Alipokaribishwa kwa mara nyingine ndani ya mkutano, alikuwa mtulivu na mwenye amani, lakini pia shujaa na mwenye heshima, kama shahidi wa Mungu miongoni mwa watu wakuu wa dunia. Yule afisa wa serikali sasa alikuwa anahitaji kupata uamuzi wa Luther. Je, alikuwa ameamua kukanusha? Luther alitoa jibu lake kwa sauti ya unyenyekevu, bila vurugu wala hofu. Mwonekano wake ulikuwa wa kutojiamini na wenye heshima; lakini alionesha ujasiri na furaha ambavyo viliwashangaza mkutano ule. TK 102.2
Alianza kwa kusema: “Mtukufu mfalme mkuu, wana adhimu wa wafalme, mabwana wenye hisani; ninasimama mbele yenu siku ya leo, ili kutimiza agizo lililotolewa kwangu jana. Ikiwa, kwa ujinga, nitakosea matumizi na taratibu za mahakama ninawasihi mnisamehe; maana sikulelewa kwenye nyumba za wafalme, bali kwenye nyumba za upweke za watawa.” 81Ibid. TK 102.3
Kisha akasema kuwa ndani ya baadhi ya kazi zake zilizochapishwa juu ya imani na matendo; hata maadui zake walisema kuwa zinafaa. Kuzikanusha ingekuwa ni kuushutumu ukweli ambao watu wote wanaukiri. Daraja la pili lilijumuisha maandishi yaliyoufunua upotovu na dhuluma za utawala wa Papa. Kuyatangua hayo kungeimarisha udhalimu wa Kanisa la Roma na kufungua mlango mpana kwa kufuru kubwa. Katika daraja la tatu aliwashambulia watu binafsi walioyatetea maovu. Kuhusiana na hayo alikiri kwa uhuru kuwa alikuwa mkali kuliko ilivyotakiwa. Lakini vitabu hivi pia hangevitangua, kwani maadui wa ukweli wangechukua fursa hiyo kuwalaani watu wa Mungu kwa ukatili mkubwa zaidi. TK 102.4
Aliendelea kusema, “Nitajitetea mwenyewe kama Kristo alivyofanya: ‘Ikiwa nimeongea uovu, uletwe ushahidi juu ya uovu’..Kwa rehema ya Mungu, ninakusihi sana wewe, mfalme mtukufu sana, na ninyi wana adhimu wa wafalme, na wanadamu wote wa kila hadhi, kuthibitishiwa kutoka kwenye Maandiko ya manabii na mitume kwamba nimekosea. Mara tu nitakaposhawishika juu ya hili, nitakanusha kila kosa,.na kuwa wa kwanza kuvichukua vitabu vyangu na kuvitupa motoni... TK 103.1
“Badala ya kutishwa, ninafurahia kuona kuwa Injili, sasa inasababisha taabu na mafarakano, kama ilivyokuwa katika nyakati zilizopita. Hii ndiyo tabia, hii ndiyo hatima ya Neno la Mungu. ‘Sikuja kuleta amani duniani, bali upanga,’ alisema Yesu Kristo... Jihadharini, isije ikawa kwa kudhani mnazuia mafarakano, kumbe mnalitesa Neno Takatifu la Mungu, na kujiletea wenyewe gharika ya kutisha ya hatari zisizoondoka, za maafa ya wakati wa sasa, na ukiwa wa milele.” 82Ibid TK 103.2
Luther alizungumza kwa Kijerumani; na sasa alitakiwa kuyarudia maneno yale yale kwa Kilatini. Kwa mara nyingine tena aliitoa hotuba yake kwa ufasaha kama aliyoitoa kwanza. Ni majaliwa ya Mungu yaliyoliongoza hili. Wakuu wengi walikuwa wamepofushwa na uongo na mapokeo potuvu kiasi kwamba mwanzoni hawakuona nguvu ya hoja za Luther, lakini marudio yaliwawezesha kutambua kwa uwazi hoja alizozileta. TK 103.3
Wale ambao kwa kiburi waliyafumba macho yao wasipate nuru, walikasirishwa kutokana na uwezo uliokuwa kwenye maneno ya Luther. Msemaji wa lile baraza akasema kwa hasira: “Hujajibu swali uliloulizwa...unapaswa kutoa jibu lililo wazi na kwa ufupi...Je, utakanusha au hutakanusha?” TK 103.4
Mwanamatengenezo akajibu: “Kwa vile wewe uliye mtakatifu sana na wakuu wenye nguvu wanataka kutoka kwangu jibu sahihi, rahisi, na fupi; nitawapa, nalo ni hili: “Siwezi kuisalimisha imani yangu kwa Papa au kwenye mabaraza, maana ni wazi kama mchana kwamba mara nyingi wamekosea na kujichanganya wenyewe. Kwa hiyo, nisiposhawishika kwa ushuhuda wa Maandiko,...Siwezi na sitaweza kukanusha, maana si salama kwa Mkristo kusema kinyume ma dhamiri yake. Huu ndio msimamao wangu, siwezi kufanya kitu kingine; Mungu anisaidie. Amina.” 83Ibid TK 104.1
