Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
  • Results
  • Related
  • Featured
No results found for: "".
  • Weighted Relevancy
  • Content Sequence
  • Relevancy
  • Earliest First
  • Latest First
    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents

    Sura 10—Kumjua Mungu

    KWA njia nyingi Mungu anajaribu kutujulisha tabia zake, ili tupate kumjua na kushirikiana naye. Viumbe vya ulimwengu vyatuonyesha wema na upendo wake milele. Moyo unaofunuliwa utaona upendo na utukufu wa Mungu jinsi unavyoonekana katika matendo yake na katika kazi za mikono yake. Tukiona na kufikiri juu ya miti na maua, mazao ya mashamba, mawingu, mvua, mito, nyota na uzuri wote wa mbingu, hatuna budi kuvutwa moyoni kumjua yeye aliyeviumba vyote.KY 90.1

    Mwokozi wetu alitoa mafundisho mengi juu ya viumbe vya ulimwengu. Akasema juu ya miti, maua, ndege, vilima, maziwa ya maji, na vitu vya mbinguni, pamoja na mambo yanayotukia kwa watu katika maisha yao siku zote; na watu walipoviona vitu vile na mambo hayo mara kwa mara iliwalazimu kukumbuka mafundisho yake.KY 90.2

    Tukifunua roho zetu na kusikiliza sauti ya Mungu katika viumbe vyake, tutapata kufundishwa namna ya kumtii na kutawakali kwa Mungu. Viumbe vyote, tangu nyota zinazofuata njia zao mbinguni, hata na vidudu vidogo, vyote hufuata mapenzi ya Mungu. Tena Mungu huangalia kila kitu alichokiumba. Huzitegemeza nyota katika mahali pakubwa mbinguni, na hata ndege wadogo wa anga huangaliwa naye. Wanadamu wakiondoka asubuhi kwenda kazini, na wakati waombapo, wakati wanapokwenda kulala usiku; tajiri katika jumba lake, hata na maskini katika kibanda chake, Baba yetu aliye mbinguni huangalia wote kwa huruma na upendo. Mtu akitoka machozi ama akiwa na furaha, Mungu huona yote.KY 90.3

    Kama tungesadiki hivyo kabisa, mahangaiko yote yasiyofaa yangeondolewa mioyoni mwetu; kwa sababu mambo yote, makubwa hata madogo, tungekuwa tunayaacha mkononi mwa Mungu; nasi tungeona raha mioyoni mwetu.KY 91.1

    Na kama unapendezwa machoni kwa kuona uzuri wa dunia hii, fikiri juu ya ulimwengu mpya ujao, ambao huko uharibifu wa dhambi na mauti hautaonekana kamwe. Tena ukumbuke ya kwamba fahari yake na utukufu wake havina kifani. Imeandikwa, “Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, wala hayakuingia katika moyo wa kibinadamu, mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao.” 1 Wakor. 2:9. Wale tu watapata furaha katika kutambua uzuri wa viumbe vya ulimwengu, ambao wanafahamu ya kwamba vyote hutangaza upendo wa Mungu kwa wanadamu.KY 91.2

    Mungu husema nasi katika matendo yake, pia katika uongozi wake, tena katika mvuto wa Roho yake mioyoni mwetu. Katika mambo yanayotukia kwetu, na katika hali yetu, twaweza kupata mafundisho yake, ikiwa mioyo yetu imekuwa wazi kuyatambua mafundisho yu Mungu. Mtungu Zaburi alisema, “Nchi imejaa wema wa Bwana.” “Mwenye hekima utayaangalia haya, nao watazijua rehema za Bwana.” Zaburi 33:5; 107:43.KY 92.1

