Lakini watu wa Mungu hawatapotoshwa. Mafundisho ya kristo huyu wa uongo hayapatani na Maandiko Matakatifu. Baraka zake zinatolewa kwa wale wanaomwabudu mnyama na sanamu yake, kundi lile lile ambalo Biblia inasema watakinywea kikombe cha ghadhabu ya Mungu isiyochanganywa na maji. TK 376.1
Zaidi ya hayo, Shetani hataruhusiwa kufanya udanganyifu wa namna ujio Wakristo utakavyokuwa. Kristo amewaonya watu wake dhidi ya udanganyifu juu ya jambo hili. “Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule.. .Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki. Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.” Mathayo 24:24-27. Angalia pia Mathayo 25:31; Ufunuo 1:7; 1 Wathesalonike 4:16,17; Ujio huu, hakuna uwezekano wa kuupotosha. Utashuhudiwa na dunia yote. TK 376.2
Ni wanafunzi tu wenye bidii ya kujifunza Maandiko ambao wamepokea upendo wa kweli watakaosimama imara dhidi ya udanganyifu unaouteka ulimwengu. Kwa ushuhuda wa Biblia hawa watamtambua mdanganyifu katika hila zake. Je watu wa Mungu wameimarika vilivyo katika neno lake kiasi cha kutoshawishiwa na ushahidi wa akili zao? Je, katika zahama kama hii wataing’ang’ania Biblia, na Biblia pekee? TK 376.3
Kwa vile tamko litakalotolewa na viongozi mbalimbali wa ulimwengu wa Ukristo dhidi ya washika amri litapelekea kuondolewa kwa ulinzi wa serikali na kuwaacha mikononi mwa wale wanaotaka kuwaharibu; watu wa Mungu watakimbia kutoka kwenye miji na vijiji kujiunga pamoja kwenye makundi, wakiishi mahali palipo ukiwa na upweke kabisa.. Wengi watatafuta makao katika maeneo ya milimani, kama Wakristo wa mabonde ya Piedmont. (Angalia sura ya nne). Lakini watu wengi kutoka mataifa yote na madaraja mbalimbali, wa hali ya juu na ya chini, maskini na matajiri,, weupe na weusi, watatupwa katika utumwa usio wa haki na wa kikatili. Wapendwa wa Bwana watapitia katika siku za kuchosha wakifungwa magerezani, watahukumiwa kuchinjwa, wataachwa wafe gizani katika magereza ya ardhini. TK 376.4
Je, Bwana atawasahau watu wake katika saa hii ya kujaribiwa? Je, aliwasahau watu wakewaaminifu Nuhu, Lutu, Yusufu, Eliya, Yeremia au Danieli? Japo adui awatupa gerezani, lakini kuta za gereza la ardhini, hataweza kukata mawasiliano kati ya roho zao na Kristo. Malaika watawaijia kwenye vyumba hivyo vyenye upweke. Gereza litakuwa kama ikulu, kuta zitaangaziwa nuru kama ilivyokuwa kwa Paulo na sila walipoimba usiku wa manane katika gereza kule Filipi. TK 377.1
Hukumu ya Mungu itawaangukia wale wanaotafuta kuwaangamiza watu wake. Kwa Mungu hukumu ni “tendo la ajabu.” Isaya 28:21; Angalia pia Ezekieli 33:11. “Bwana, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli; mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi; wala si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe.” Kutoka 34:6,7; Nahumu 1:3. Taifa ambalo amelivumilia na ambalo limekijaza kikombe cha uharibifu wake hatimaye litakunywa kikombe cha ghadhabu ya Mungu kisichochanganywa na rehema. TK 377.2
Kristo atakapoacha kufanya upatanisho katika patakatifu pa mbinguni, ghadhabu isiyochanganywa na maji dhidi ya wale wanaomwabudu mnyama itamwagwa. Mapigo kule Misri yalifanana na hukumu zile zilizokuwa za kutisha ambazo ndizo zitakazoupata ulimwengu kabla ya ukombozi wa mwisho wa watu wa Mungu. Mwandishi wa Ufunuo anasema: “Pakawa na jipu baya, bovu, juu ya wale watu wenye chapa ya huyo mnyama, na wale wenye kuisujudia sanamu yake.” Bahari, “ikawa damu kama damu ya mfu ... mito na chemchemi za maji; zikawa damu.” na malaika akasema, “Wewe u mwenye haki, uliyeko na uliyekuwako, Mtakatifu, kwa kuwa umehukumu hivi; Kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu na ya manabii, nawe umewapa damu wainywe; nao wamestahili.” Ufunuo 16:2-6. Kwa kuwahukumu watu wa Mungu adhabu ya kifo, hakika wamepokea hatia ya damu yao kana kwamba ilimwagwa kwa mikono yao. Kristo alisema juu ya hatia ya Wayahudi wa wakati wake ya umwagaji damu ya watakatifu tokea zamani za Habili (Mathayo 23:34-36), kwa kuwa wao pia walikuwa na roho ile ile kama wale wauaji wa manabii. TK 377.3
Katika pigo lililofuata, jua linapewa uwezo, “ili kuwaunguza wanadamu kwa moto.” Ufunuo 16:8,9. Nabii anaeleza kuhusu wakati huu wa kutisha, “Maana mavuno ya mashamba yamepotea...Naam, miti yote ya mashamba imekauka; maana furaha imekauka katika wanadamu...Jinsi wanyama wanavyougua! Makundi ya ng’ombe yamefadhaika, kwa sababu hawana malisho. ..Kwa maana vijito vya maji vimekauka, na moto umeyateketeza malisho ya nyikani.” Yoeli 1:11, 12, 18-20. TK 377.4
Mapigo haya hayatapiga sehemu zote za dunia, lakini yatakuwa mapigo yanayotisha kuliko yote yaliyopata kutokea. Hukumu zote zitakazo tokea kabla ya mlango wa rehema kufungwa zitakuwa zimechanganywa na rehema. Damu ya Kristo inamlinda mwenye dhambi toka kwenye hatia kamili; lakini wakati wa hukumu ya mwisho utakapowadia, ghadhabu haitachanganyika na rehema. Wengi wataitamani rehema ya Mungu ambayo walikuwa wakiidharau. TK 378.1
Watu wa Mungu hawataachwa waangamie japokuwa wanateseka na kutaabika kwa sababu ya mambo mema. Malaika watawahudumia kwa mahitaji yao, . atapewa chakula chake; maji yake hayatakoma.” mimi, Bwana, nitawasikia, mimi, Mungu wa Israeli, sitawaacha.”Isaya 33:16; 41:17. TK 378.2
Lakini katika macho ya kibinadamu itaonekana kuwa watu wa Mungu watakuwa radhi kutia muhuri ushuhuda wa maisha yao kwa damu yao, kama walivyofanya wafia dini waliowatangulia. Utakuwa wakati wa uchungu wa kutisha. Waovu watawadhihaki kwa kusema, “Iko wapi sasa imani yenu? “Ikiwa kweli ninyi ni watu wa Mungu, kwa nini hajawakomboa kutoka mikononi mwetu?” Lakini watu watakaokuwa na subira watakumbuka jinsi Yesu alivyokuwa akifa pale msalabani. Kama Yakobo, wote watakuwa wakimng’ang’ania Mungu. TK 378.3