“Kila amtazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake” Mathayo 5:28 Mar 143.1
Vijana wengi wana shauku ya vitabu. Wanasoma kila kitu wanachoweza kukipata. Hadithi za kusisimua za mapenzi na picha chafu zina mvuto wenye kupotosha. Vitabu vya hadithi za kubuni vinasomwa na wengi, na matokeo yake ni kwamba fikra za wengi zitanajisika. Ndani ya magari, picha za wanawake ambao wako uchi zinasambazwa kwa ajili ya kuuzwa. Picha hizi zenye kuchukiza zinaning’inizwa kwenye kuta za wale wanaofanya biashara ya kutia nakshi. Hiki ni kizazi ambacho upotovu unaenea kila mahali. Tamaa ya macho na ya mwili inaamshwa kwa kutazama na kusoma. Moyo unachafuliwa kwa njia ya fikra. Akili inapendezwa kufikiria matukio yanayoamsha tamaa mbaya. Picha hizi zenye kutia aibu, ambazo zinatazamwa kupitia fikra zilizonajisiwa, zinaharibu tabia na kumwandaa mtu ambaye amedanganyika na kupumbazwa na upendo, ashindwe kujizuia katika tamaa za mwili. Ndipo inafuata dhambi na uhalifu ambavyo vinawavuta wanadamu ambao wameumbwa kwa mfano wa Mungu, kwenda chini kabisa hadi kufikia kiwango sawa na wanyama, na hatimaye kuwazamisha katika uangamivu. Epuka kusoma na kuangalia mambo ambayo yataleta mawazo mabaya. Hebu akili zetu zisidhoofishwe na kupotoshwa hata kwa kusoma sana vitabu vya hadithi. . . Mar 143.2
Haiwezekani vijana kuwa na hali njema kiakili na kanuni sahihi za kidini isipokuwa kama wanafurahia kusoma neno la Mungu. Kitabu hiki (Biblia) kinaeleza visa vyenye kuvutia sana, kinaonesha njia ya wokovu kupitia kwa Kristo, na ndio mwongozo kwa maisha bora na ya juu zaidi. Kama mawazo yao yasingekuwa yamepotoshwa na hadithi za kusisimua ambazo ni za kubuni, basi wote wangeweza kutamka kuwa Biblia ndicho kitabu ambacho kinavutia sana kati ya vyote walivyowahi kusoma. Ninyi ambao mnamtazamia Bwana wenu kuja mara ya pili na kubadilisha miili yenu ya kufa ipate kufanana na mwili wake wa utukufu, mnapaswa kufikia kiwango cha juu cha utendaji. Imewapasa kufanya kazi kwa mtazamo wa juu zaidi kuliko ambavyo mmekuwa mkifanya, ama sivyo hamtakuwa miongoni mwa wale watakaobadilishwa na kuvikwa kutokufa. Mar 143.3