Ukosefu wa uaminifu wa kanisa kwa Kristo kwa kuruhusu mambo ya kidunia yautawale moyo unafananishwa na kuvunja kiapo cha ndoa. Dhambi ya Israeli katika kumwacha Bwana imeelezewa kwa kielelezo kifuatacho: “Hakika kama vile mke amwachavyo mumewe kwa hiana, ndivyo mlivyonitenda mimi kwa hiana, Ee nyumba ya Israeli, asema Bwana.” Mmekuwa kama “mke wa mtu, aziniye! Akaribishaye wageni badala ya mumewe!” Yeremia 3:20; Ezekieli 16:32. TK 241.4
Mtume Yakobo anasema: “Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu.” Yakobo 4:4. TK 242.1
Mwanamke huyu (Babeli) alikuwa “amevikwa nguo ya rangi ya zambarau, na nyekundu, amepambwa kwa dhahabu, na kito cha thamani, na lulu, naye alikuwa na kikombe cha dhahabu mkononi mwake, kilichojawa na machukizo, na machafu ya uasherati wake. Na katika kipaji cha uso wake alikuwa na jina limeandikwa, la siri, Babeli mkuu, mama wa makahaba na machukizo ya nchi.” Babeli ni “mji ule mkubwa, wenyeufalme juu ya wafalme wa nchi.” Ufunuo 17:4-6, 18. TK 242.2
Mamlaka ambayo kwa kame nyingi ilikuwa inadhibiti wafalme katika nchi za Kikristo ni ile ya Kanisa la Roma. Rangi ya zambarau, na nyekundu, na dhahabu, na kito cha thamani, na lulu, vinaonesha utukufu ambao mamlaka ya Kanisa la Roma ilikuwa imejivika. Hakuna mamlaka nyingine inayoweza kuelezewa kwa usahihi kama mwanamke ambaye “amelewa kwa damu ya watakatifu, na kwa damu ya mashahidi wa Yesu” (Ufunuo 17:6) kama kanisa ambalo liliwatesa wafuasi Wakristo kikatili. TK 242.3
Babeli pia inatuhumiwa kwa kuwa na uhusiano batili na “wafalme wa dunia.” Kanisa la Kiyahudi lilipomwacha Bwana na kushikamana na wapagani, lilikuwa kahaba, na lile la Roma lilipotumia nguvu za kudunia linastahili hukumu hiyo hiyo. TK 242.4
“Babeli ni “mama wa makahaba.” Mabinti zake ni makanisa yanayoshikilia mafundisho yake na kufuata mfano wake wa kutelekeza ukweli ili yashikamane na ulimwengu. Ujumbe unaotangaza kuanguka kwa Babeli unahusu taasisi za kidini ambazo zilikuwa safi hapo mwanzo na sasa zimeasi. Kwa kuwa ujumbe unafuata baada ya ule ujumbe wa onyo la hukumu, basi unapasa kutolewa katika siku za mwisho. Hivyo hauwezi kulihusu Kanisa la Roma peke yake, kwani kanisa hilo limekuwepo katika hali ya kuanguka kwa kame nyingi. TK 242.5
Isitoshe, watu wa Mungu wanaitwa watoke Babeli. Kulingana na andiko hili, wengi wa watu wa Mungu bado wako ndani ya Babeli. Sehemu kubwa na wafuasi Wakristo wanapatikana katika taasisi zipi za kidini sasa hivi? Ni katika makanisa yanayokiri imani ya Kiprotestanti. Yalipoanzishwa makanisa haya yalikuwa na msimamo safi wa kutetea ukweli, na baraka za Mungu ziliambatana nayo. Ila yalianguka kwa tamaa ile ile iliyowaangusha Israeli—kuiga desturi na kufanya urafiki na wasiomcha Mungu. TK 243.1