    Mungu husema nasi tena katika Neno lake. Hapo imefunuliwa dhahiri sana namna ya sifa zake na tabia zake, jinsi anavyowatendea wanadamu, na kazi yake kubwa katika kuwakomboa wanadamu. Hapo zimesimuliwa habari za wazee wakuu na manabii na wengine wa zamani waliokuwa watu wa Mungu. Hao nao wakawa watu wenye “tabia moja na sisi.” Yakobo 5:17. Twasoma juu yao jinsi walivyoshindana na mambo ya kulegeza moyo kama sisi tunavyolazimishwa kushindana; walijaribiwa na kuvutwa na mabaya kama sisi tunavyopata kuvutwa; hata hivyo walijitia moyo tena, wakashinda kwa uwezo na neema ya Mungu; na sisi pia tukijua hivyo imetupasa kujitia moyo na kuendelea kujitahidi katika kuyanyosha maisha yetu ili yawe na haki ma- choni pa Mungu. Kama tunaona namna ya kazi ya wale watu wa zamani waliyofanya kwa neema na msaada wa Mungu, na jinsi walivyobarikiwa na kupata furaha katika kufanya kazi ile, sisi pia twatamani kufanana nao katika sifa zao na kuendelea pamoja na Mungu kama wao.KY 92.2

    Maandiko Matakatifu hutoa habari za Kristo, jinsi alivyosema, “na hayo ndiyo yanayonishuhudia.” Yoh. 5:39. Biblia nzima hutoa habari za Kristo. Tangu habari za mwanzo juu ya kuumbwa kwa ulimwengu kwa kuwa “pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh. 1:3—mpaka ahadi ya mwisho, “Angalieni, naja upesi,” Uf. 22:12, twasoma juu ya matendo yake tena twasikiliza sauti yake. Kama unataka kumjua yule aliye Mwokozi, heri ufanye bidii katika kuyachunguza maneno ya Biblia, yaani Maandiko Matakatifu.KY 93.1

    Ujaze moyo mzima maneno ya Mungu. Hayo ndiyo maji ya uzima, na mkate wa uzima utokao juu. Yesu alisema, “Msipoila nyama yake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu.” Akazidi kueleza maana yake hivi: “Maneno ninayowaambieni ni roho, tena ni uzima.” Yoh. 6:53, 63. Kadiri miili yetu inavyokuwa mizima na kupata afya njema kwa ajili ya vile tulavyo na tunywavyo, basi vivyo hali yetu ya kiroho itazidi kuwa njema na kuongezeka nguvu kwa vile tunavyofikiri na kuwaza mambo ya kiroho.KY 93.2

    Jambo la ukombozi wa watu katika Kristo ndilo jambo ambalo malaika wanatamani kulichungulia; tena litakuwa jambo kuu katika kuelimisha wateule wa Mungu katika ufalme wake hata milele. Je, si jambo lifaalo kufikiriwa hata na sisi katika siku hizi? Imetupasa kufikiri sana juu ya rehema na upendo wa Yesu, na jinsi alivyojitoa maisha yake kwa ajili yetu. Imetupasa kuchunguza sifa na tabia za Mwokozi wetu. Ni wajibu wetu kufikiria kazi yake katika kuwaokoa watu katika dhambi zao. Na tunapowaza mambo matakatifu, imani yetu na upendo wetu vitaongezeka kwake, tena kwa hiyo maombi yetu yatazidi kukubaliwa na Mungu. Tutazidi kumtegemea na kumtumainia Kristo na uwezo wake “kuwaokoa kabisa wao wajao kwa Mungu kwa yeye.” Waeb. 7:25.KY 94.1

    Na tunapofikiri juu ya Mwokozi jinsi alivyo mkamilifu na mwenye sifa bora, tutatamani kugeuka moyo kuwa wapya na hufanana naye hasa katika usafi wake. Tena tukizidi kumfikiria Kristo, tutazidi kumshuhudia kwa wengine.KY 94.2

    Biblia haikuandikwa kwa ajili ya wenye elimu nyingi tu; bali ilikusudiwa kuwa ya watu wote, hata na akina sisi. Mafundisho makubwa juu ya wokovu yamekuwa dhahiri kabisa, na mtu ye yote aweza kuyafahamu; hakuna awezaye kukosa njia ya haki ila yeye afuataye nia yake mwenyewe badala ya kufuata mapenzi ya Mungu.KY 94.3

    Tusikubali neno lo lote la binadamu juu ya mafundisho ya Biblia, bali tujifunze wenyewe maneno ya Mungu na kuyachunguza hata tufahamu maana yake. Tukifanya bidii katika kujifunza mambo ya Biblia, tukilinganisha sehemu fulani ya Biblia na sehemu nyingine, na mambo ya kiroho, kwa mambo tutaona ya kuwa akili zetu zinaongezeka.KY 95.1

