Ndugu zangu, msistaajabu ulimwengu ukiwachukia. Sisi tunajua ya kuwa tumepita toka mautini kuingia uzimani, kwa maana twawapenda ndugu. Yeye asiyependa, akaa katika mauti.” 1 Yohana 3:13, 14. Mar 142.1
Mtu ambaye ana uhusiano kamili na Kristo ameshinda chuki inayotokana na rangi au tabaka za watu. Imani yake imeshikilia mambo ya umilele. Mungu, ambaye ndiye mwanzilishi wa ukweli hana budi kutukuzwa. Mioyo yetu ni lazima ijazwe kwa imani itendayo kazi kwa upendo na kuitakasa nafsi. Kazi ya Msamaria mwema ni mfano ambao tunapaswa kuufuata. Mar 142.2
Itakuwa ni vigumu kurekebisha mambo yote kuhusiana na suala la tofauti za rangi kulingana na utaratibu wa Bwana hadi pale wale wanaouamini ukweli watakapokuwa wameungana kabisa na Kristo kiasi cha kuwa kitu kimoja naye. Washiriki wetu wa jamii zote-yaani, weupe na weusi, hawana budi kuongoka. Wapo baadhi kutoka katika jamii hizi ambao hawana busara, na wakati suala la tofauti za rangi linapojitokeza, wanadhihirisha kuwa hawajaongoka wala kutakaswa tabia zao. Hisia za ugomvi huamshwa kwa urahisi miongoni mwa wale ambao, kwa sababu hawajawahi kujifunza kujitia nira ya Kristo, ni wenye kiburi na wakaidi. Ndani ya watu kama hao, nafsi inadai utawala kwa nia thabiti ambayo haikutakaswa. Mar 142.3
Kadiri muda unavyopita na chuki ya kikabila kuongezeka, katika sehemu nyingi itakuwa vigumu sana kwa watumishi kutoka jamii ya watu weupe kufanya kazi miongoni mwa watu weusi. Wakati mwingine watu kutoka katika jamii ya weupe ambao hawaitakii mema kazi yetu, watajiunga na watu weusi ili kuipinga, wakidai kuwa mafundisho yetu ni juhudi za kuyavunja makanisa na kusababisha matatizo kuhusu suala la Sabato. Baadhi ya wachungaji kutoka jamii ya weupe na weusi watatoa maelezo ya uongo, na hivyo kuchochea hisia za upinzani mkali katika akili za watu kiasi kwamba watakuwa tayari kuharibu au kuua. Mar 142.4
Nguvu za jehanamu zinatenda kazi kwa werevu wao wote ili kuzuia kutangazwa kwa ujumbe wa mwisho wa rehema miongoni mwa watu weusi. Shetani anatenda kazi ili kufanya iwe ni vigumu kwa wahubiri wa Injili kupuuza chuki iliyopo kati ya watu weupe na weusi. Mar 142.5
Hebu tufuate njia ya busara. Tuepuke kufanya jambo lo lote ambalo Iitaamsha upinzani - jambo lo lote ambalo litazuia utangazaji wa ujumbe wa Injili. Mar 142.6