Vyumba viwili vya patakatifu pa mbinguni vinawakilishwa na vile vyumba viwili katika patakatifu pa duniani. Yohana alioneshwa hekalu la Mungu kule mbinguni. Aliona “taa saba za moto zikiwaka mbele ya kile kiti cha enzi.” Aliona malaika “mwenye chetezo cha dhahabu, akapewa uvumba mwingi, ili autie pamoja na maombi ya watakatifu wote juu ya madhabahu ya dhahabu, iliyo mbele ya kiti cha enzi.” Ufunuo 4:5; 8:3. Hapa nabii huyu alikuwa anaona chumba cha kwanza cha patakatifu pa mbinguni; na hapo aliona “taa saba za moto” na “madhabahu ya dhahabu,” vilivyokuwa vinawakilishwa na kinara cha taa cha dhahabu na madhabahu ya kufukizia uvumba katika patakatifu pa duniani. TK 258.4
“Hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa” tena, na akatazama ndani ya pazia katika patakatifu sana. Hapo aliona “sanduku la agano” lililokuwa linawakilishwa na sanduku lililokuwa limetengenezwa na Musa kwa ajili ya kuwekea sheria ya Mungu. Ufunuo 11:19. Kwa hiyo wale waliokuwa wanachunguza suala hili walipata ushahidi wa kuwepo kwa patakatifu mbinguni. Yohana anashuhudia kuwa alipaona. TK 259.1
Katika lile hekalu la mbinguni, ndani ya patakatifu sana, kuna sheria ya Mungu. Sanduku linalohifandhi sheria hiyo limefunikwa kwa kiti cha rehema, ambacho Kristo anasimama mbele yake na kusihi kwa damu yake kwa niaba ya mwenye dhambi. Kwa njia hiyo, muungano wa haki na rehema vinawakilishwa katika mpango wa ukombozi, mwungano unaoifanya mbungu yote istaajabu. Hii ndiyo siri ya rehema ambayo malaika wanatamani kuitazama—kwamba Mungu anaweza kuwa mwenye haki na wakati huo huo akamhesabia haki mwenye dhambi atubuye, kwamba Kristo aliweza kuinama ili awainue wengi kutoka katika uharibifu na kuwavika mavazi safi ya haki yake mwenyewe. TK 259.2
Kazi ya Kristo kama mwombezi wa mwanadamu inaelezewa katika Zekaria: “Tazama, mtu huyu ndiye ambaye jina lake ni Chipukizi; naye atakua katika mahali pake, naye atalijenga hekalu la Bwana. Naam, yeye atalijenga hekalu la Bwana; naye atauchukua huo utukufu; ataketi akimiliki katika kiti chake cha enzi; na kutakuwa na kuhani katika kiti chake cha enzi; na shauri la amani litakuwa kati ya hao wawili.” Zekaria 6:12,13. TK 259.3
“Naam, yeye atalijenga hekalu la Bwana.” (Zekaria 6:12): Kwa njia ya dhabihu yake na upatanishi wake, Kristo ni msingi na mjenzi wa kanisa la Mungu, “jiwe kuu la pembeni ambalo katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana.” Waefeso 2:20, 21. TK 259.4
“Naye atauchukua huo utukufu.” (Zekaria 6:13): Wimbo wa waliokombolewa utakuwa: “Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake. . . utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina.” Ufunuo 1:5,6. TK 259.5
“Ataketi akimiliki katika kiti chake cha enzi; na kutakuwa na kuhani katika kiti chake cha enzi” (Zekaria 6:13): Ufalme wa utukufu haujaanza bado. Kazi yake kama mwombezi itakapokoma ndipo Mungu atakapamkabidhi ufalme ambao “utakuwa hauna mwisho.” Luka 1:33. Sasa hivi Kristo amekaa pamoja na Baba katika kiti chake cha enzi kama kuhani. Katika kiti hicho cha enzi amekaa yeye “ayachukuaye masikitiko yetu, amejitwika huzuni zetu,” ambaye “alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi,” ili aweze “kuwasaidia wao wanaojaribiwa.” Isaya 53:4; Waebrania 4:15; 2:18. Ile mikono yenye majeraha, ubavu uliochomwa, miguu iliyoumizwa, inasihi kwa ajili ya mwanadamu aliyeanguka ambaye ukombozi wake ulinunuliwa kwa gharama hiyo. TK 260.1
“Na shauri la amani litakuwa kati ya hao wawili.” (Zekaria 6:13): Upendo wa Baba ni Chemchemi ya wokovu kwa jamii ya waliopotea. Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “Baba mwenyewe awapenda ninyi.” Mungu “alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake.” “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” Yohana 16:27; 2 Wakorintho 5:19; Yohana 3:16. TK 260.2