Mle patakatifu mlikuwa na kinara cha taa upande wa kusini kikiwa na taa zake saba zilizokuwa zinatoa nuru usiku na mchana; upande wa kaskazini kulikuwa na meza ya mikate ya wonyesho. Mbele ya pazia lililokuwa linatenganisha patakatifu na patakatifu sana, kulikuwa na madhabahu ya dhahabu ya kufukizia uvumba, ambapo wingu la manukato lilikuwa linapanda pamoja na maombi ya wana wa Israeli kwenda mbele za Mungu kila siku. TK 257.2
Baada ya Waebrania kukaa katika nchi ya Kanaani, ile hema ilibadilishwa na kujengwa hekalu la Sulemani, ambalo, pamoja na kuwa jengo la kudumu, na kubwa zaidi, lilikuwa na uwiano ule ule na lilikuwa na samani zile zile. Patakatifu paliendelea kuwa hivyo mpaka palipoharibiwa na Warumi mwaka wa 70 B.K., isipokuwa wakati palipokuwa gofu wakati wa Danieli. Hapa ni patakatifu pekee duniani ambapo panazungumziwa na Biblia, patakatifu pa agano la kwanza. Lakini je, agano jipya halina patakatifu? TK 257.3
Walipokiangalia tena kitabu cha Waebrania, wale waliokuwa wanatafuta ukweli waligundua kwamba patakatifu pengine au patakatifu pa agano jipya palikuwa panagusiwa katika maneno yaliyokwisha kunukuliwa; “Basi hata agano la kwanza lilikuwa na kawaida za ibada, na patakatifu pake, pa kidunia.” (Ebr. 9:1). TK 257.4
Walipoangalia mwanzoni mwa sura ya nyuma yake, walisoma: “Tunaye kuhani mkuu wa namna hii,aliyeketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha ukuu mbinguni, mhudumu wa patakatifu, na wa ile hema ya kweli, ambayo Bwana aliiweka wala si mwanadamu.” Waebrania 8:1,2. TK 257.5
Hapa panaoneshwa patakatifu pa agano jipya. Patakatifu pa agano la kwanza palijengwa na Musa; patakatifu pa sasa pamejengwa na Bwana. Katika patakatifu pa kwanza, walikuwa wanahudumu makuhani wa kidunia; katika patakatifu pa pili Kristo, Kuhani wetu Mkuu anahudumu akiwa mkono wa kulia wa Mungu. Patakatifu pa kwanza palikuwa duniani, na pa pili pako mbinguni. TK 258.1
Hema iliyojengwa na Musa ilijengwa kulingana na mfano. Bwana alielekeza: “Sawasawa na haya yote nikuonyeshayo, mfano wa maskani, na mfano wa vyombo vyake vyote, ndivyo mtakavyovifanya.” “Nawe angalia ya kwamba uvifanye kama mfano wake, ulioonyeshwa mlimani.” Hema ya kwanza ilikuwa “mfano wa wakati huu uliopo sasa; wakati huo sadaka na dhabihu zinatolewa,” na patakatifu pake palikuwa “nakala za mambo yaliyo mbinguni.” Makuhani walihudumu kama “mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni.” ” Kristo hakuingia katika patakatifu palipofanyika kwa mikono, ndio mfano wa patakatifu halisi; bali aliingia mbinguni hasa, aonekane sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu.” Kutoka 25:9, 40; Waebrania 9:9, 23; 8:5; 9:24. TK 258.2
Patakatifu pa mbinguni ni patakatifu chanzi na patakatifu palipojengwa na Musa palikuwa nakala yake. Utukufu wa ile hema ya duniani ulikuwa unaakisi utukufu wa lile hekalu la mbinguni ambapo Kristo anahudumu kwa ajili yetu mbele ya kiti cha enzi cha Mungu. Ukweli muhimu juu ya patakatifu pa mbinguni na wokovu wa mwanadamu ulifundishwa kwa kutumia patakatifu pa duniani pamoja na huduma zake. TK 258.3