Mfalme alikaa kwenye kiti chake. Alikuwa amezungukwa na watu mashuhuri zaidi katika ufalme wake. “Mwonekano huu kwa peke yake ulikuwa alama ya ushindi dhidi ya utawala wa Papa. Papa alikuwa tayari amemhukumu Luther, na sasa alikuwa anasimama mbele ya mahakama ambayo, kwa kitendo hicho, ilijiweka yenyewe juu ya Papa. Papa alikuwa amempiga marufuku, akamtenga kutoka kwenye jamii nzima ya wanadamu; na bado aliitwa kwa lugha yenye staha, na akapokelewa mbele ya kusanyiko adhimu zaidi duniani...Roma ilikuwa tayari inashuka kutoka kwenye enzi yake, na ilikuwa ni sauti ya huyu mtawa iliyosababisha fedheha hii.” 77Ibid. TK 100.2
Mwanamatengenezo huyo aliyezaliwa kwenye familia duni alionekana kutishika na kutahayari. Wakuu kadhaa walimsogelea, na mmoja wao akamnong’oneza kuwa asiwaogope “wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho.” Mwingine akasema: “Nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema.” Angalia Mathayo 10:28, 18, 19. TK 100.3
Kukawa na ukimya mkuu kwenye kusanyiko la umati wa watu. Ndipo yule afisa wa serikali akasimama, akiyaonesha Maandiko ya Luther na kumtaka Mwanamatengenezo huyo ajibu maswali mawili- ikiwa aliyatambua kuwa ni yake, na endapo alikuwa amefikiria kukanusha maoni yaliyomo ndani ya Maandiko yale. Vilipokwisha kusomwa vichwa vya vitabu, Luther alijibu swali la kwanza kwamba alivitambua kuwa ni vyake. “Kuhusu swali la pili,” akasema, “Nitatenda bila busara ikiwa nitajibu bila kutafakari. Ninaweza nikatoa uthibitisho kidogo kuliko hali inavyohitaji, ama zaidi ya vile ukweli unavyotaka. Kwa sababu hii ninakusihi mfalme mtukufu, kwa unyenyekevu wote, nipatie muda, ili niweze kujibu pasipo kulikosea Neno la Mungu.” 78Ibid. TK 101.1
Luther alilishawishi kusanyiko kuwa katika kutenda jambo lile hakuongozwa na hisia au mihemuko ya ghafla. Utulivu na kujiamini kwa namna ile, ambako hakukutarajiwa ndani ya mtu imara asiyebadili msimamo; ulimwezesha baadaye kujibu kwa busara na heshima iliyowashangaza adui zake na ikawa onyo kwa ufidhuli wao. TK 101.2
Siku iliyofuata, Luther alipaswa kutoa jibu lake la kwanza. Kwa muda mfupi moyo wake ulishuka. Adui zake walielekea kupata ushindi. Mawingu yalimzunguka na yalionekana kumtenga na Mungu. Akiwa na huzuni kuu rohoni, alimwaga vilio vya moyo uliopondeka na kuraruka, ambayo hakuna awezaye kuvifahamu isipokuwa Mungu. “Oo Mungu mkuu na wa milele,” alimsihi, “Ikiwa ni lazima niweke tumaini langu katika uwezo wa ulimwengu huu tu, kila kitu kimekwisha...Saa yangu ya mwisho imekuja, hukumu yangu tayari imetolewa...Oo Mungu, unisaidie dhidi ya hekima ya ulimwengu...Kazi ni yako...na ni kazi ya haki na ya milele. Oo Bwana, unisaidie! Mungu uliye mwaminifu na ambaye si kigeugeu, siliweki tumaini langu juu ya mwanadamu yeyote...Umenichagua kwa ajili ya kazi hii...Simama upande wangu, kwa ajili ya Mwanao mpendwa Yesu Kristo, ambaye ndiye mlinzi wangu, ngao yangu, na ngome yangu . 79Ibid. TK 101.3
Jambo lililomtia hofu kubwa halikuwa kuogopa taabu yake binafsi, mateso, ama kifo. Alikuwa anahisi kuwa upungufu na udhaifu wake ungeweza kudhoofisha kusudio la ukweli. Alishindana na Mungu si kwa ajili ya usalama wake mwenyewe, bali kwa ajili ya ushindi wa Injili. Katika udhaifu wake usio na msaada kabisa, aliishikilia imani yake kwa Kristo, Mwokozi mwenye nguvu. Asingetokea akiwa pekee yake mbele ya baraza. Amani ilirejea moyoni mwake, na alifurahi kwa sababu aliruhusiwa kuliinua Neno la Mungu mbele ya watawala wa mataifa. TK 101.4
Luther alitafakari juu ya jibu lake, alizichunguza aya ndani ya maandishi yake, na kutoa ndani ya Maandiko Matakatifu ushahidi unaofaa kutetea msimamo wake. Kisha, aliuweka mkono wake wa kushoto juu ya Kitabu Kitakatifu, akauinua mkono wake wa kuume mbinguni na kuapa “kudumu akiwa mwaminifu katika Injili, na kuikiri imani yake kwa uhuru, hata kama ushuhuda wake ungegharimu maisha yake.” 80Ibid. TK 102.1