Wakati wa kwanza ambao Bwana alikuwa anatarajiwa kuja ulipopita—majira ya kuchipusha ya mwaka 1844—wale waliokuwa wametarajia kuonekana kwake walikuwa katika mashaka na wasiwasi. Wengi waliendelea kuyachunguza Maandiko, wakiupima upya ushuhuda wa imani yao. Ule unabii, uliokuwa wa wazi na usio na mashaka, ulikuwa unaonesha kwamba Ujio Wakristo ulikuwa umekaribia. Baraka za Bwana katika uongofu na uamsho miongoni mwa Wakristo ulikuwa umedhihirisha kuwa ule ujumbe ulikuwa umetoka mbinguni. Pamoja na unabii ambao walikuwa wameuchukulia kuwa ulikuwa unahusu wakati wa Ujio wa pili, kulikuwa na maelekezo yaliyokuwa yanawahimiza kungoja kwa subira wakiamini kwamba mambo ambayo yalikuwa giza katika ufahamu wao kwa sasa yangewekwa wazi. Kati ya unabii huo ulikuwapo ule wa Habakuki 2:1-4. Hata hivyo hakuna aliyegundua kuwa katika unabii huo kulikuwa na uchelewaji dhahiri—wakati wa kukawia. Baada ya kuvunjika moyo, andiko hili lilionekana kuwa na maana kubwa: “Njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia... Mwenye haki ataishi kwa imani yake.” TK 247.1
Unabii wa Ezekieli pia ulikuwa faraja kwa wale waumini: “Basi uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; ... Siku hizo ni karibu, na utimilizo wa maono yote. ... Maana mimi ni Bwana; mimi nitanena, na neno lile nitakalolinena litatimizwa; wala halitakawilishwa tena.” “Neno nitakalolinena litatimizwa, asema Bwana MUNGU.” Ezekieli 12:23-25, 28. TK 247.2
Wale waliokuwa wakisubiri walifurahi. Yeye anayeujua mwisho tangu mwanzo alikuwa amewapatia tumaini. Bila sehemu za Maandiko kama hizo, imani yao ingetoweka. TK 247.3
Ule mfano wa wanawali kumi wa Mathayo 25 pia unaonesha mambo yaliyowapata waliokuwa wanaamini juu ya Ujio. Katika mfano huo, linadhihirishwa kanisa la siku za mwisho. Mambo yaliyowapata yanaelezewa kwa matukio ya arusi ya watu wa Mashariki ya Kati. TK 247.4
“Ndipo ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali kumi, waliotwaa taa zao, wakatoka kwenda kumlaki bwana arusi. Watano wao walikuwa wapumbavu, na watano wenye busara. Wale waliokuwa wapumbavu waiizitwaa taa zao, wasitwae na mafuta pamoja nao; bali wale wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao. Hata bwana arusi alipokawia, wote wakasinzia wakalala usingizi. Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki.” Mathayo 25:1-6. TK 248.1
Ujio Wakristo, kama ulivyotangazwa na ujumbe wa malaika wa kwanza, ulieleweka kuwa ulikuwa unawakilishwa na Ujio wa bwana arusi. Matengenezo yaliyoenea kila mahali kutokana na tangazo la kuja kwa Kristo ambako kulikuwa kumekaribia, yalikuwa sawa na kutoka kwa wale wanawali. Katika mfano huu, wote walikuwa wamechukua taa zao, yaani Biblia, na walikuwa wamekwenda “kumlaki bwana arusi.” Lakini wale wapumbavu hawakutwaa “mafuta pamoja nao,” wale wenye busara “walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao.” Wale wenye busara walikuwa wamesoma Maandiko na kuujua ukweli na walikuwa wameguswa wao wenyewe, yaani walikuwa na imani ambayo isingeweza kushindwa kwa sababu ya kuvunjika kwa matumaini na kuchelewa. Wengine walikuwa wanasukumwa na msisimko, uliotokana na hofu iliyosababishwa na ule ujumbe. Lakini walikuwa wanategemea imani ya ndugu zao, wakiwa wameridhika na mwanga hafifu wa mihemko, bila kuwa na ufahamu kamili wa ukweli au kazi halisi ya neema ndani ya moyo. Hawa walikuwa wamekwenda kumlaki bwana arusi wakitarajia tuzo ya haraka lakini hawakuwa tayari kukutana na ucheleweshaji na kuvunjika kwa matumaini. Imani yao ilizimia. TK 248.2
“Hata bwana arusi alipokawia, wote wakasinzia, wakalala usingizi.” Kukawia kwa bwana arusi kunawakilisha kupita kwa ule muda, kuvunjika kwa matumaini na kile kilichoonekana kama uchelewaji. Wale ambao imani yao ilikuwa imejengwa katika ujuzi binafsi wa Biblia walikuwa na mwamba chini ya miguu yao ambao mawimbi y kuvunjika kwa matumaini yasingeweza kuuhamisha. “wote wakasinzia, wakalala usingizi,” kundi moja likiwa limeiacha imani, na lingine likingoja kwa subira hadi nuru kubwa zaidi itakapotolewa. Wale waliokuwa na imani ya juu juu wasingeweza tena kutegemea imani ya ndugu zao. Kila mtu alitakiwa kusimama au kuanguka mwenyewe. TK 248.3