“Lakini watu wabaya na wadanganyaji wataendelea, na kuzidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika” 2 Timotheo 3:13. Mar 141.1
Halikuwa kusudi la Mungu kwamba watu wake wasongamane katika miji mikubwa, huku wakiwa wamerundikana katika vyumba na nyumba ambazo zimesongamana. Hapo mwanzo Mungu aliwaweka wazazi wetu katika bustani katikati ya mandhari nzuri na sauti zinazovutia za viumbe vya asili, na anatamani kwamba hata leo wanadamu wangefurahia mandhari na sauti hizo za asili. Mar 141.2
Mungu amenipatia nuru kwamba miji mikubwa itajawa na machafuko, vurugu, na uhalifu, na mambo haya yatazidi kuongezeka hadi mwisho wa historia ya dunia hii. Mar 141.3
Huu ni wakati wa watu wetu kuondoa familia zao katika miji mikubwa na kwenda mashambani, vinginevyo vijana wengi, na wengi pia miongoni mwa watu wazima, watanaswa na kuchukuliwa na yule adui. “Tokeni mijini: tokeni mijini!” - huu ndio ujumbe ambao Bwana amenipatia. Mar 141.4
Machafuko na ghasia ambazo zimeenea katika miji mikubwa, hali ya mambo inayosababishwa na migomo na vyama vya wafanyakazi, vitakuwa ni kikwazo kikubwa kwa kazi yetu. Watu wanatafuta kuwaleta wale ambao wameajiriwa katika kazi mbalimbali chini ya utumwa katika muungano wa aina fulani. Huu sio mpango wa Mungu, bali ni mpango wa mamlaka ambayo hatupaswi kuikubali kabisa. Neno la Mungu linatimilizwa; waovu wanajikusanya pamoja tayari kwa kuchomwa moto. Mar 141.5
Wakati huu tunapaswa kutumia uwezo wetu wote katika kutangaza ujumbe wa mwisho wa onyo kwa ulimwengu. Katika kuifanya kazi hii hatuna budi kudumisha msimamo wetu. Hatupaswi kujiunga na vyama vya siri au vyama vya wafanyakazi. Imetupasa kusimama tukiwa huru katika Bwana, daima tukimtazama Kristo. Mar 141.6
Miji ya ulimwengu huu ambayo imejaa maovu itafagiliwa mbali na ufagio wa maangamizi. Katika majanga ambayo sasa yanayapata majengo makubwa na sehemu kubwa za miji, Mungu anatuonesha yale yatakayoupata ulimwengu wote kwa ujumla. Alituambia kuwa: Basi kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno u karibu; nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu milangoni.” Mt. 24:32, 33. Mar 141.7