Kama vile alivyofanya Yohana Mbatizaji, wahubiri hao waliweka shoka katika shina la mti na kuwahimiza wote “kuzaa matunda yapasayo toba.” Kinyume na hotuba za amani na usalama zilizokuwa zinasikika katika madhabahu maarufu, ushuhuda sahili wa Maandiko ulileta imani ambayo haikuwa rahisi kupingika. Wengi walimtafuta Bwana kwa toba. Mapenzi yaliyokuwa yamezama katika vitu vya duniani sasa yalielekezwa mbinguni. Wakiwa na mioyo iliyolainika na kunyenyekea waliungana kupaza sauti; “Mcheni Mungu, na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja.” TK 234.1
Wenye dhambi waliuliza huku wakilia: “Yanipasa nifanye nini ili nipate kuokoka?” Wale ambao hawakuwa waaminifu walikuwa wanahaha kutaka kufidia. Wote waliokuwa na amani katika Kristo walitamani kuona wengine wakifaidi baraka hizo. Mioyo ya wazazi iliwaelekea watoto wao, na mioyo ya watoto iliewaelekea wazazi wao. Malaki 4:5,6. Vikwazo vya kiburi na kusitasita viliondoka. Maungamo ya dhati yalifanyika. Kila mahali kulikuwa na mioyo inayomsihi Mungu. Wengi walikuwa wanakesha katika maombi wakitaka uhakika kama dhambi zao zimesamehewa, au kuombea ndugu na majirani zao waongoke. TK 234.2
Watu wa madaraja yote, matajiri kwa maskini, wakuu na wanyonge, walikuwa na shauku ya kulisikia fundisho la ujio Wakristo. Roho wa Mungu aliupatia nguvu ukweli wake. Uwepo wa malaika watakatifu ulihisiwa katika mikusanyiko hiyo ya watu, na walioamini walikuwa wanaongezeka kila siku. Makundi makubwa ya watu yalisikiliza maneno hayo muhimu kwa utulivu. Mbingu na dunia zilikuwa kana kwamba zimekaribiana. Watu walikwenda nyumbani kwao wakiwa na vinywa vilivyojaa sifa, na sauti ya furaha ilijaa katika hewa tulivu ya usiku. Hakuna hata mmoja aliyehudhuria mikutano hiyo ambaye angesahau matukio hayo makuu yaliyokuwa yanavutia. TK 234.3