa vyao. Mahali pale wafia dini wa kwanza wa imani ya Kiprotestanti walipochomwa moto kwenye karne ya kumi na sita, wahanga wa kwanza walikatwa vichwa katika karne ya kumi na nane. Wakati vizuizi vilivyo katika sheria ya Mungu vilipowekwa kando, taifa lilisombwa na uasi na machafuko. Vita dhidi ya Biblia inasimama katika historia ya dunia kama Utawala wa Udhalimu. Yule aliyepata ushindi siku ya kwanza, alihukumiwa siku ya pili. TK 182.5
Mfalme, mapadre, na watawala walilazimika kutii udhalimu mkubwa uliokuwa unafanywa na watu waliokuwa wamegeuka kuwa wendawazimu. Wale waliokuwa wanatangaza kifo cha mfalme walimfuata mapema kwenye jukwaa la kunyongea. Mauaji ya kikatili yalitangazwa kwa wale wote waliokuwa wanachukia Mapinduzi. Ufaransa ikawa uwanja mkubwa wa makundi ya watu yaliyokuwa yanashindana, yakisukasukwa huku na huko kwa hasira kali. “Mjini Paris machafuko yalifuata machafuko mengine, na raia walikuwa wamegawanyika katika makundi ya fujo, yaliyokuwa hayakusidii kufanya jambo lolote la maana isipokuwa kuangamiza... Nchi ilikuwa karibu kufilisika, majeshi yalikuwa yanazozana kwa ajili ya kupunjwa malipo yao, wakazi wa Paris walikuwa wanakufa njaa, mikoa ilikuwa imeharibiwa vibaya na wanyang’anyi na ustaarabu ulikuwa karibu kutoweka kwa sababu ya machafuko na watu kujifanyia mambo walivyokuwa wanataka.” TK 183.1
Pia watu walikuwa wamejifunza ukatili na mateso ambayo Kanisa la Roma lilikuwa linayafundisha kwa bidii. Wakati huu haukuwa kwa wafuasi wa Yesu kubumtwa kupelekwa kwenye mti wa kuchomea watu moto. Miaka mingi ilikuwa imepita tangu walipoangamia ama kulazimika kukimbilia uhamishoni. “Majukwaa ya kunyongea watu yalikuwa mekundu kwa damu ya mapadre. Vyombo vya baharini na magereza yaliyokuwa hapo mwanzo yamejaa wanamatengenezo Wahuguenot, sasa yalikuwa yamejaa watesi wao. “Akiwa amefungwa kwenye benchi na kusumbuka kwa kazi ngumu na ya muda mrefu, padre wa Kanisa Katoliki la Roma alipitia maumivu yote yaliyokuwa yanaendeshwa na kanisa lao bila kizuizi chochote kwa waasi wa mafundisho yake. (Angalia Kiambatisho.) TK 183.2
“Zikaja siku ambazo wapelelezi walikuwa wanavizia kila sehemu; wakati mashine ya kukata vichwa vya watu ilipokuwa inafanya kazi nzito na kwa muda mrefu kila asubuhi; wakati magereza yalipokuwa yamejazwa kama meli ya kubebea watumwa, wakati mitaro ya maji ilipojazwa kwa mapovu ya damu kuelekea mto Seine....Misururu mirefu ya mateka waliuawa kwa risasi zilizokuwa zinafyatuliwa toka kwenye mzinga. Matundu makubwa yalitobolewa chini ya meli zilizojaza watu. Mamia ya wavulana na wasichana wa umri wa miaka kumi na saba waliuawa na serikali hiyo dhalimu. Watoto waliopokonywa kutoka matitini kwa mama zao waliuawa kwa kuchomwa mikuki na wanachama wa Jacobin, moja ya vyama waasisi wa Mapinduzi ya Ufaransa.” (Angalia Kiambatisho.) TK 183.3
Mambo haya yote ndiyo aliyokuwa anayataka Shetani. Sera zake ni udanganyifu na kusudi lake ni kuwadhalilisha wanadamu, kuharibu kazi ya Mungu ndani yao, kuumbua kusudi la upendo wa Mungu na hivyo kuihuzunisha mbingu. Na kwa kutumia stadi zake za udanganyifu, huwaongoza wanadamu kumtupia Mungu lawama, kana kwamba mateso haya yote yalikuwa ni matokeo ya mpango wa uumbaji wa Mungu. Watu walipogundua udanganyifu wa Kanisa la Roma, aliwachochea kuichukulia dini kuwa ni ulaghai na Biblia kama hekaya za kubuni. TK 184.1