Ujumbe wa ujio ulishaanza kuhubiriwa kule Uingereza tangu mwaka 1826. Kwa sehemu kubwa muda halisi wa ujio huo ulikuwa hautajwi, ila ukweli wa kuja upesi kwa Kristo katika uweza na utukufu ulitangazwa kila mahali. Mwandishi mmoja wa Kiingereza alieleza kuwa wachungaji wapatao 700 wa Kanisa la Uingereza walikuwa wanaihubiri “Injili hii ya ufalme.” TK 230.2
Ujumbe uliokuwa unaelekeza mwaka 1844 kama wakati wa kuja kwa Bwana ulihubiriwa pia huko Uingereza, Scotland na Wales. Machapisho kutoka Marekani yaliyokuwa yanahusu kuja kwa Yesu yalisambazwa kila mahali. Mwaka 1842 Robert Winter, Mwingereza aliyekuwa amepata imani ya ujio wa Yesu kule Marekani, alirejea nchini kwake kutangaza kurudi kwa Bwana. Wengi walijiunga naye katika kazi hiyo katika sehemu mbalimbali za Uingereza. TK 230.3
Huko Amerika ya Kusini, Lacunza ambaye ni Mhispania na Mjesuti, aliupokea ukweli wa ujio wa Yesu uliokuwa umekaribia. Ili aepuke karipio kutoka Kanisa la Roma, alichapisha kitabu chake kwa jina la bandia la Rabbi Bin Ezra, akijifanya Myahudi aliyeongoka. Mwaka 1825 kitabu chake kilitafsiriwa katika lugha ya Kiingereza. Kilisaidia kuimarisha mwamko ambao tayari ulishajionesha huko Uingereza. TK 230.4