Pambano kuu kati ya Kristo na Shetani litakwisha muda si mrefu, yule mwovu anaongeza juhudi yake maradufu ili kuishinda kazi ya Kristo kwa niaba ya mwanadamu. Lengo analotaka kulitimiza ni kuwashikilia watu gizani na kuwafanya wasitubu hadi kazi ya Mwokozi ya maombezi imekwisha. TK 319.1
Kutojali kunapoenea kanisani, Shetani hasumbuliwi na jambo hilo. Lakini wakati nafsi za watu zinapojiuliza, “Nifanye nini ili niokolewe?” yupo uwanjani kwa ajili ya kulinganisha nguvu zake dhidi ya Kristo na kupinga mvuto wa Roho Mtakatifu. TK 319.2
Katika tukio moja ambapo malaika walijihudhurisha, Shetani pia alikuja kati yao, siyo kwa lengo la kumsujudia Mfalme wa milele, bali kuendeleza makusudi yake mabaya dhidi ya haki. Angalia Ayubu 1:6. Huwa anakuwepo pale wanadamu wanapokusanyika kufanya ibada, akifanya kazi kwa juhudi kudhibiti mioyo ya wale wanaoabudu. Anapomwona mjumbe wa Mungu akichunguza Maandiko, huliwekea alama somo litakalotolewa. Kisha hutumia ujanja na werevu wake ili kwamba ujumbe usiwafikie wale ambao anawadanganya kuhusiana na somo lile. Yule ambaye atalihitaji sana lile onyo atasukumwa kuwa na jambo fulani la kufanya ama kwa njia yoyote nyingine atazuiwa kusikiliza neno. TK 319.3
Shetani anahakikisha kuwa watumishi wa Bwana wamelemewa kwa sababu ya giza linalowagubika watu. Anasikia maombi yanayotolewa kwa ajili ya neema ya Mungu na uwezo wa kuvunja hali ya kutojali na uvivu. Kisha kwa juhudi mpya huwajaribu wanadamu kwa njia ya uchu wa chakula ama kwa kufurahisha tamaa zao binafsi, na hivyo kupumbaza ufahamu wao ili wasisikie yale mambo wanayohitaji zaidi kujifunza. TK 319.4
Shetani anajua kwamba wale wote wanaopuuzia maombi na Maandiko watashindwa kwa mashambulizi yake. Kwa hiyo anabuni kila mbinu iwezekanayo kuishughulisha akili. Mawakala wake wanatenda kazi kwa bidii wakati Mungu awapo kazini. Huwawasilisha wale watumishi waaminifu Wakristo na wale wanaojikana nafsi kana kwamba wamedanganyika ama ni wadanganyifu. Ni kazi yao kupotosha nia ya kila tendo jema, kusambaza visingizio na kuamsha mashaka ndani ya moyo ya wale wasio na uzoefu. Hata hivyo inaweza kuonekana kwa urahisi kwamba ni watoto wa nani, ni mfano wa nani wanaufuata, na ni kazi ya nani wanaifanya. “Mtawatambua kwa matunda yao.” Mathayo 7:16; pia Angalia Ufunuo 12:10. TK 319.5