Shetani, ambaye alichochea uasi mbinguni, alitamani kuwashawishi wakazi wa dunia katika vita vyake dhidi ya Mungu. Adamu na Hawa walikuwa na furaha kamilifu kwa kuitii sheria ya Mungu-ushuhuda wa daima dhidi ya madai aliyoyatoa Shetani mbinguni kwamba sheria ya Mungu ilikuwa ya ukandamizaji. Shetani alikuwa ameazimu kusababisha anguko lao, ili aimiliki dunia, na auanzishe ufalme wake hapa kinyume na Aliye juu. TK 327.1
Adamu na Hawa walikuwa wameonywa kuhusu adui huyu wa hatari, lakini alitenda kwa kificho, akilifunika kusudi lake. Akimtumia nyoka kuwa chombo chake, wakati huo akiwa kiumbe mwemye mwonekano wa kuvutia, alimwuliza Hawa: “Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani?” Hawa alijihatarisha kwa kuzungumza naye na akawa mhanga wa hila zake: “Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa. Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya” Mwanzo 3:1-5. TK 327.2
Hawa akakubali kushindwa, na kwa mvuto wake Adamu akashawishika kuingia dhambini. Waliyakubali maneno ya nyoka; walimwonea shaka Mwumbaji wao na walifikiri kuwa alikuwa anauwekea mipaka uhuru wao. TK 327.3
Lakini kwa Adamu maneno; “kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.”, yalikuwa yanamaanisha nini?. Je, angeingizwa kwenye maisha ya juu zaidi? Adamu hakuona kuwa hii ndiyo maana ya kauli ya Mungu. Mungu alitamka kuwa mwanadamu alilazimika kurudi mavumbini ikiwa ni adhabu ya dhambi zake: “...u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.” Mwanzo 3:19. Maneno ya Shetani, “...mtafumbuliwa macho”, yalithibitika kuwa kweli kwa maana hii tu: macho yao yalifumbuliwa ili watambue upuuzi wao. Waliyajua mabaya na wakalionja tunda chungu la uasi. TK 327.4
Mti wa uzima ulikuwa na uwezo wa kuudumisha uhai. Adamu angeweza kuendelea kuwa na fursa ya uhuru wa kuufikia mti huu na kuwa hai milele, lakini alipotenda dhambi alizuiliwa mti wa uzima na kuwa mwenye kupatwa na mauti. Hali ya kutokufa iliondolewa kwa sababu ya uasi. Hakungekuwa na tumaini kwa jamii iliyoanguka, endapo Mungu, kwa njia ya kafara ya Mwanawe, asingeisogeze hali ya kutokufa karibu nao. Wakati dhambi iliwafikia, “watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi,” Kristo aliufunua “uzima na hali ya kutokufa, kwa njia ya Injili.” Ni kwa njia ya Kristo pekee hali ya kutokufa inaweza kupatikana. “Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima.” Warumi 5:12; 2Timotheo 1:10; Yohana 3:36. TK 328.1