Upinzani kule Spires na Ungamo la Imani pale Augsburg vilifuatiwa na miaka ya giza na mapambano. Hatima ya Uprotestanti ilionekana kwenda kwenye uangamivu kwa sababu ulikuwa umedhoofishwa na mgawanyiko. TK 136.1
Lakini katika wakati ule ambapo mfalme alionekana kuwa mshindi dhahiri, hapo ndipo alipozidiwa nguvu. Hatimaye alilazimika kukubali kuvumilia mafundisho ambayo lengo lake kuu maishani lilikuwa ni kuyaangamiza. Aliyaona majeshi yake yakiangamia vitani, hazina yake ilikaukiwa, na falme nyingi zilizokuwa chini yake zilikuwa zinatishia kuasi, na kila mahali imani aliyokuwa akitaka kuikomesha ilikuwa inaendelea kupanuka. Charles V alikuwa akipigana na Mungu Mwenyezi. Mungu alikuwa amesema, “Iwe nuru,” lakini mfalme alikuwa amekusudia giza lisivujwe. Huku akiwa amechoshwa sana na vita vya muda mrefu, aling’atuka toka kwenye kiti chake cha enzi na kwenda kujificha kwenye makazi ya watawa. TK 136.2
Wakati majimbo mengi kule Uswisi yalikuwa yamepokea imani ya matengenezo, wengine waling’ang’ania kanuni za imani za Kanisa la Roma. Mateso yalichochea vita vya wenyewe kwa wenyewe. Zwingli na wengine wengi waliokuwa wamejiunga kwenye matengenezo walianguka kwenye uwanja wa damu kule Cappel. Kanisa la Roma lilipata ushindi na katika maeneo mengi lilionekana kuyakomboa majimbo yote lililokuwa limeyapoteza. Lakini Mungu alikuwa hajasahau kazi yake ama watu wake. Kwenye maeneo mengine alinyanyua watendakazi kuendeleza matengenezo. TK 136.3
Nchini Ufaransa, mtu aliyekuwa wa kwanza kuipata nuru alikuwa ni profesa kwenye chuo kikuu cha Paris, aliyekuwa anaitwa Lefevre. Katika utafiti wake kwenye Maandiko ya kale, usikivu wake ulielekezwa kwenye Biblia, na alianzisha somo la Biblia miongoni mwa wanafunzi wake. Alikuwa amejitolea kuandaa historia ya watakatifu na wafia dini kama ilivyotolewa katika masimulizi ya kanisa na alikuwa ameifanya kwa sehemu kubwa, na katika muda huo, alianza kufikiria kupata msaada kutoka kwenye Biblia, hivyo alianza kujifunza Biblia. Hapa alikutana na watakatifu si kama vile wanavyoelezewa kwenye orodha ya Kanisa la Roma. Huku akiwa ameudhika kwa hilo, aliachana na jukumu alilokuwa amejitwisha na kujitoa kujifunza Neno la Mungu. TK 136.4
Mnamo mwaka 1512, kabla ya Luther au Zwingli kuanza kazi ya matengenezo, Lefevre aliandika, “Mungu hutupatia kwa njia ya imani ile haki ambayo kwa neema peke yake huwa tunahesabiwa haki hata uzima wa milele.” 131Wylie, bk. 13, ch. 1. Na wakati alipokuwa anafundisha kwamba utukufu wa wokovu ni mali ya Mungu peke yake, pia alitangaza ya kuwa jukumu la kutii ni la mwanadamu. TK 137.1
Baadhi ya wanafunzi wa Lefevre walikuwa wakiyasikiliza kwa makini maneno yake na muda mrefu baada ya sauti ya mwalimu wao kunyamazishwa, wao waliendelea kuutangaza ukweli. Hivyo ndivyo alivyokuwa William Farel. Mwana wa wazazi waliokuwa wacha Mungu na mfuasi mwaminifu wa Kanisa la Roma, alikuwa anakasirika sana na kuwa na ari ya kuwaangamiza wale ambao wangediriki kulipinga kanisa. Baadaye alikuja kusema, “Ningesaga meno yangu mithili ya mbwa mwitu mwenye hasira, nilipomsikia mtu yeyote akizungumza maneno kinyume na Papa.” Lakini kuwatukuza watakatifu, kuabudu kwenye madhabahu, na kuyapamba kwa tunu mahekalu matakatifu, hakukuleta amani moyoni. Kujisikia hatia ya dhambi kuliendelea kumsonga, hata matendo yote ya kitubio hayakuweza kuiondoa hali ya hatia. Aliyasikiliza maneno ya Lefevre. “Wokovu ni kwa neema.” “Ni msalaba Wakristo peke yake uwezao kufungua malango ya mbinguni na kuyafunga malango ya kuzimu.” 132Ibid. bk. 13, ch. 2. TK 137.2
Kwa uongofu kama ule wa Paulo, Farel aligeuka kutoka kwenye utumwa wa mapokeo na kwenda katika uhuru wa wana wa Mungu. “Badala ya moyo wa uuaji wa mbwa mwitu mkali,” alirejea toka huko na anasema akiwa “mtulivu na mnyenyekevu na asiyedhuru kama mwanakondoo, baada ya moyo wake wote kuondolewa kwa Papa na kuutoa kwa Yesu Kristo.” 133D’Aubigne, bk. 12, ch. 3. TK 137.3
Lefevre alikuwa akisambaza nuru kwa wanafunzi, Farel alikuwa anaendelea mbele kuutangaza ukweli mbele ya watu. Mtu mwenye cheo kanisani, askofu wa Meaux, mapema aliungana nao. Walimu wengine walijiunga katika kuitangaza Injili, na ilipata wafuasi toka kwenye familia za wasanii na wakulima mpaka katika ikulu ya mfalme. Dada yake Francis wa Kwanza aliipokea imani ya matengenezo. Wakiwa na matumaini makubwa, Wanamatengenezo waliutazamia wakati ambao Ufaransa ingetekwa kwa Injili. TK 138.1