    Hakuna njia nyingine ya kuzidisha akili zaidi ila ya kujifunza na kuyachunguza maneno ya Biblia. Mafundisho yake yaweza kuadilisha fikara na kuzidisha akili kwa namna isiyowezekana kwa kusoma kitabu kingine cho chote.KY 95.2

    Kama wanadamu wangejifunza na kulichunguza Neno la Mungu kama inavyostahili, wangekuwa na maarifa mengi na sifa bora, na kuimarishwa mioyoni.KY 95.3

    Lakini hakuna faida katika kusoma Biblia ovyo ovyo kwa haraka. Kwa kusoma namna hiyo tungeweza kuisoma Biblia nzima bila kutambua uzuri wake wala kufahamu maana yake, hasa maana ya siri ya ndani. Yafaa kuisoma sehemu moja na kuichunguza sana mpaka maana yake imekuwa dhahiri, na kuona jinsi inavyohusiana na mpango wa Mungu kwa kuwaokoa wanadamu; kufanya hivyo kwa kila sehemu ya Biblia kutakuwa na faida sana kuliko kusoma tu sura nyingi bila kusudi la kujifunza hakika yake. Biblia yako iwe karibu nawe kila mara. Kila upatapo nafasi, isome; jifunze mafungu yake kwa moyo. Hata wakati utembeapo, waweza kulisoma fungu fulani na kufikiri maana yake, na kulitia moyoni.KY 95.4

    Hatuwezi kupata kuelimishwa bila kujitahidi na kukaza moyo kwa kujizoeza kusoma pamoja na kuomba. Kuna sehemu nyingi za Biblia ambazo maana yake imekuwa dhahiri kabisa; lakini kuna sehemu zingine tena ambazo maana yake si rahisi kufahamiwa mara moja. Yafaa kulinganisha sehemu moja na sehemu nyingine, na kuzifikiri na kuzichungua sana pamoja na kuomba. Tusifungue kabisa Biblia na kuyasoma maneno yake bila kuomba. Kabla ya kuifungua Biblia heri tusali ili tupate mwangaza wa Roho Mtakatifu, ndipo tutaupata. Nathanael alipomwendea Yesu, Mwokozi alisema, “Tazama, huyu ni Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake.” Nathanael akamwambia, “Umepataje kunijua?” Yesu akamjibu, “Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwa chini ya mtini, nalikuona.” Yoh. 1:47, 48. Tena Yesu ataonana nasi katika mahali pa siri pa sala, ikiwa tutamwomba ili tupate kuelimishwa na kujua yaliyo ya kweli. Malaika watokao mbinguni watawasaidia wale watakao kuongozwa na Mungu.KY 96.1

    Roho Mtakatifu humtukuza na kumsifu Mwokozi. Kazi yake ni kutuonyesha Kristo, na hali yake jinsi ilivyo yenye haki na usati, na kutudhihirishia habari za wokovu tupatao kwake. Yesu alisema, “Atatwaa katika iliyo yangu, atawapasheni habari.” Yohana 16:14. Roho ya kweli ndiye mwalimu wa pekee awezaye kutujulisha barabara yaliyo kweli ya Mungu. Ni dhahiri ya kwamba Mungu huona wanadamu kuwa wa thamani kubwa, kwa kuwa alimkubali Mwanawe afe kwa ajili yetu, tena ameweka Roho wake Mtakatifu kuwa mwalimu na kiongozi wa wanadamu daima.KY 97.1

    Nataka nimjue Yesu,
    Na nizidi kumfahamu;
    Nijue pendo lake, na
    Wokofu wake kamili.

    Nataka nimwone Yesu,
    Na nizidi kusikia
    Anenapo kitabuni,
    Kujidhihirisha kwangu.

    Nataka nifahamu, na
    Nizidi kupambanua
    Mapenzi yake, nifanye
    Yale yanayompendeza.

    Nataka nikae naye,
    Kwa mazungumzo zaidi,
    Nizidi kuwaonyesha
    Wengine wokofu wake.
    KY 97.2

    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents