Yesu akaendelea kusema: “Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili, na kilichozaliwa kwa Roho ni Roho.” Kwa asili hali ya mwili ni uovu. Tazama Ayubu 14:4. Hakuna uvumbuzi wa kibinadamu unaoweza kupata dawa ya moyo wa mtu wa dhambi, “Moyo wa asili ni uadui na Mungu.” Katika moyo hutoka “mawazo mabaya, uuaji, uasherati, uzinzi, wizi, uongo, makufuru.” Warumi 8:7; Mathayo 15:19. Chemchemi ya moyo lazima iwe safi; kabla ya maji yake kuwa safi. Yule anayejaribu kuingia mbinguni kwa matendo yake, kwa kushika sheria, hufanya jambo lisilowezekana. Maisha ya Ukristo siyo kutengeneza maisha ya zamani yawe bora, ila ni mabadiliko ya hali ya asili, ya mwili. Kufa kwa ubinafsi, na hali ya dhambi, na kuishi maisha mapya kabisa. Mabadiliko ya namna hiyo huletwa na Roho Mtakatifu peke yake. TVV 90.2
Nikodemo, alikuwa angali akitatanika. Ndipo Yesu akatumia mfano wa upepo kama kielelezo. Akasema: “Upepo huvuma utakapo, na sauti yake waisikia, lakini huwezi kujua utokako, wala uendako. Kadhalika na mtu aliyezaliwa wa Roho.” TVV 90.3
Upepo husikiwa ukitikisa majani na maua, walakini hauonekani. Hali kadhalika na Roho Mtakatifu katika moyo wa mtu. Mtu hawezi kusema kwa hakika ni lini, au wapi alipata kuongoka, lakini jambo kama hili siyo kusema kuwa bado hajaongoka, ati kwa sababu hajui ni lini au wapi. Kwa njia ya uwezo usioonekana kama upepo, Kristo hufanya hivyo kwa moyo wa mtu, kidogo kidogo hali ya mvuto wa kuelekea kwa Kristo hufanyika kwa mtu. Mambo haya hufanyika kwa ajili ya kusoma maandiko matakatifu, au kwa ajili ya kusikia mahubiri ya mhubiri. Ghafla kiasi cha msukumo wa Roho Mtakatifu, mtu hujitoa kwa Kristo. Watu wengi huita hali hii kwamba ni kuongoka kwa ghafla. Lakini sivyo, ni kazi ya Roho Mtakatifu ya wakati mrefu. TVV 90.4
Upepo hufanya vitu vionekane na kusikia. Vivyo hivyo na kazi ya Roho Mtakatifu itajidhihirisha kwa matendo bora kwa mtu anayesukumwa naye. Roho Mtakatifu hubadilisha maisha ya mtu. Mawazo maovu huachwa, matendo ya dhambi hukanushwa. Upendo, unyenyekevu, amani huja badala ya hasira, wivu, na mashindano. Furaha huja badala ya huzuni. Mtu anapojitoa kwa Yesu kwa imani, uwezo ambao hauonekani kwa macho, huumba utu mpya kwa mfano wa Mungu. Mwanzo wa ukombozi tunaweza kuufahamu hapa duniani, kwa njia ya maisha; matokeo yake hufikia umilele. TVV 91.1