“Hema ya kweli” iliyo mbinguni ndiyo patakatifii pa agano jipya. Wakati Kristo alipokufa huduma kielelezo zilikoma. Kwa kuwa Danieli 8:14 ilitimia katika kipindi cha agano jipya, basi patakatifu panapozungumziwa hapa ni lazima pawe pa agano jipya. Kwa hiyo unabii unaosema “Hata nyakati za jioni na asubuhi elfu mbili na mia tatu; ndipo patakatifu patakapotakaswa,” unahusu patakatifu pa mbinguni. TK 260.3
Lakini kutakaswa kwa patakatifu ni nini? Je, kunaweza kukawa na kitu cho chote cha kutakaswa mbinguni? Katika Waebrania 9 kutakaswa kwa patakatifu pa duniani na patakatifu pa mbinguni panaelezewa: “Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo. Basi ilikuwa sharti nakala za mambo yaliyo mbinguni zisafishwe kwa hizo, lakini mambo ya mbinguni yenyewe yasaflshwe kwa dhabihu zilizo bora kuliko hizo” (Waebrania 9:22, 23), yaani damu ya Kristo iliyo na thamani. TK 260.4