Kanuni za Biblia zilifundishwa nyumbani, shuleni, na kanisani; matunda yake yalidhihirika katika mafanikio, akili, usafi, na kiasi. Kwa miaka mingi mtu asingeweza kumwona “mlevi, ama kusikia jina la Mungu linatajwa bure, au kukutana na ombaomba.” 190Bancroft, pt. 1, ch. 19, par. 25. TK 191.4
Kanuni za Biblia ni kinga ya uhakika kwa ukuu wa taifa. Makoloni dhaifu yalikua na kuwa nchi zenye nguvu, na ulimwengu uliweka alama ya ustawi wa “kanisa bila Papa, na nchi pasipo mfalme” Lakini idadi iliongezeka ya watu waliovutwa kwenda Marekani wakisukumwa na malengo tofauti na yale ya Mahujaji. Idadi ya wale waliokuwa wanatafuta faida za kidunia tu iliongezeka. TK 192.1
Wakoloni wa awali waliruhusu washiriki wa kanisa pekee kupiga kura au kupewa uongozi serikalini. Kipimo hiki kilikubalika ili kutunza usafi wa taifa; matokeo yake yalikuwa ni uharibifu kwa kanisa. Wengi walijiunga na kanisa bila badiliko la moyo. Hata ndani ya huduma walikuwemo wasiojua uwezo wa Roho Mtakatifu unaomfanya mtu kuwa mpya. Tangu wakati wa Kostantino hadi sasa, kujaribu kulijenga kanisa kwa msaada wa serikali, yaweza kuonekana kuwa ulimwengu unavutwa karibu na kanisa, lakini uhalisia ni kwamba kanisa linavutwa karibu na ulimwengu. TK 192.2
Makanisa ya Kiprotestanti ya Marekani na yale ya Ulaya, yalishindwa kusukuma mbele njia ya matengenezo. Walio wengi, kama vile Wayahudi wakati Wakristo au waumini wa Kanisa la Papa wakati wa Luther, waliridhika kuamini kile ambacho baba zao waliamini. Makosa na mapokeo potovu vilitunzwa. Matengenezo yalikufa polepole, hadi ilipoonekana kuwa kunahitaji kubwa la matengenezo ndani ya makanisa ya Waprotestanti kama ilivyokuwa kwa Kanisa la Roma wakati wa Luther. Kulikuwa na tabia ile ile ya kuheshimu maoni ya watu na kulibadilisha Neno la Mungu na mahali pake kuweka nadharia za wanadamu. Watu waliacha kuyachunguza Maandiko na hivyo wakaendelea kushika mafundisho yasiyo na msingi kwenye Biblia. Majivuno na ubadhirifu viliendelezwa ndani ya umbo la dini, na makanisa yakaharibika. Desturi ambazo baadaye zingewaharibu mamilioni; zilikuwa zinakita mizizi chini. Kanisa lilikuwa linaziinua desturi hizi badala kushindania “imani waliyopewa watakatifu mara moja.” Hivi ndivyo zilivyohafifishwa kanuni ambazo Wanamatengenezo walizitesekea sana. TK 192.3