Nchini Ujerumani, mauzo ya hati za msamaha wa dhambi yaliendeshwa na mtu mwovu kupindukia aliyekuwa anaitwa Tetzel. Na nchini Uswisi biashara hii ilikuwa ikisimamiwa na mtawa wa Kiitaliano aliyekuwa anaitwa Samson. Samson tayari alikuwa amekusanya kiasi kikubwa cha pesa na kuzijaza katika hazina ya utawala wa Papa kutoka nchini Ujerumani na Uswisi. Na kwa wakati huu alikwenda huku na huko nchini Uswisi akiwapora wakulima maskini mapato yao kidogo na kuwatoza matajiri vitu vya thamani. Mara moja Mwanamatengenezo huyo alijitosa kumpinga. Zwingli alifanikiwa sana kufunua unafiki wa mtawa huyu kiasi cha kumlazimisha kuondoka kwenda sehemu nyingine. Kule Zurich, Zwingli alihubiri kwa nguvu sana dhidi ya wachuuzi wa hati za msamaha wa dhambi, na Samson alipokwcnda mahali pale, alikutana na muuzaji wa vyeti kutoka katika baraza kukiwa na dalili kwamba alikuwa akitarajiwa kupita pale. Kwa werevu aliruhusiwa kuingia pale, lakini aliondoshwa bila kuuza cheti hata kimoja cha msamaha na baada ya muda mfupi aliondoka nchini Uswisi. TK 116.1
Mnamo mwaka 1519 tauni ama Janga Kuu la kifo liliikumba Uswisi. Wengi waliongozwa kujisikia jinsi zisivyofaa na zisivyokuwa na thamani yoyote hati za msamaha ya dhambi walizokuwa wamezinunua. Walitamani sana kupata msingi wa hakika wa imani yao. Kule Zurich, Zwingli aliugua sana, na taarifa zilienea kila sehemu ya kuwa alikuwa amekufa. Na katika saa hiyo ya kujaribiwa, aliuangalia kwa imani msalaba wa Kalivari, akitumainia upatanisho unaotosha kabisa dhidi wa dhambi. Aliponusurika kufa, alihubiri Injili kwa hamasa kubwa kuliko hapo kabla. Watu walikuwa wametoka kuwahudumia wagonjwa na wale waliokuwa wanakufa, na walijisikia hitaji la Injili kuliko ilivyokuwa hapo kabla. TK 116.2
Zwingli alikuwa ameelewa dhahiri ukweli wa Injili maana yeye mwenyewe alikuwa amepitia kikamilifu zaidi uwezo ya Injili wa kufanywa upya. Alisema, “Kristo amenunua kwa ajili yetu ukombozi usiokoma kamwe... Shauku yake kuu ni...kafara ya milele inayoleta uponyaji wenye matokeo yanayotakiwa na yasiyokoma, ambayo huridhisha haki ya Mungu milele kwa niaba ya wote wanaoitegemea kwa uthabiti na imani isiyoyumba... Popote palipo na imani kwa Mungu, shauku huja ya kusihi na kuwahimiza watu kutenda matendo mema.” 102Ibid., 8, ch. 9. TK 116.3
Hatua kwa hatua, matengenezo yalikua kule Zurich. Kwa mshtuko wa hofu waliinuka kuleta upinzani mkubwa. Mashambulizi ya mara kwa mara yalifanywa dhidi ya Zwingli. Mwalimu wa uzushi ni sharti anyamazishwe. Askofu wa Constance aliwatuma wasaidizi wake watatu kwenda kwenye Baraza la Zurich, akimshitaki Zwingli kwa kuhatarisha amani na utaratibu katika jamii. Alisihi kuwa, ikiwa mamlaka ya kanisa ingewekwa kando; vurugu ingetokea kila mahali. TK 117.1
Baraza lilikataa kumchukulia hatua Zwingli, kwa hiyo Kanisa la Roma likaanza kujiandaa kwa ajili ya mashambulizi mapya. Mwanamatengenezo huyu aliitikia kwa kusema: “Hebu na waje maana ninawaogopa kama vile jabali linaloning’inia linavyoyaogopa maji yanayoupiga msingi wake.” 103Wylie, bk. 8, ch. 11 Juhudi za makasisi kutaka kuiangusha kazi ya Wanamatengenezo viliifanya iendelee kusonga mbele. Ukweli ulikuwa unaendelea kuenea. Nchini Ujerumani wafuasi wake waliokuwa wamekatishwa tamaa na kutoweka kwa Luther, walitiwa moyo tena walipoona maendeleo ya Injili nchini Uswisi. Matengenezo yalipokita mizizi kule Zurich matunda yake yalionekana kwa ukamilifu kwa kukomeshwa kwa uovu na kukuzwa kwa mfumo wa maisha yenye utaratibu. TK 117.2