Kanuni za ukweli zilikuwa zinathaminiwa kuliko nyumba, ardhi, marafiki, ndugu na hata uhai wenyewe. Tangu mapema katika utoto, vijana walikuwa wanafimdishwa kuheshimu na kutambua utakatifu wa matakwa ya sheria ya Mungu. Nakala za Biblia zilikuwa adimu; kwa sababu hiyo, maneno haya ya thamani yalikuwa yanakaririwa. Wengi walikuwa wanaweza kukariri sehemu kubwa za Agano la Kale na Jipya. TK 46.1
Tangu utotoni walikuwa wamefundishwa kustahimili matatizo na kufikiri na kutenda wao wenyewe. Walikuwa wamefundishwa kubeba majukumu, kuwa waangalifu katika usemi, na kuelewa hekima ya kuwa kimya. Neno moja tu la siri lingefika masikioni mwa adui zao lingehatarisha maisha ya mamia ya ndugu, kwani maadui wa ukweli walikuwa waawafuatilia kama mbwa mwitu, wale waliokuwa wanathubutu kujipatia uhuru wa imani ya kidini. TK 46.2
Wawaldensia walihangaikia chakula chao kwa uvumilivu mkubwa. Kila eneo la ardhi lililopatikana kati ya milima lilitumiwa vema na kwa uangalifu. Uchumi na kujikana nafsi vilikuwa miongoni mwa elimu ambayo ilitolewa kwa watoto . Mchakato ulikuwa mgumu lakini wenye manufaa, ule ambao mwanadamu anauhitaji katika hali yake ya dhambi. Vijana walikuwa wanafundishwa kwamba nguvu zao zote zilikuwa za Mungu, na kwamba iliwapasa kuziendeleza kwa ajili ya kazi yake. TK 46.3
Makanisa ya wafuasi wa Wawaldensia yalikuwa yanafanana na kanisa la wakati wa mitume. Waliiamini Biblia kama mamlaka pekee isiyoweza kukosea huku wakipinga mamlaka ya Papa na maaskofu. Kinyume na mapadre wa kimwinyi wa Kanisa la Roma, wachungaji wao walililisha kundi la Mungu, wakilingoza kwenye malisho mabichi na chemchemi hai za Neno lake Takatifu. Watu walikuwa hawakutani kwenye makanisa ya fahari au makubwa, bali kwenye mabonde ya milima ya Alps, na wakati wa hatari, walikuwa wanakutana kwenye ngome za miamba, kusikiliza maneno ya ukweli kutoka kwa watumishi Wakristo. Wachungaji walikuwa hawahubiri Injili tu, lakini pia walikuwa wakiwatembelea wagonjwa, pia walikuwa wanafanya kazi ya kuhimiza umoja na upendo wa kidugu. Kama Paulo, fundi wa mahema, kila mmoja alijifunza ufundi fulani kwa ajili ya kujikimu. TK 46.4
Vijana walipata mafunzo kutoka kwa wachungaji wao. Biblia ndiyo ilikuwa somo lao kuu. Injili za Mathayo, Yohana pamoja na nyaraka nyingine nyingi zilikaririwa. TK 47.1
Maandiko Matakatifu yaliandikwa bila kuchoka, fungu kwa fungu, wakati mwingine wakijimulikia kwa myenge kwenye mapango yenye giza. Malaika toka mbinguni waliwazingira hawa wafanyakazi waaminifu. TK 47.2
Shetani alikuwa amewashawishi mapadre na maaskofu wa mamlaka ya Papa kulifukia Neno la ukweli kwenye takataka za uongo na imani za mapokeo potovu. Lakini kwa namna ya ajabu, lilihifadhiwa bila kuharibiwa katika kipindi chote cha zama za giza. Kama ilivyokuwa safina katika vilindi vya mawimbi makubwa, Neno la Mungu hushindana na dhoruba zinazotishia kuliangamiza. Kama vile mgodi ulivyo na mikondo ya dhahabu au fedha iliyofichika chini ya ardhi, ndivyo Maandiko Matakatifu yalivyo na hazina ya ukweli unaoonekana kwa mtafuataji mnyenyekevu mwenye maombi. Mungu alikuwa amekusudia Biblia iwe kitabu cha kujifunzia kwa wanadamu wote, kama njia ya kujifunua yeye mwenyewe. Kila ukweli unaoonekana ni ufunuo mpya wa tabia ya Mtunzi wa Biblia. TK 47.3
Kutoka katika shule zao kule milimani, baadhi ya vijana walipelekwa kwenye vyuo kule Ufaransa na Italia, ambako kulikuwa na uwanja mpana zaidi wa kujifunza na uchunguzi kuliko katika Milima yao ya Alps. Vijana waliokuwa wanapelekwa huko walikuwa wanakutana na majaribu. Walikuwa wanakutana na mawakala wa Shetani ambao TK 47.4
walikuwa wanashawishi kukubaliana na uasi uliofichika na udanganyifu hatari. Lakini elimu yao kutoka utoto ilikuwa imewaandaa kwa ajili ya jambo hilo. TK 47.5
Katika shule walizokuwa wanakwenda, hawakutakiwa kumwamini mtu ye yote. Mavazi yao yalikuwa yametengenezwa kwa namna ambayo yangeweza kuficha hazina yao kuu—Maandiko. Kila walipoweza, waliweka kwa uangalifu sehemu za Maandiko katika njia za wale ambao mioyo yao ilikuwa tayari kupokea ukweli. Watu waliongolewa kuufuata ukweli katika vyuo hivi, na mara nyingi kanuni za ukweli zilienea shule nzima. Hata hivyo viongozi wa mamlaka ya Papa walishindwa kufuatilia chanzo cha kile walichokiita “uasi” uharibuo. TK 48.1