“Wafungue nao malaika wanne waliofungwa kwenye mto mkubwa Frati. Wale malaika wanne wakafunguliwa, waliokuwa wamewekwa tayari kwa ile saa na siku na mwezi na mwaka, ili kwamba waue theluthi ya wanadamu.” Ufunuo 9:14, 15. Mar 152.1
Historia ya mataifa ambayo moja baada ya lingine yametimiza zamu zao, mataifa ambayo bila kujua, walishuhudia ukweli ambao wao wenyewe hawakujua maana yake, inazungumza nasi. Kwa kila taifa na mtu binafsi, Mungu amewapatia sehemu ya kufanya katika mpango wake mkuu. Leo, watu binafsi na mataifa wanapimwa kwa timazi iliyo katika mikono yake Yeye asiyeweza kukosea. Kutokana na uchaguzi wetu wenyewe kila mmoja anaamua juu ya hatima yake, na Mungu anatangua yote ili kukamilisha kusudi lake ... Mar 152.2
Hadi wakati huu, yote ambayo unabii ulikuwa umetabiri kwamba yatatokea, yameweza kuonekana katika matukio ya kihistoria, na hivyo tunaweza kuwa na uhakika kuwa yale ambayo bado yako katika siku za usoni yatatimia katika utaratibu wake. Mar 152.3
Mwaka 1840, utimilizo mwingine wa pekee wa unabii uliamsha shauku ya watu wengi. Miaka miwili kabla, Josiah Litch, aliyekuwa mmoja wa viongozi waliokuwa wanahubiri kuhusu marejeo ya Kristo, alichapisha ufafanuzi wa kitabu cha Ufunuo sura ya 9, ambao ulitabiri kuanguka kwa Ufalme wa Uturuki. Kulingana na makisio yake, ni kuwa ufalme huo ungeangushwa “mnamo mwaka 1840, katika mwezi wa Agosti;” na siku chache tu kabla ya utimilizo wake akaandika: “Kwa kukubali kwamba kipindi cha kwanza cha miaka 150 kilitimizwa kabla ya Deacozes kuingia madarakani kwa kibali cha Waturuki, na kwamba miaka 391 na siku kumi na tano ilianza mwishoni mwa kipindi cha kwanza, basi muda huo ungeishia tarehe 11 Agosti 1840, wakati ambapo mamlaka ya Uturuki kule Constantinople inatarajiwa kuvunjika. Nami ninaamini hivi ndivyo itakavyokuwa.” - Josiah Litch, Signs of the Times, and Expositor of Prophecy, Aug. 1, 1840. Mar 152.4
Kwa wakati uleule uliokuwa umetajwa, kupitia kwa mabalozi wake, Uturuki ilikubali ulinzi wa majeshi ya muungano wa Ulaya, na hivyo kujiweka chini ya utawala wa mataifa ya Kikristo. Tukio hili IiIitimiza unabii kwa ukamilifu kabisa. . . Vuguvugu la marejeo likawa limepata nguvu ya ajabu. Mar 152.5