“Husema, Njoni, nitaleta divai, na tunywe sana kileo; na kesho itakuwa kama leo, sikukuu kupita kiasi” Isaya 56:12 Mar 144.1
Mtumwa yule mbaya anasema moyoni mwake, “Bwana wangu anakawia kuja.” Hasemi kuwa Kristo hatakuja. Wala hadhihaki wazo la kuja kwake mara ya pili. Lakini moyoni mwake na kupitia vitendo vyake na maneno yake, anatangaza kwamba kuja kwa Bwana kumekawia. Anaondoa katika mawazo ya wengine usadikisho kuwa Bwana anakuja upesi. Mvuto wake unawaongoza wengine katika kukawia kwa kujiamini zaidi na kutokujali. Wanathibitika katika kupenda mambo ya ulimwengu na kutokujali. Tamaa za kidunia na mawazo potofu huzitawala akili. Mtumwa huyu mbaya anakula na kunywa pamoja na walevi, na kujiunga na ulimwengu katika kutafuta anasa. Anawapiga watumwa wenzake akiwashtaki na kuwalaumu wale ambao ni waaminifu kwa Bwana wao ... Mar 144.2
Kuja kwa Kristo kutawashtukiza walimu wa uongo. Wao wanasema, “Amani na salama.” Sawa na makuhani na walimu kabla ya uharibifu wa Yerusalemu, wanatazamia kanisa kufurahia mafanikio na utukufu wa duniani. Wanafasiri ishara za nyakati kuashiria matarajio yao. Lakini je, Maandiko Mtakatifu yanasemaje? “Uharibifu utawajia ghafla” ... Mar 144.3
Watu wanaweka mbali sana ujio wa Bwana. Wanadhihaki maonyo. Madai yenye majivuno yanatolewa yakisema, “Tangu hapo babu zetu walipolala, vitu vyote vinakaa hali iyo hiyo” 2Petro 3:4. “Kesho itakuwa kama leo, sikukuu kupita kiasi” Isaya 56:12. Tutazama zaidi katika kupenda anasa. Lakini Kristo anasema, “Tazama naja kama mwivi” Ufu. 16:15. Katika wakati huu ambapo ulimwengu unauliza kwa kubeza, “Je, iko wapi ahadi ya kuja kwake?” dalili zinatimia. Wakati wanaposema, “Amani na salama,” ndipo uharibifu utakapowajia ghafla. Wakati wale wenye kudhihaki, ambao wameukataa ukweli, watakapokuwa wamejiamini mno; wakati kazi za kawaida katika njia mbalimbali za kujipatia pesa zitakapokuwa zinaendelea kufanyika bila kujali kanuni; wakati mwanafunzi atakapokuwa anatafuta maarifa ya kila namna isipokuwa Biblia, ndipo Kristo atakuja kama mwivi. Mar 144.4