Wakati ambapo kujifunza Maandiko kutafanywa bila roho ya maombi na inayokubali kufundishwa fungu lililo wazi sana litapotoshwa kutoka kwenye maana yake ya kweli.Biblia nzima ni lazima iletwe kwa watu kama inavyosomeka. TK 321.1
Mungu alilitoa neno la unabii lililo imara; malaika na hata Kristo mwenyewe alikuja kumfahamisha Danieli na Yohana mambo ambayo kwamba, “hayana budi kuwako upesi” Ufunuo 1:1. Mambo makubwa yanayohusu wokovu wetu hayakufunuliwa katika hali ya kutatanisha na kumpotosha mtu anayeutafuta ukweli kwa uaminifu. Neno la Mungu liko wazi kwa wote wanaojifunza kwa moyo wa maombi. TK 321.2
Kwa ajili ya kilio cha uhuru, watu wamepofushwa wasione mbinu za adui yao. Yeye amefanikiwa kuuweka ubahatishaji wa wanadamu mahali pa Biblia; sheria ya Mungu imewekwa kando ; na makanisa yako chini ya utumwa wa dhambi huku yakidai kuwa yako huru. TK 321.3
Mungu ameruhusu nuru kubwa katika ulimwengu kwa ajili ya uvumbuzi wa kisayansi. Lakini hata uwezo huo wa juu wa akili, kama hautaongozwa na Neno la Mungu, utatatizwa katika majaribio ya kuchunguza uhusiano wa sayansi na Ufunuo. TK 321.4
Mwanadamu anajua kwa sehemu, ufahamu wake siyo mkamilifu; Kwa hiyo wengi hawawezi kupatanisha mitazamo yao ya sayansi na Maandiko. Wengi wanazikubali nadharia tu kama kweli za kisayansi, na wanadhani kuwa Neno la Mungu linapaswa kuhakikiwa kwa, “...elimu iitwayo elimu kwa uongo” 1 Timotheo 6:20. Kwa sababu hawawezi kumwelezea Mwumbaji na kazi zake kwa kutumia sheria za asili; historia ya Biblia imechukuliwa kuwa haiaminiki. Wale wanaotilia mashaka Agano la Kale na Agano Jipya, wanapiga hatua nyingine mbele na kutilia mashaka uwepo wa Mungu. Kwa sababu wameacha nanga yao, wamebaki wakigonga mwamba wa kutoamini. TK 321.5
Ni kazi ya usanifu wa udanganyifu wa Shetani kuwafanya wanadamu waendelee kukisia maana ya mambo ambayo Mungu hakuyafunua. Lusifa hakuridhika kwa sababu siri zote za makusudi ya Mungu hakupewa yeye, na alipuuzia kile kilichokuwa kimefunuliwa. Na sasa anatafuta kuwajaza wanadamu roho ile ile na kuwaongoza wao pia kutozingatia amri za Mungu. TK 322.1
Kwa kadiri mafundisho yasiyokuwa ya kiroho na yenye msukumo kidogo wa kujikana nafsi yanavyozidi kutolewa, ndivyo yatakavyopendwa na kupokelewa kwa nguvu zaidi. Shetani yuko tayari kutimiza shauku ya moyo, na kushawishi hadi uongo utakapochukua nafasi ya ukweli. Hivyo ndivyo ilivyokua hadi utawala wa Papa ukapata nguvu juu ya mioyo ya wanadamu. Na kwa kuukataa ukweli kwa vile unahusisha msalaba; Waprotestanti wanaifuata njia ie ile. Wote wanaojifunza urahisi na sera, ili wasitofautiane na dunia; wataachwa kupokea, “uharibifu usiokawia” 2 Petro 2:1. Yule anayetishwa kwa udanganyifu mmoja ataupata mwingine mara moja, “Kwa hiyo Mungu awaletea nguvu ya upotevu, wauamini uongo; ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu.” 2 Wathesalonike 2:1,12. TK 322.2