Lakini huduma ya meza ya Bwana haikukusudiwa kuwa wakati wa huzuni. Kadiri wanafunzi wa Yesu watakavyokusanyika Mezani pa Bwana, hawapaswi kuomboleza kwa ajili ya upungufu wao. Hawapaswi kutafakari tofauti zao na wenzao. Huduma ya kutawadhana imeshughulikia yote hayo. Sasa wanakuja kukutana na Kristo, Hawapaswi kusimama kwenye kivuli cha msalaba bali katika mwanga wake wa wokovu. Wapaswa kufungua mioyo yao kwa nuru itokayo Jua la Haki. Wanapaswa kusikia Maneno yake: “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi si kama ulimwengu utoavyo.” Yohana 14:27. TVV 373.4
Bwana wetu asema, “Mkiteswa na kuudhiwa kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, kumbukeni upendo wangu, jinsi ulivyo mkuu hata nikatoa maisha yangu kwa ajili yenu. Kazi yenu ikionekana kuwa ngumu mno, na mzigo ukiwalemea, kumbuka kwamba niliuvumilia msalaba kwa ajili yenu, nikiidharau aibu. Mwokozi wenu yu hai akiwaombea. TVV 374.1
Huduma ya meza ya Bwana huwaelekeza watu kwenye tukio la kurudi kwake Kristo. Ilikusudiwa kuendeleza tumaini hili mawazoni. “Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.” 1 Wakorinto 11:26. TVV 374.2
Kristo aliianzisha huduma hii ili ipate kuzungumza na akili zetu daima juu ya upendo wa Mungu. Haiwezekani kuwa na umoja kati ya roho zetu na Mungu usipokuwa kupitia kwa kristo. Wala hakuna kitu kingine kinachofanya upendo wake uwe na manufaa kwetu isipokuwa kifo cha Kristo. Na ni kwa sababu ya kifo chake tu ndipo tunaweza kukutazamia kurudi kwake kwa furaha. Dhamiri zetu zinahitaji kuamshwa na kuhimizwa kushikilia siri ya utauwa, kutambua zaidi kuliko tunavyotambua, mateso ya kulipia ya Kristo. TVV 374.3
Bwana wetu amesema: “Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuiinywa damu yangu, hamna uzima ndani yenu . . . kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli.” Yohana 6:53-55. Kwa kifo cha Yesu tunawiwa hata na uzima wa sasa. Chakula tunachokula kimenunuliwa kwa mwili wake uliovunjwa; na maji tunayokunywa, hutokana na damu yake iliyomwagika. Hakuna mtakatifu mmoja au mwenye dhambi alaye chakula chake cha kila siku bila kuboreshwa na mwili na damu ya Kristo. Msalaba wa Kalwari umepigwa chapa juu ya kila kipande cha mkate; na nuru yake huonekana katika kila chemchemi ya maji. Nuru inayong’aa kutoka katika Huduma ya meza ya Bwana huvitakasa vitu vyote vya maisha yetu ya kila siku. Mkusanyiko wa jamaa huwa sawa na meza ya Bwana na kila mlo Ushirika Mtakatifu (Sacrament). TVV 374.4
Kuhusu hali yetu ya asili ya kiroho Yesu anasema, “Aulaye mwili wangu, na kuiinywa damu yangu, anao uzima wa milele.” Kwa kulipokea neno lake, na kuyafanya maagizo yake, hushirikiana naye. Alisema, “Aulaye mwili wangu, na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba, kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi.” Yohana 6:56, 57. Kadiri imani itakavyotafakari kafara kuu ya Bwana wetu, moyo huungana na maisha ya kiroho ya Kristo. Kila adhimisho la Meza ya Bwana huleta kiungo hai ambacho kwacho muumini hufunganika na Kristo na hivyo na Baba. TVV 374.5
Tunapopokea mkate na divai inayofananishwa na mwili wa Kristo, uliovunjika na damu iliyomwagwa kwa mawazo tunashuhudia mashindano ambayo kwayo upatanisho wetu na Mungu, ulipatikana Kristo huonekana amesulibishwa miongoni mwetu. Wazo la Kalwari huamsha hisia hai na takatifu katika mioyo yetu. Kiburi na ibada ya nafsi haviwezi kusitawi katika roho ambayo daima hutunza kumbukumbu ya matukio ya kalwari. Yeye autazamaye upendo wa Mwokozi usio kikomo atabadilishwa kitabia. Ataondoka kwenda kuwa nuru kwa ulimwengu, akiangaza kwa kiwango fulani upendo huu wa ajabu. TVV 375.1