“Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote, wala kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu.” Waefeso 5:3 Mar 153.1
Katika mazungumzo ya siku hizi, kuna lugha zisizofaa na zenye kutia hofu, ambazo zinaonesha hali duni ya mawazo na maadili. Heshima ya kweli katika tabia ni nadra sana. Staha na utulivu wa kweli vinaonekana kwa nadra sana. Wapo watu wachache tu ambao ni safi na wasiotiwa unajisi. . . Mar 153.2
Mawazo machafu yanapohifadhiwa yanageuka na kuwa mazoea, na roho ya mtu inaathirika na kunajisiwa. Tendo moja baya linapokuwa limefanyika, doa linakuwa limetokea ambalo haliwezi kuondolewa kwa njia ya kitu kingine cho chote isipokuwa damu ya Kristo; na iwapo mazoea hayo hayataachwa kutokana na kudhamiria kwa dhati, roho huchafuliwa, na vijito vinavyotiririka kutoka katika chemchemi hiyo iliyochafuliwa, huwachafua wengine pia. Mar 153.3
Wapo wanaume na wanawake ambao wanakaribisha majaribu; wanajiweka mahali ambapo watajaribiwa, mahali ambapo ni lazima tu watajaribiwa, wakati wanapojipeleka katika jamii yenye tabia za kuchukiza. Njia bora kabisa ya kujiepusha na dhambi ni kwa kuenenda kwa uangalifu sana wakati wote na katika hali zote, na kamwe kutotenda au kuchukua hatua kutokana na msisimko. Enenda daima ukiwa umetanguliza kicho cha Mungu mbele yako, nawe utakuwa na hakika ya kutenda kwa usahihi. Mar 153.4
Hatari za kimaadili ambazo zinawakabili wote, wazee kwa vijana, zinaongezeka kila siku. Kuharibika kwa maadili, ambako tunakuita upotovu, unapata nafasi ya kutosha kutenda kazi na wanaume, wanawake, na vijana ambao wanadai kuwa ni Wakristo, wataacha mvuto ambao ni duni, wa kupenda anasa, na wa kishetani . . . Mar 153.5
Wale ambao wamejifunza ukweli lakini hawana matunda yanayolingana na madai ya imani yao, wako chini ya majaribu ya Shetani. Katika kila hatua wanayopiga wanakabiliwa na hatari. Katika njia yao Wanakutana na uovu, wanaona mambo, na wanasikia sauti ambazo zinaamsha tamaa zao ambazo hazijadhibitiwa; wanakuwa chini ya mivuto ambayo inawaongoza kuchagua uovu badala ya wema kwa sababu mioyo yao si mikamilifu ... Mar 153.6
Hakuna mafunzo yanayohitajika sana sasa kuliko yale ambayo yanawaandaa vijana kuwa wanyofu kimaadili na kusafisha roho zao dhidi ya kila doa au waa la uchafu wa kimaadili. Mar 153.7