Hivi ndivyo alivyosimama huyu mtu mwenye haki. Ukuu na usafi wa tabia yake, amani na furaha yake ya moyo, vilionekana kwa wote alipokuwa akishuhudia ukuu wa ile imani iushindayo ulimwengu. TK 104.2
Katika jibu lake la kwanza Luther alizungumza akiwa na mwonekano wa heshima na kujisalimisha. Watawala wa Kanisa la Roma walichukulia kuwa ombi la muda wa ziada lilikuwa ni utangulizi wa kuyakanusha maoni yake. Mfalme Charles mwenyewe, alilitazama kwa dharau kidogo umbile la mtawa lililochakaa, akiwa kwenye mavazi yake ya kawaida, na usahili wa hotuba yake, alitamka kuwa: “Mtawa huyu kwangu mimi siyo mwasi.” Ujasiri na uimara ambao sasa aliuonesha, uwezo wake wa kujenga hoja, ulisababisha watu wote kupigwa na butwaa. Mfalme, akiwa amevutwa na kustaajabu, alitamka kwa mshangao: “Huyu mtawa anazungumza kwa moyo wa ushujaa na ujasiri usiotikisika.” TK 104.3
Wafuasi wa Kanisa la Roma walikuwa wamedanganywa. Walitaka kudumisha mamlaka yao kwa njia ya vitisho, hoja ya Kanisa la Roma isiyoshindwa, si kwa njia ya kuuliza kwenye Maandiko matakatifu bali, Msemaji wa baraza alisema: “Ikiwa hukanushi, mfalme na serikali ya ufalme wataamua ni hatua gani waichukue dhidi ya mwasi mwenye tabia isiyobadilika.” Luther alijibu kwa utulivu: “Mungu awe msaada wangu, maana siwezi kukanusha chochote.” 84Ibid TK 104.4
Alikuwa ameelekezwa kufuta msimamo wake wakati wakuu walipokuwa wakinajadiliana. Tendo la Luther kukataa kujisalimisha lingeweza kuathiri historia ya kanisa kwa vizazi vingi. Iliamuliwa kuwa apewe nafasi nyingine zaidi ya kukanusha. Swali liliulizwa tena, endapo angeyafuta mafundisho yake? “Sina jibu lingine?” alisema, “zaidi ya lile ambalo tayari nimelitoa.” TK 105.1
Viongozi wa utawala wa Papa walihuzunika kwani mamlaka yao ingepuuzwa na mtawa huyu duni. Luther alikuwa amezungumza kwa wote kwa heshima ya Kikristo na utulivu, maneno yake yalikuwa huru dhidi ya msisimko na upotovu. Hakujiona yeye bali alihisi tu kuwa alikuwa mbele ya Yule mwenye ukuu usio na kikomo anayewazidi Mapapa, wafalme, na watawala. Roho wa Mungu alikuwepo, akigusa mioyo ya wakuu na ufalme. TK 105.2
Baadhi ya wakuu kwa ushupavu walitambua ujasiri wa msimamo wa Luther. Kundi jingine kwa wakati huo halikuweza kueleza msimamo wao, lakini wakati wa baadaye, wakawa waungaji mkono wasio na hofu wa Matengenezo. TK 105.3
Frederick, mjumbe wa baraza la uchaguzi, aliisikiliza hotuba ya Luther kwa hisia ya kina. Kwa furaha na fahari alishuhudia ujasiri wa Daktari yule na kujiamini kwake, na akaazimu kusimama imara katika kumlinda. Aliona kuwa hekima ya Mapapa, wafalme, na maaskofu iligeuzwa kuwa ubatili kwa uwezo wa ukweli. TK 105.4
Balozi wa Papa alipotambua athari ya hotuba iliyotolewa na Luther, aliazimia kutumia kila njia iliyokuwa ndani ya uwezo wake kuhakikisha Mwanamatengezo huyu anaangushwa. Alitumia ujuzi wa kidiplomasia na lugha yenye ushawishi kumwonesha mfalme kijana, hatari ya kuutoa kafara urafiki na msaada wa Kanisa la Roma kwa ajili ya suala la huyu mtawa asiye na maana. TK 105.5
Siku iliyofuata baada ya jibu la Luther, Charles alilitangazia baraza juu ya uamuzi wake wa kuidumisha na kuilinda dini ya Ukatoliki. Hatua kali zingetakiwa kutumika dhidi ya Luther pamoja na mafundisho yake ya uasi aliyoyatoa: “Nitautoa kafara ufalme wangu, hazina zangu, marafiki zangu, mwili wangu, damu yangu, roho yangu, na uhai wangu...nita...nitafungua kesi dhidi yake na dhidi ya wafuasi wake kwamba ni waasi wasiojali mamlaka, kwa kuwatenga, kwa kuwapiga marufuku, na kwa kila njia itakayopanga kwa umakini kuwaangamiza.” 85Ibid. Hata hivyo, mfalme alitangaza kuwa hakikisho la usalama wa Luther lilikuwa ni lazima lizingatiwe. Ilikuwa ni lazima aruhusiwe kufika nyumbani kwake kwa usalama. TK 105.6