Kanisa lilianzaje kuuacha usahihi wa Injili? Kwa kukubaliana na upagani, ili Ukristo ukubalike na wapagani. “Kuelekea sehemu ya mwisho ya kame ya pili makanisa mengi yalichukua sura mpya. ... Wale wanafunzi wazee walipokuwa wanalala makaburini, watoto wao pamoja na waumini wapya...walikuja na kubadili kusudi la Injili” “Wimbi la wapagani liliingia kanisani, likiwa na utamaduni, desturi na saanamu zao. 220Robert Robinson. Ecclesiastical Researches (ed. 1792), ch. 6, par. 17, p. 51.. Dini ya Kikristo ikapata kibali na kuungwa mkono na watawala wa dunia. Ilipokelewa nusunusu na wengi. Lakini wengi “waliendelea kuwa wapagani kwa ndani, huku wakiabudu miungu yao kwa siri.” 221Gavazzi, Lectures (ed. 1854), p. 278. TK 244.1
Je, mchakato wa aina hiyo hiyo haujajirudia karibu katika kila kanisa linalojiita la Kiprotestanti? Waasisi wenye moyo halisi wa matengenezo wanapokufa, watoto wao “hubadili kusudi”. Kwa kuwa walikataa kupokea nuru yo yote zaidi ya ile waliyokuwa nayo baba zao, watoto wa wana-matengenezo waliuacha mfano wao wa kujikana nafsi na kuukataa ulimwengu. TK 244.2
Ni ajabu kwamba makanisa yetu maarufu yamekiacha kiwango cha Biblia! Akizungumzia pesa, John Wesley alisema: “Msipoteze sehemu yo yote ya talanta hii yenye thamani, kwa ajili ya mavazi aghali yasiyo ya lazima, au mapambo yasiyohitajika. Msipoteze sehemu yake katika kupamba nyumba kifahari; katika samani aghali; katika picha, au nakshi za dhahabu. Kadiri unavyoendelea kuvaa ‘nguo za rangi ya zambarau, na kitani safi, na kula siku zote kwa anasa,’ bila shaka wengi watasifia uzuri wa mwonekano wako, wema na ukarimu wako. Lakini ni bora uridhike na heshima itokayo kwa Mungu.” 222Wesley Works, Sermon 50, “The LJse of Money TK 244.3
Watawala, wanasiasa, wanasheria, madaktari, wafanya biashara, hujiunga na kanisa kama njia ya kuendeleza maslahi yao ya kidunia. Taasisi za kidini, zikitiwa nguvu na wapenda anasa hawa waliobatizwa, hujitahidi kutafuta umaarufu zaidi. Makanisa makubwa ya kifahari hujengwa. Mshahara mkubwa hulipwa kwa mchungaji mwenye kipawa kwa ajili ya kuburudisha watu. Hotuba zake lazima ziwe laini, za kupendeza katika masikio ya kisasa. Kwa njia hiyo dhambi zinazopendwa na wengi hufichwa katika utauwa wa bandia. TK 245.1
Mwandishi mmoja katika gazeti la New York Independent alisema hivi juu ya Umethodisti: “Tofauti kati ya watauwa na wasiokuwa na dini inatoweka taratibu na kuwa kama uvuli, na watu wenye ari wa pande zote wanajitahidi kuifuta tofauti iliyopo katika aina ya matendo na burudani zao.” TK 245.2
Katika wimbi hili la kutafuta anasa, kujikana nafsi kwa ajili ya Kristo kumekaribia kutoweka kabisa. “Kama pesa zinatakiwa sasa, ... watu wasiombwe kutoa. Labda uwe na maonesho ya biashara, maonesho ya picha, mahakama ya bandia, chakula cha kijadi au adimu, au chakula cho chote—kitu cho chote kinachoburudisha watu.” TK 245.3
Robert Atkins anaonesha taswira ya kuanguka kiroho huko Uingereza: “Uasi, uasi, uasi, umeandikwa mbele kabisa ya kila kanisa; na kama wangejua, kama wangeweza kuhisi, kungekuwa na tumaini, lakini sasa, wanasema, “mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu.” 223Second Advent Library, tract No. 39. TK 245.4
Dhambi kubwa ambayo Babeli inatuhumiwa ni kuwanywesha “mataifa yote mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake.” Kikombe hiki kinawakilisha mafundisho potovu ambayo imeyapokea kutokana na urafiki wake na dunia. Nayo kwa upande wake imekuwa na ushawishi kwa ulimwengu kwa kufundisha mafundisho yanayopingana na maelezo ya wazi ya Biblia. TK 245.5
Kama ulimwengu huu ungekuwa haujalewa mvinyo wa Babeli, wengi wangeamini na kuongolewa na ukweli dhahiri wa Neno la Mungu. Lakini imani ya dini inaonekana kuwa imechafuliwa na kukanganyika kiasi kwamba watu hawajui waamini nini. Dhambi ya ulimwengu kukosa toba imekaa mlangoni mwa Kanisa. TK 245.6
Ujumbe wa malaika wa pili haukutimia kikamilifu mwaka 1844. Wakati huo makanisa yalianguka kimaadili kwa kuikataa nuru ya ujumbe wa Ujio, lakini anguko hilo halikuwa kamilifu. Kadiri wanavyoendelea kuukataa ukweli maalum wa wakati huu wamekuwa wakianguka zaidi na zaidi. Hata hivyo bado haiwezi kusemwa kuwa “umeanguka Babeli, ... maana umewanywesha mataifa yote mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake.” Makanisa ya Kiprotestanti yanajumuishwa katika tangazo hilo la malaika wa pili. Lakini kazi ya uasi haijafikia kilele chake. TK 246.1
Kabla ya kuja kwa Bwana, Shetani atafanya kazi “kwa uwezo wote, na ishara na ajabu za uongo; na katika madanganyo yote ya udhalimu;” na wote ambao “hawakukubali kuipenda ile kweli, ili wapate kuokolewa,” wataachwa wapokee “nguvu ya upotevu, wauamini uongo.” 2 Wathesalonike 2:9-11. Kuanguka kwa Babeli kutakamilika pale muungano wa kanisa na ulimwengu utakapokuwa umekamilika. Badiliko hili ni la hatua kwa hatua na utimilifu wa Ufunuo 14:8 uko katika siku za usoni. TK 246.2
Pamoja na giza la kiroho lililo katika makanisa yanayounda Babeli, watu wengi walio wafuasi wa kweli Wakristo bado wako katika ushirika wa makanisa hayo. Wengi hawajauona ukweli maalumu wa wakati huu. Si wachache wanaotamani nuru zaidi. Wanatafuta bila mafanikio sura ya Kristo katika makanisa waliyojiunga nayo. TK 246.3
Ufunuo 18 inatuelekeza katika wakati ambao watu wa Mungu walioko Babeli watatakiwa kujitenga na Babeli. Ujumbe huu, ambao ni wa mwisho kutolewa kwa ulimwengu, utakamilisha kazi yake. Nuru ya ukweli itawaangazia wote ambao mioyo yao iko tayari kuipokea, na watoto wote wa Bwana walio Babeli watautii mwito huo: “Tokeni kwake, enyi watu wangu.” Ufunuo 18:4. TK 246.4