Mkono wa Mungu ulipoonekana kana kwamba unawaelekeza ng’ambo ya bahari katika nchi ambayo wangeanzisha taifa ambalo wangeacha urithi wa uhuru wa dini kwa watoto wao; walisonga mbele wakiwa katika uongozi wa Mungu. Mateso na kufukuzwa kulifungua njia kuelekea kwenye uhuru. TK 188.1
Mara ya kwanza walipolazimishwa kujitenga na Kanisa la Uingereza, watu walioitwa Puritans walijiunga wenyewe kwa agano kama watu wa Mungu walio huru “kutembea pamoja katika njia zake zote wanazozijua au watakazozijua” 180J. Brown, The Pilgrim Fathers, p. 74. Hapa ndipo ilipokuwa kanuni ya muhimu ya Uprotestanti. Wakiwa na lengo hili Mahujaji waliondoka kutoka Uholanzi ili watafute makao kwenye Ulimwengu Mpya. John Robinson, mchungaji wao, katika hotuba yake ya kuwaaga aliwaambia: Nawapa wajibu mbele za Mungu na malaika zake wenye baraka kunifuata mimi si zaidi ya vile nilivyomfuata Kristo. Kama Mungu atawafunulia kitu chochote, kwa kutumia chombo chake chochote, mwe tayari kupokea kama mlivyokuwa tayari kuupokea ukweli wa huduma yangu; maana nina hakika Bwana anao ukweli na nuru ambayo hajaitoa bado kutoka kwenye Neno lake takatifu.” 181Martyn, vol. 5, p. 70. TK 188.2
“Kwa upande wangu, siwezi kuisikitikia kwa ukamilifu hali ya makanisa yaliyofanya matengenezo, ni nani...kwa wakati huu, ambao hawatakwenda mbali zaidi kuliko kuwa watumishi wa matengenezo. Walutheri hawawezi kuvutwa na kwenda mbali ya kile alichokiona Luther;...na wafuasi wa Calvin, unaona, wanasimama imara pale walipochwa na yule mtu wa pekee wa Mungu, ambaye naye hakuona vitu vyote...Ingawa kwa wakati wao walikuwa ni nuru iliyokuwa inawaka na kung’aa, lakini hawakupenya kwenye mawaidha yote ya Mungu, lakini kama wangekuwa hai, wangekuwa tayari tena kuipokea nuru zaidi kama ile waliyoipokea awali.” 182D. Neal, History of Puritans, vol. 1, 269. TK 188.3
“Ikumbukeni ahadi na agano kati yenu na Mungu na ninyi kwa ninyi, kuupokea ukweli na nuru yoyote atakayoifunua kwenu kutoka kwenye Neno lililoandikwa; lakini juu ya hayo, iweni waangalifu, ninawasihi, ni kitu gani mnakipokea kama ukweli, na kukilinganisha na kukipima kwa Maandiko mengine ya ukweli kabla ya kukikubali; maana haiwezekani ulimwengu wa Kikristo uchelewe kutoka kwenye giza hili nene la mpinga Kristo, na ule ufahamu mkamilifu utatokea mara.” 183Martyn, vol. 5, pp. 70, 71. TK 189.1
Shauku ya uhuru wa dhamiri iliwatia moyo Mahujaji kuivuka bahari, kuuvumilia ugumu wa jangwani, na kuuweka msingi wa taifa kubwa. Lakini Mahujaji hawakufahamu bado kanuni ya uhuru wa kidini. Uhuru walioupata kwa kujitoa mhanga sana, hawakuwa tayari kuutoa kwa wengine. Fundisho linalosema kwamba Mungu amelipatia kanisa haki ya kudhibiti dhamiri, kubaini, na kuadhibu uasi, ni moja kati ya yale makosa ya utawala wa Papa yenye mizizi ya kina. Wanamatengenezo, hawakuachwa huru kabisa, bila ile roho ya Kanisa la Roma ya kutovumiliana. Giza nene ambalo kwalo Kanisa la Roma lilikuwa limeufunika ulimwengu wa Ukristo, lilikuwa halijatawanyika kikamilifu. TK 189.2