Yesu aliporudi Kapernaumu, alitafuta nyumba atakayoishi kwa muda. Siku zilizobaki za kuishi Galilaya alizitumia kuwafundisha wanafunzi wake kuliko kuhubiria makutano. TVV 246.1
Kristo alikuwa amewaambia kuwa atauawa na kufufuka tena. Alisema kuwa atasalitiwa na maadui zake. Mpaka sasa wanafunzi walikuwa hawakuelewa kwa maneno yake. Ijapokuwa kivuli cha huzuni kilikuwa kikiwajia, wao walikuwa na mashindano tu ya kwamba ni nani atakuwa mkuu katika ufalme wa Mungu. Walijaribu kuficha mabishano hayo, ili Yesu asiyafahamu, lakini Yesu alingoja kwa uvumilivu wakati watakapofahamu dhahiri mambo haya. TVV 246.2
Mara walipofika mjini, mtoza ushuru wa hekaluni aliuliza swali kwa Petro: “Je, mwalimu wenu hulipa kodi?” Kodi hii iliyoulizwa iliwahusu watu wa dini waliopaswa kulipa fungu fulani kila mwaka. Mtu asipolipa mchango huu alihesabika kwa marabi kuwa ni kosa baya. Sasa adui zake walitafuta makasoro juu ya Yesu. Katika mchango huo waliona sababu ya kumpata. TVV 246.3
Ili kumkinga na laumu Bwana wao Petro alijibu kwa haraka kuwa Yesu atalipa kodi. Lakini baadhi ya watu walikuwa wakiachwa wasilipe mchango huo. Makuhani na Walawi, walihesabiwa kuwa wahudumu hekaluni, kwa hiyo hawakupaswa kutoa mchango huo. Manabii pia hawakupaswa kutoa mchango huo. Kwa kumdai Yesu kutoa mchango, marabi, walimhesabu kuwa si nabii, ila ni mtu wa kawaida tu. Kukosa kutoa mchango, kungehesabiwa kama kutojali mambo ya hekalu, au kwa upande mwingine, kama Yesu akilipa fungu hilo ingedhihirisha kuwa yeye si nabii. Jibu la Petro kwa jumla liliruhusu madai ya uongo ya Mafarisayo na wakuu juu ya Yesu. TVV 246.4
Petro alipoingia ndani Mwokozi hakumwuliza juu ya mambo yaliyotokea ila alisema; “Wafikirije Simoni, wafalme wa nchi huwatoza kodi akina nani, wana wao, au wageni?” Akajibu: “Wageni”. Yesu akasema: ‘Basi wana wako huru.” Watu wanapotozwa kodi kwa ajili ya kuimarisha mambo ya wafalme, watoto wa wafalme hawatozwi kodi hiyo. Hivyo Waisraeli, watu wa Mungu walipotoa michango kwa ajili ya kutengeneza mambo ya Mungu Yesu aliye Mwana wa Mungu hakujaliwa hali hiyo. TVV 246.5
Kama Yesu angalilipa kodi hiyo bila upinzani wowote, angekuwa karibu kukubaliana na madai yao, na wakati ule ule kuukana Uungu. TVV 247.1
Lakini aliyakanusha madai yaliyokusudiwa. Alipotayarisha malipo kwa njia ya kimuujiza, alidhihirisha labia ya Uungu wake, kwa hiyo hakuwa mlipa kodi wa kawaida kama watu wengine, wa ufalme. TVV 247.2
Akamwambia Petro: “Nenda baharini, ukatupe ndoana, na samaki atakayenaswa mara ya kwanza, ukifunua kinywa chake utaona ndani yake kipande cha fedha, ulipe kwa ajili yangu na kwa ajili yako.” TVV 247.3
Yesu alipoeleza kwamba hapaswi kulipa kodi ya jinsi hiyo, hakuna mtu aliyembishia. Alilipa mchango huo ili asiwachukize, ingawa hakupaswa kufanya hivyo. Fundisho hili lingekuwa muhimu kwa wanafunzi wake. Wasingejitia katika ushindani usio wa lazima, ili kushikilia haki na kutengeneza mambo. Wakristo wasingepaswa kuacha kanuni yoyote, ila inawapasa kuepukana na matatizo yoyote kadiri iwezekanavyo. TVV 247.4
Wakati Petro alipokwenda baharini, Yesu aliwaita wanafunzi wengine, akawauliza: “Mbona mlikuwa mkihojiana na kubishana huko njiani?” Wakanyamaza kwa ajili ya kuona aibu. Yesu akawakumbushia kuwa alikuwa amewaambia kuwa, atakufa kwa ajili yao, na hali yao ya kutaka ukuu ilikuwa kinyume cha hali yake ya upendo usiokuwa wa binafsi. Lakini ijapokuwa amewaambia wazi kuhusu mambo yanayomkabili, usemi wake wa kwenda Yerusalemu, uliamsha matumaini yao ya kwamba anaenda kutawazwa kwa kuwa mfalme. Jambo hili lilileta maswali kwamba ni nani atakuwa mwenye cheo cha juu katika utawala huo. Mwishowe mmoja alithubutu kumwuliza Yesu: “Nani atakuwa mkuu katika ufalme wa mbinguni?” TVV 247.5