Yuda alikuwa ameondoka katika kile chumba cha ghorofa, na Kristo alibaki pekee na wale kumi na mmoja. Alikuwa karibu kuzungumzia kuhusu kutengana kwake na wanafunzi wake; lakini kabla ya haya alitaja kazi yake kuu iliyomleta hapa duniani. Alikumbusha mara kwa mara kuwa kudhalalishwa kwake kote na mateso yake yote vitalitukuza jina la Baba yake. Kwa jambo hili alilielezea kwanza mawazo ya wanafunzi wake. TVV 376.1
Bwana, na Mkuu wao, Mwalimu na Rafiki wao mpendwa, alikuwa wa thamani mno kuliko maisha yao. Na sasa alikuwa awaache. Giza la mambo yajayo lilifunika mioyo yao. TVV 376.2
Lakini maneno ya Mwokozi yalijaa matumaini. Alijua kuwa mbinu za Shetani hufaulu sana kwa wale wanaotingwa na matatizo. Kwa hiyo aliwaelekeza mawazo yao kwa makao ya mbinguni: “Msifadhaike mioyoni mwenu; Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.” (Yohana 14:1-3). Nikiondoka, bado nitawaangalia kwa dhati. Naenda kwa Baba, kushirikiana naye kwa niaba yenu. TVV 376.3
Kuondoka kwa Kristo kulikuwa, kinyume na vile wanafunzi walivyokuwa wakihofia hakukuwa na maana ya kutengana milele. Alikuwa akienda kuwaandalia mahali, ili apate kuwapokea kwake. Wakati akiwaandalia makao, wao watakuwa wakijiandaa tabia zao ili zifananena za mbinguni. Tomaso akisumbuliwa na mashaka, akasema, “Bwana, sisi hatujui uendako, nasi twaijuaje njia? Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba, tangu sasa mnamjua, tena mmemwona.” TVV 376.4
Hakuna njia nyingi za kufikia mbinguni. Hakuna uwezekano wa kila mmoja kuchagua njia yake. Kristo alikuwa ndiye njia ambayo kwayo wazee wa zamani na manabii waliokolewa. Yeye ndiye njia pekee ambayo kwayo sisi tunaweza kupitia ili kumfikia Mungu. TVV 377.1
Lakini bado wanafunzi hawakuelewa hivyo. ‘’Bwana utuonyeshe Baba, yatutosha,” Filipo akasema ghafula. Kristo aliuliza kwa mshangao wa uchungu: “Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo?” Je, inawezekana kwamba humwoni Baba katika kazi azitendazo kupitia kwangu? “Basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba?” “Aliyeniona mimi amemwona Baba,” Kristo hakukoma kuwa Mungu alipofanyika mwanadamu. Utatu mtakatifu ulidumu kuwa wake. Kazi za Kristo zilidhihirisha uungu wake. Katika Yeye Baba alikuwa amefunuliwa. TVV 377.2
Kama wanafunzi watauamini mwungano huu muhimu kati ya Baba na Mwana basi, imani yao isingalitikiswa wakati wakiona mateso na kifo cha Kristo. Ni kwa kiasi gani Mwokozi alitafuta kwa bidii kuwaandaa wanafunzi kwa tufani kubwa ya majaribu iliyokuwa ikiwakabili wote. Wote waliokuwapo walijisikia kicho kitakatifu walipoyasikiliza kwa makini maneno yake. Na kwa jinsi mioyo yao ilivyovutwa kwake Kristo kwa upendo zaidi, vilivyo hivyo ndivyo walivyovutwa kila mmoja kwa mwenzake. Walijisikia kuwa mbingu zilikuwa karibu sana nao. TVV 377.3
Mwokozi alikuwa na shauku ya kutaka wanafunzi wake waelewe kwa nini Uuungu wake uliungana na ubinadamu. Alikuja ulimwenguni kuonyesha utukufu wa Mungu, ili mwanadamu avutwe kwa uwezo wake kuinuliwa na kurudishwa kwake. Yesu hakuonyesha sifa zo zote zile wala kutumia uwezo wo wote ule ambao mtu hawezi kuupata akiwa na imani kwa Yesu. Hali kamilifu ya ubinadamu wake ni hali ambayo kila mfuasi wake anaweza kuwa nayo, iwapo atajitoa kwa Mungu kama yeye alivyojitoa. TVV 377.4
“Na kazi kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa baba”. Kwa maneno haya Kristo alikuwa na maana kuwa kazi ya wanafunzi wake itakuwa na matokeo makubwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Baada ya kupaa kwa Kristo, wanafunzi walitambua utimilizo wa ahadi yake. Walijua kuwa Mwalimu wa mbinguni alikuwa kama vile alivyosema. Kadri walivyoutukuza upendo wa Mungu mioyo ya watu ilitiishwa na makutano wakamwamini Yesu. TVV 377.5