Sikuzote huwa kuna makundi mawili miongoni mwa wale wanaodai kumfuata Kristo. Wakati kundi moja linajifunza maisha ya Mwokozi na kutaka kwa dhati kusahihisha dosari zao na kufanana na Yeye aliye kielelezo, kundi lingine linaepuka ukweli uliodhahiri, unaofaa kutumika maishani, ambao unafunua makosa yao. Hata kipindi kanisa lilipokuwa katika hali nzuri kuliko vipindi vingine vyote, sio wote waliokuwa wakweli na waaminifu kanisani. Yuda aliwekwa pamoja na wanafunzi, ili aweze kuona makosa yake kwa njia ya maelekezo na mfano Wakristo. Lakini kwa kuendekeza dhambi alikaribisha majaribu ya Shetani. Alikuwa anakasirika wakati makosa yake yanakemewa na jambo hilo ililimfanya amsaliti Bwana wake. Soma Marko 14:10, 11. TK 32.1
Anania na Safira walijifanya kutoa sadaka yote kwa Mungu huku wakibakiza kiasi fulani kwa ajili yao wenyewe. Roho wa ukweli akawafunulia mitume tabia halisi ya wanafiki hao, na hukumu ya Mungu iliondoa doa baya lililokuwa katika usafi wa kanisa. Soma Matendo 5:1- 11. Mateso yalipokuja kwa wafuasi Wakristo, wale waliokuwa tayari kuyaacha yote kwa ajili ya ukweli, ndio waliotamani kuwa wanafunzi wake. Lakini mateso yalipokoma, waongofu waliongezeka ambao hawakuwa waaminifu sana, na njia ya Shetani kujiimarisha, ikafunguka. TK 32.2
Wakristo walipokubali kuungana na wale waliokuwa wameongoka nusu nusu kutoka kwenye upagani, Shetani alishangilia. Kisha akawaamsha wawatese wale waliokuwa wanaendelea kuwa wakweli kwa Mungu. Wakristo hawa waasi, wakiungana na wale waliokuwa nusu wapagani, walielekeza mashambulizi yao kwenye sehemu nyeti za fundisho la Kristo. Ilihitaji juhudi kubwa kusimama imara dhidi ya udanganyifu na machukizo yaliyokuwa yameingizwa kanisani. Biblia ilikuwa haikubaliki kama kipimo cha imani. Fundisho la uhuru wa kidini liliitwa uasi, na wale waliokuwa wanalifuata walipigwa marufuku. TK 32.3
Baada ya mgogoro wa muda mrefu, waaminifu waliona kujitenga lilikuwa jambo la lazima. Hawakuthubutu kuvumilia makosa yaliyokuwa yanaweza kuangamiza roho zao na kuhatarisha imani za watoto wao na watoto wa watoto wao. Waliona kuwa amani ingekuwa imenunuliwa kwa gharama kubwa sana kama ingelazimu kuziacha kanuni ili kuipata. Kama umoja ungepatikana kwa kuhafifisha ukweli tu, basi ni heri kuwe na tofauti, na hata vita. TK 32.4
Kwa kweli, Wakristo wa awali walikuwa watu wa pekee. Walikuwa wachache, hawakuwa na mali, vyeo au nafasi za heshima, walikuwa wanachukiwa na waovu, kama Habili alivyokuwa anachukiwa na Kaini. Soma Mwanzo 4:1-10. Tangu siku za Kristo hadi sasa wanafunzi wake waaminifu wamekuwa wakiamsha chuki na upinzani kutoka kwa wale wanaopenda dhambi. TK 33.1
Inawezekanaje basi, Injili iitwe ujumbe wa amani? Malaika waliimba juu ya nyanda za Bethlehemu: “Atukuzwe Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.” Lk. 2:14. Inaonekana kama kuna ukinzani kati ya matamshi haya ya kiunabii na maneno ya Kristo: “Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! Sikuja kuleta amani, bali upanga.” Mt. 10:34. Lakini kama yakieleweka vema, matamko haya mawili yanakubaliana kabisa. Injili ni ujumbe wa amani. Kama dini ya Kristo, ingepokelewa na kutiiwa, ingeleta amani na furaha duniani kote. Kazi ya Yesu ilikuwa ni kupatanisha watu na Mungu na pia watu wao kwa wao. Lakini dunia yote imekuwa chini ya utawala wa Shetani, ambaye ni adui mkubwa Wakristo. Injili inawasilisha kanuni za maisha ambazo ziko tofauti kabisa na tabia na tamaa za kidunia, na hivyo dunia inazipinga. Wanaoipenda dunia huchukia usafi ambao unakemea dhambi, na hivyo huwatesa wale wanaowasisitizia madai matakatifu ya usafi huo. Ni katika mazingira haya, Injili huitwa upanga. Soma Mathayo 10:34. TK 33.2
Wengi walio dhaifu katika imani wako tayari kutoendelea kumwamini Mungu kwa sababu huwaruhusu watu wabaya wafanikiwe, wakati walio wema zaidi na walio safi huteswa na mamlaka zao dhalimu. Inawezekanaje Yeye aliye mwenye haki na mwenye rehema na mwenye uwezo usio na mwisho avumilie udhalimu kiasi hicho? Mungu ametupatia uthibitisho wa kutosha wa upendo wake. Haitupasi kuwa na shaka na wema wake eti kwa sababu tumeshindwa kuyaelewa majaliwa yake. Mwokozi alisema, “Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika neno langu watalishika na lenu.” Yn. 15:20. Wale wanaolazimika kupata mateso na kifo kwa ajili ya imani wanapita tu katika nyayo za Mwana mpendwa wa Mungu. TK 33.3
Wenye haki hutiwa katika tanuru la mateso ili wasafishwe, ili mfano wao uwafanye wengine waamini juu ya uhalisi wa imani na utauwa na kwamba, mwenendo wao usioyumba, uwahukumu wasio watauwa na wasio amini. Mungu anawaruhusu waovu wasitawi na kuonesha uadui wao dhidi yake ili wote wapate kuona haki na rehema yake watakapoangamizwa. Adhabu itatolewa kwa ajili ya kila tendo la ukatili linalofanywa dhidi ya waaminifu wa Mungu kana kwamba alifanyiWakristo mwenyewe. TK 34.1
Paulo alisema “Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa.” 2 Tim. 3:12. Kwa nini basi, mateso yanaonekana kuchelewa? Sababu pekee ni kwamba kanisa limekubaliana na kiwango cha dunia, kwa hiyo, haliamshi upinzani. Dini ya wakati wetu, siyo ile dini safi na takatifu ya Kristo na mitume wake. Kwa sababu ukweli wa Neno la Mungu haujaliwi, kwa sababu utauwa wa kweli ni kidogo sana katika kanisa, likristo umechukua sura ya ulimwengu. Kukiwa na uamsho wa imani ya kanisa la mwanzo, moto wa mateso utawaka upya TK 34.2