“Ukiweza kufanya jambo lolote, fanya, utuhurumie, na kutusaidia.” Ni watu wangapi wenye kulemewa na mizigo ya dhambi huomba ombi hilo. Kwa vyovyote vile, jawabu ni kwamba, “Mambo yote huwezekana kwake aaminiye.” Mungu ameandaa mambo kwa njia ya Kristo, ili kushinda kila aina ya dhambi na majaribu yanayowajia watu wa Mungu. Lakini wengi huwa na upungufu wa imani, kwa hiyo huwambali na Kristo. Watu kama hawa wasijitegemee na kujiangalia wenyewe, bali wamtegemee Kisto. TVV 244.1
Imani huja kwa ajili ya neno la Mungu. Wakashikilia ahadi ya Kristo kwamba “Yeye ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe.” Yohana 6:37. Jitupe miguuni pake, ukilia, “Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu.” Ufanyapo hivyo, hutapotea kamwe! Kwa muda mfupi, wanafunzi waliopata bahati, waliona mwanadamu akigeuka sura kufanana na hali ya Uungu, na pia kushushwa mfano wa kishetani Walimwona Yesu akitangazwa kuwa Mwana wa Mungu na kumwona akikutana na kijana mwenye pepo, akisaga meno kwa uchungu. Huyu Mkombozi mkuu ambaye muda uliopita, alionekana akiwa na utukufu, aliinama kumwinua mtu aliyefungwa na Shetani na kutiwa chini ardhini, akamleta kwa babaye na nyumbani. TVV 244.2
Hili lilikuwa somo kuu la ukombozi. Mwana wa Mungu alishuka chini ili kusudi awaokoe waliopotea. Hali hiyo ndiyo itawahusu wanafunzi wake wawe hivyo pia. Maisha ya wanafunzi wa Yesu hayatazamiwi kuwa ya kuishi juu ya mlima pamoja na Yesu peke yake, ila hata chini uwandani pia wanatakiwa kuwahudumia watu walioko, ambao wamefungwa na Shetani, na kuwaweka huru. TVV 244.3
Wakati Yesu alipokuwa na wale wanafunzi tisa peke yao, walimwuliza wakisema, “Mbona sisi hatukuweza kumtoa yule pepo?” Yesu aliwajibu na kusema, “Kwa sababu ya kutokuamini kwenu. Maana amini nawaambieni, mkiwa na imani kama punje ya mbegu ya haradali, mtaweza kuuambia mlima huu, ondoka hapa hata kule, nao utaondoka, wala hakuna kitu kisichowezekana kwenu. Walakini kwa namna hii, haiwezekani, ila kwa kufunga na kuomba.’ Kutokuamini kwao kulikowatenga na Kristo, na kutojali wajibu mtakatifu waliokabidhiwa, vil-iwafanya washindwe kuponya. Wivu kwa wanafunzi waliochaguliwa kupanda mlimani na Kristo, ulikuwa ndio maongezi yao maalum, kwa hiyo walipokuwa katika hali hiyo ya giza walijiingiza katika mashauri ya Shetani. TVV 244.4
Ili kushinda katika mashindano hayo iliwapasa kuwa katika maombi ya juhudi, wakifunga na kujinyenyekesha mbele za Mungu. Iliwapasa kuondoa ubinafsi kabisa, na kujazwa na nguvu za Roho Mtakatifu na uweza wa Mungu. Imani inayomtegemea Mungu kabisa bila kubakiza sehemu yoyote, na kujiweka wakfu hasa katika kazi yake, hali hiyo peke yake ndiyo inaweza kumletea uwezo wa Roho Mtakatifu atakayewawezesha kushinda nguvu za roho za mashetani. TVV 245.1
Shika neno la Mungu, na kufuata misaada yote Mungu aliyoweka kusaidia. Ndivyo roho yako itakuwa hodari Mitego na vizuizi vyote Shetani anavyoweka mbele yako, kama milima ya milele, vitatoweka kwa njia ya imani’ “Hakuna jambo lisilowezekana kwenu.” TVV 245.2