Utakasaji katika huduma halisi sharti ufanyike kwa damu ya Kristo. “na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo.” Kuondoa dhambi ndiyo kazi inayopasa kufanyika. TK 261.1
Lakini ingewezekana vipi kukawa na dhambi inayohusiana na hekalu la mbinguni? Jambo hili linaweza kueleweka kwa kuangalia ile huduma kielelezo, kwa kuwa makuhani wa duniani walihudumu kama “mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni.” Waebrania 8:5. TK 261.2
Huduma katika patakatifu pa duniani ilikuwa na sehemu mbili. Makuhani walikuwa wanahudumu kila siku katika chumba cha patakatifu, na mara moja kwa mwaka kuhani mkuu alikuwa anafanya kazi maalum ya upatanisho katika chumba cha patakatifu sana, kwa ajili ya kupatakasa patakatifu. Kila siku mwenye dhambi alikuwa analeta dhabihu yake na kuweka mikono yake juu ya kichwa cha mhanga huyo akiungama dhambi zake, kama kielelezo cha kuzihamisha kutoka kwake kwenda kwa ile dhabihu isiyo na hatia. Kisha yule mnyama alikuwa anauawa. “Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu.” Walawi 17:11. Sheria ya Mungu iliyokuwa imevunjwa ilikuwa inahitaji uhai wa mkosaji. Damu, inayowakilisha uhai wa mwenye dhambi ambaye hatia yake ilikuwa inachukuliwa na yule mhanga, ilikuwa inapelekwa na kuhani katika chumba cha patakatifu na kunyunyiziwa mbele ya pazia, ambalo nyuma yake kulikuwa sheria ambayo mwenye dhambi alikuwa ameivunja. Kwa utaratibu huu dhambi ile ilikuwa kana kwamba imehamishiwa patakatifu. Wakati mwingine ile damu ilikuwa haipekekwi katika chumba cha patakatifii, bali nyama ilikuwa inaliwa na kuhani. Utaratibu wote huu ulikuwa unawakilisha kuhamishwa kwa dhambi kutoka kwa mtu aliyetubu kwenda patakatifu. TK 261.3
Hiyo ndiyo kazi iliyokuwa inafanyika mwaka mzima. Dhambi za Israeli zilikuwa zinahamishiwa patakatifu kwa njia hiyo, na hivyo kazi maalum ya kuziondoa ilikuwa inahitajika. TK 261.4