Mdanganyifu mkuu ana mafundisho mengi aliyoyatayarisha yaliyo kinyume na ukweli kufaa vionjo mbalimbali vya wale ambao angeweza kuwaangamiza. Ni mpango wake kuleta ndani ya kanisa mambo ya unafiki na yasiyo na wongofu ambayo yatachochea mashaka na kutoamini. Wengi ambao hawana imani kwa Mungu wanazikubali baadhi ya kanuni za ukweli na kukubalika kama Wakristo, na hivyo kuwezeshwa kuingiza makosa kuwa sehemu ya mafundisho ya msingi. Shetani anajua kuwa ukweli ukipokelewa kwa upendo, utaitakasa nafsi. Kwa hiyo badala ya Injili, anaweka nadharia potovu na hadithi za kubuni. Tangu mwanzo, watumishi wa Mungu walipambana na walimu wa uongo, siyo tu kama watu waovu, bali kama wafundishaji wa uongo unaofisha nafsi. Eliya, Yeremia, na Paulo walisimama imara kuwapinga wale waliokuwa wakiwageuza watu kutoka kwenye Neno la Mungu. Uhuru ule unaoichukulia imani sahihi kuwa siyo kitu muhimu haukukubaliwa na watetezi watakatifu wa ukweli. TK 320.1
Fasili za Maandiko zenye mashaka na zenye mawazo yanayopendelewa pamoja na nadharia zinazokinzana katika ulimwengu wa Kikristo ni kazi ya adui yetu mkuu ili kuichanganya mioyo. Kutokubaliana pamoja na migawanyiko miongoni mwa makanisa kwa sehemu kubwa ni kwa sababu ya upotoshaji wa Maandiko ili kuunga mkono nadharia inayopendwa. TK 320.2
Ili kuyasimamisha mafundisho potovu, wengine huchukua aya za Maandiko zikiwa zimeondolewa kwenye muktadha wake, wananukuu sehemu ya aya ili ifae kuthibitishwa hoja zao wakati sehemu ya aya inayosalia huonesha maana iliyo kinyume chake. Kwa kutumia ujanja wa nyoka wanajikita wakiwa na maneno yasiyo na muunganiko yaliyotengenezwa ili yafae kwa ajili ya kuifaa tamaa ya mwili. Wengine huchukua michoro na vielezo na kuvipa tafsiri zinazoyafaa mawazo wanayoyapendelea, wakizingatia kidogo tu ushuhuda wa Maandiko kujitafsiri yenyewe, na kisha kuyaleta mashaka yao kama mafundisho ya Biblia. TK 320.3