Kwa kadiri Mwanamatengenezo alivyoendelea, umati wa watu wenye shauku walimzunguka, na sauti zenye urafiki zilimwonya juu ya utawala wa Kanisa la Roma. Baadhi walisema, “Watakuchoma moto, na kuteketeza mwili wako kuwa majivu kama walivyomfanyia John Huss.” Luther aliwajibu kuwa, “Hata kama watawasha moto njia nzima kutoka Worms hadi Wittenberg,...kwa jina la Bwana nitatembea kwenye njia hiyo; nitasimama mbele yao,...nikimkiri Bwana Yesu.” 73Ibid. TK 98.4
Kukaribia kufika kwa Luther huko Worms kulisababisha ghasia kubwa. Marafiki zake walikuwa wanahofia usalama wake; maadui zake walihofu juu ya kusudi lao. Akichochewa na watawala wa Kanisa la Roma, alitakiwa aende kwenye nyumba ya mtu mmoja mwema na mwenye hadhi ya juu, ambako, mambo yote magumu yangetatuliwa kirafiki. Marafiki walielezea hatari zilizokuwa zinamkabili. Luther bila kutetemeka alitamka kuwa: “Hata kama mji wa Worms utakuwa na maShetani wengi kama vigae vya paa la nyumba, bado nitauingia” 74Ibid. TK 99.1
Alipowasili katika mji wa Worms, kundi kubwa la watu lilikuwa limejaa langoni ili kumpokea. Kulikuwa na msisimko wa hali ya juu. Alipokuwa akitelemka kutoka kwenye gari lake la farasi alisema, “Mungu atakuwa mlinzi wangu.” Kuwasili kwake kuliwajaza fadhaa viongozi wa Kanisa la Roma. Mfalme aliwaita washauri wake. Aliwauliza ni njia gani wangeitumia. Kiongozi mmoja shupavu wa Kanisa la Roma alitamka kuwa: “Tumejadiliana kwa muda mrefu juu ya jambo hili. Hebu wewe mfalme mtukufu mfutilie mbali mtu huyu mara moja. Je, Sigismund hakuamuru John Huss achomwe moto? Hatufungwi na kanuni kumpa au kutimiza hakikisho la usalama wa mtu mwasi.” “Hapana” mfalme alisema, “Ni lazima tuitimize ahadi yetu.” 75Ibid., ch. 8. Iliamriwa kuwa Mwanamatengenezo apate nafasi ya kusikilizwa. TK 99.2
Watu wote wa mji ule walikuwa na shauku ya kumwona mtu huyu asiye na kifani. Luther alikuwa amechoka kwa safari, alihitaji pumziko na utulivu. Lakini alipata saa chache tu za kupumzika pale, watu wenye vyeo, waheshimiwa, mapadre, na raia walipokusanyika kumzunguka. Miongoni mwao ni waheshimiwa ambao kwa ujasiri walimtaka mfalme afanye matengenezo juu ya shutuma zilizolihusu kanisa. Marafiki na maadui walikuja kumwangalia mtawa huyu asiye na hofu. Mwonekano wake ulikuwa thabiti na wa kijasiri. Uso wake mwembamba, uliokuwa unaonekana, kunyong’onyea ulivaa mwonekano wa upole na furaha. Maneno yake ya dhati yalisababisha nguvu ambayo hata adui zake hawakuweza kuihimili kikamilifu. Wengine walishawishika kuwa alikuwa na nguvu ya Mungu iliyokuwa inamwongoza; wengine, kama Mafarisayo walivyomwambia Kristo, walitamka kuwa, “Ana pepo.” Yohana 10:20. TK 99.3
Katika siku iliyofuata afisa mmoja wa serikali aliteuliwa kumwongoza Luther kwenye ukumbi ili akasikilizwe. Kila mahali palikuwa pamejaa watazamaji wenye shauku ya kumwona mtawa aliyethubutu kumpinga Papa. Jemadari mmoja mzee, aliyewahi kushinda vita vingi, alimwambia kwa upole, “Maskini mtawa, sasa unakwenda kuonesha msimamo bora kuliko mimi au uliowahi kuoneshwa na makapteni wowote kwenye mapambano yetu yenye umwagaji damu. Lakini ikiwa kusudi lako ni la haki,...songa mbele katika jina la Mungu, na usiogope chochote. Mungu hatakuacha.” 76Ibid. TK 100.1