Hoja hizo zilikuwa na ushawishi mkubwa, na “kelele ya usiku wa manane” ilitangazwa na maelfu ya waumini. Harakati hizo zilienea kutoka mji hadi mji na kutoka kijiji hadi kijiji kama wimbi za bahari. Itikadi kali zilitoweka kama ukungu kabla ya kuchomoza kwa jua. Harakati hizo zilikuwa zinafanana na vile vipindi vya kumrudia Bwana miongoni mwa wana wa Israeli vilivyokuwa vinatokea baada ya maonyo ya watumishi wake. Hakukuwa na nderemo sana, bali kujipeleleza mioyo kwa kina, maungamo ya dhambi, na kuachana na ulimwengu. Kulikuwa na kujitoa kikamilifu kwa Mungu. TK 251.2
Katika harakati zote za kidini tangu wakati wa mitume, hakuna harakati zilizokuwa hazina dosari za wanadamu na hila za Shetani kama zile za majira ya kupukutisha ya mwaka 1844. TK 251.3
Baada ya mwito, “Haya, bwana arusi anakuja,” wote waliokuwa wakisubiri “wakaondoka ... wakazitengeneza taa zao”; walijifunza Neno la Mungu kwa shauku kubwa ambayo ilikuwa haijawahi kutokea. Hawakuwa wale wenye vipaji, bali wale wanyenyekevu na watauwa, ndio waliokuwa wa kwanza kuutii mwito huo. Wakulima waliyaacha mazao yao mashambani, mafundi waliacha zana zao, wakatoka kwa furaha kwenda kutoa ujumbe wa onyo. Makanisa kwa ujumla yaliukataa ujumbe huo, na wengi walioupokea ujumbe huu walijitenga na makanisa hayo. Wasioamini ambao walikuwa wanakusanyika kwenye mikutano ya Waadventista waliihisi nguvu ya ushawishi iliyoambana na ujumbe huo: “Haya, bwana arusi anakuja!” Imani ilileta majibu kwa maombi. Roho wa neema aliwashukia kama manyunyu ya mvua kwenye ardhi kavu, wale waliokuwa wanatafuta ukweli kwa dhati. Wale waliokuwa wanatarajia kuonana uso kwa uso na Bwana wao karibuni, walikuwa na furaha. Roho Mtakatifu aliiyeyusha mioyo yao. TK 251.4
Wale waliokuwa wameupokea ule ujumbe walifika katika kipindi ambacho walikuwa wanategemea kukutana na Bwana wao. Waliomba pamoja. Mara nyingi walikuwa katika sehemu zisizokuwa na watu wengi ili waongee na Mungu, na sauti yao ya kuombea wengine ilipanda kwenda mbinguni kutoka katika mashamba. Uhakika wa kukubalika na Bwana ulikuwa wa lazima sana kwao kuliko chakula cha kila siku, na pale mashaka yalipoingia katika akili zao, hawakutulia mpaka walipoona ushahidi wa neema ya msamaha. TK 252.1