Wengi katika hao waliokusanyika huko Yordani walikuwako wakati Yesu alipobatizwa. Lakini ishara iliyotolewa ilifahamika kwa watu wachache tu kati yao. Miezi iliyotangulia huduma ya Yohana Mbatizaji, watu wengi walikataa mwito wa kutubu. Hivyo wakati mbingu ilivyomshuhudia Yesu wakati wa ubatizo wake, hawakutambua. Watu ambao hawakuwa na imani kwake, hawakuuona ufunuo wa utukufu wa Mungu. Masikio ambayo hayakusikiliza sauti yake, hayakutambua ushuhuda huo. Hivyo ndivyo ilivyo na sasa. Kila mara kuwako kwa Yesu, na malaika wahudumu hudhihirika katika mikutano ya watu, lakini wengi huwa hawana habari. Hawasikii kitu kigeni. Lakini kwa wengine kuwako kwa Mwokozi hudhihirika kwao. Wao hufarijika, na kutiwa nguvu, na kubarikiwa. TVV 67.5
Wakuu waliotoka Yerusalemu walimwuliza Yohana: “Kwa nini unabatiza?” Nao walikuwa wakingojea jawabu lake. Ghafla, alipowaangalia makutano uso wake ulingaa na mwili mzima ukabadilika. Mara akinyosha mikono yake, alisema, “Nawabatiza katika maji lakini kati yenu anasimama msiyemjua yule ajaye nyuma yangu, ambaye sistahili hata kulegeza gidamu za viatu vyake.” Ujumbe uliwekwa kando tu, kama usio na maana, wa kupelekwa kwa wazee wa baraza la Sanhedrin. TVV 68.1
Wakati wa ubatizo wa Yesu mawazo ya Yohana yaliongozwa kwenye fungu la Isaya 53:7 lisemalo: “Kama Mwana Kondoo apelekwaye machinjioni.” Katika majuma yaliyofuata, Yohana alijifunza sana unabii huu, na pamoja na matoleo ya kafara. Aliona kuwa kuja kwa Kristo kulikuwa muhimu sana kuliko makuhani na watu walivyodhani. Alipomwona Yesu yuko katika mkutano baada ya kutoka jangwani, alisubiri kwa subira asikie Mwokozi akitangaza kazi yake. Lakini hakusikia neno, wala hakuona ishara yoyote. Yesu hakujibu lolote kwenye ubatizo wake katika tangazo lililotolewa, bali aliunganika na wanafunzi wa Yohana, wala hakujionyesha. TVV 68.2
Siku ya pili yake Yohana alimwona Yesu akimjia, akiwa na nuru ya utukufu wa Mungu iking’aa juu yake, nabii alinyosha mikono yake, akasema: “Tazama Mwana Kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu.” Huyu ndiye niliyesema kuwa, ajaye nyuma yangu ni mkuu .... Niliona Roho akishuka kama njiwa kutoka mbinguni juu yake. . . . Aliyenituma nibatize kwa maji, aliniambia,. . . Huyu ndiye abatizaye kwa Roho Mtakatifu.” Nami nimeona na kushuhudia kwamba huyu ni Mwana wa Mungu.’ TVV 68.3