Wakati huu Yohana Mbatizaji alikuwa akihubiri huko Bethlehemu, kando ya mto wa Yordani. Mahubiri ya Yohana yalikuwa yamewaingia watu sana. Hakuwajali wakuu wa Sanhedrin wala hakutaka ruhusa kwao, walakini kazi yake ilipendeza sana, akaongeza kuifanya zaidi na zaidi. TVV 66.1
Baraza la Sanhedrin lilihusika na makuhani, watawala na walimu. Wakati wa utawala wa Wayahudi, baraza la Sanhedrin ndilo lilikuwa baraza kuu la taifa, ingawa kwa wakati huu lilikuwa chini ya watawala wa Kirumi, lakini lilikuwa likihesabiwa kuwa ni baraza la mambo yahusuyo dini. Sanhedrin basi lisingeweza kuacha kuchunguza kazi ya Yohana. Wengine walitaja mafunuo yaliyokuja kwa Zakaria hekaluni, kuhusu mtoto wake kwamba ndiye Masihi aliyetangazwa. Mambo haya yaliwataharuki watu kuhusu kazi ya Yohana. TVV 66.2
Muda ulikuwa umepita, tangu Waisraeli walipopata nabii. Madai ya kutaka watu watubu yalionekana kuwa mapya na ya kustusha. Waongozi wengi wasingekwenda kusikia ujumbe wa Yohana wasije wakafunuliwa siri za maisha yao. Walakini mahubiri yake yalikuwa ni matangazo ya Masihi. TVV 66.3
Ilikuwa inaeleweka kuwa unabii wa Daniel wa majuma sabini, ulifunika na kuja kwa Masihi pia. Nao ulikuwa karibu kumalizika. Kwa hiyo walitazamiwa kushiriki katika ufalme wa utukufu kama walivyotazamia. Jambo hilo ndilo lililokuwa likiwatumainisha kwa uchangamfu. Na Sanhedrin ingepaswa kuukubali ujumbe wa Yohana au kuukataa. Mpaka wakati huo walikuwa na tatizo jinsi ya kuwatuliza watu, wasishughulike na mahubiri ya Yohana. Ili kufikia uamuzi fulani walituma wajumbe kutoka kwa makuhani na walawi wapate kwenda Yordani kwa Yohana, ambaye ni mwalimu mpya. TVV 66.4
Wajumbe walipofika walikuta makutano wanasikiliza mahubiri ya Yohana. Walikuja wakijionyesha jinsi walivyokuwa maarufu, ili kusudi kufanya mvuto kwa watu, lakini watu waliwaona vivi hivi tu, ingawa walijionyesha jinsi walivyokuwa na fahari. TVV 67.1
Watu wakuu wakiwa na mavazi rasmi., walisimama mbele ya Yohana na kusema: “Wewe ni nani?” Yohana akijua mambo yao, alisema: “Mimi siye Kristo.” Nini basi, wewe ni Eliya?” “Mimi siye Eliya.” “Je, wewe u nabii?” “La.” Wewe u nani basi, ili tuwapelekee majibu waliotutuma?” “Wewe wajinena kuwa nani?” “Mimi ni sauti iliayo nyikani: Itengenezeni njia ya Bwana, yanyoosheni mapito yake,” kama alivyosema Isaya. TVV 67.2
Zamani mfalme alipotaka kutembelea nchi yake, watu walitumwa kwenda kutengeneza njia, mabonde yalijazwa, na kusawazisha mahali palipoharibika, ili mfalme apate kusafiri katila hali ya usalama. Hali hii imesemwa na nabii ‘ Isaya ili kuonyesha kazi ya Injili, “Kila bonde litajazwa na kila mahali palipoinuka patasawazishwa.” Isaya 40:4. Roho wa Mungu anapomjaza mtu, kiburi chake hudhiliwa. Anasa za ulimwengu, cheo, na kujitukuza huonekana kuwa havina thamani yoyote. Kisha unyenyekevu, kujinyima, na upendo. Hayo ndiyo huonekana yenye thamani kwake. Hii ndiyo kazi ya Injili, ambayo Yohana alikuwa akifanya. Ndiyo ujumbe kwake. TVV 67.3
Walimu wa Kiyahudi waliendelea kumwuliza: “Mbona unawabatiza watu, kama wewe siye Kristo, wala Eliya, au nabii?” Kusema nabii, kulimaanisha Musa. Wakati Yohana Mbatizaji alipoanza kazi yake, watu wengi walidhani kuwa ni Musa aliyefufuka toka ufuni. Iliaminiwa pia kwamba, kabla ya kuja kwa Masihi, Eliya ataonekana wazi kimwili kwanza. Yohana alilikanusha tazamio hilo. Lakini baadaye Yesu alisema, habari za Yohana: “Mkitaka kukubali, ndiye Eliya atakayekuja.” Mathayo 11:14. Yohana alikuja katika nguvu na roho ya Eliya ili kufanya kazi ya aina ile Eliya aliyofanya. Lakini Wayahudi hawakukubali ujumbe wake. Kwao hakuwa Eliya. TVV 67.4