Katika Ufunuo 14 ujumbe wa malaika wa kwanza unafuatiwa na malaika wa pili, anayesema “Umeanguka, umeanguka Babeli, mji ule ulio mkubwa, maana ndio uliowanyweshamataifa yote mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake.” Ufunuo 14:8. “Babeli” inamaanisha machafuko. Katika Maandiko inawakilisha mifumo mbalimbali ya diniza uongo au zilizoasi. Katika Ufunuo 17, Babeli inaelezewa kama mwanamke— kielelezo kitumikacho katika Biblia kuwakilisha kanisa, mwanamke safi huwakilisha kanisa safi; mwanamke fuska huwakilisha kanisa lililoasi. TK 241.2
Katika Biblia, uhusiano kati ya Kristo na kanisa lake unawakilishwa na ndoa. Bwana anasema: “Nami nitakuposa uwe wangu kwa milele; naam, nitakuposa kwa haki, na kwa hukumu, na kwa ufadhili, na kwa rehema.” “Rudini, enyi watoto wenye kuasi, asema Bwana; maana mimi ni mume wenu.” Naye Paulo asema: “Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi.” Hosea 2:19; Yeremia 3:14; 2 Wakorintho 11:2. TK 241.3