Hali ya usalama ilikuwa njema kule Wartburg, Luther alifurahia kuwa huru mbali na msuguano mkali na vurugu za mapambano. Akiwa amezoea maisha ya shughuli nyingi na mabishano makali, angeweza kuvumilia kwa shida sana kukaa bila shughuli yoyote. Katika siku hizo za upweke hali ya Kanisa ilikuja mbele yake. Aliingiwa na hofia kuwa angeonekana kuwa ni mwoga kwa kujitoa katika shindano. Alijilaumu mwenyewe kwa uvivu na kujishughulisha na mambo kupita kiasi. TK 110.3
Hata hivyo, wakati huohuo alikuwa akifanya mambo mengi kuliko anavyoweza mtu mmoja kutenda. Kalamu yake haikukoma kuandika. Adui zake walistaajabu na kuchanganyikiwa kwa uthibitisho dhahiri kuwa alikuwa bado akifanya kazi. Vijitabu vingi alivyoviandika vilitawanywa katika Ujerumani yote. Pia alitafsiri Agano Jipya katika lugha ya Kijerumani. Kwa karibu mwaka mzima aliendelea kuihubiri Injili kutoka katika Patmo yake ya mlima wa majabali na kukemea makosa ya wakati huo. TK 110.4
Mungu alikuwa amemwondoa mtumishi wake kutoka katika maisha ya hadhara. Katika maisha ya upweke na mashaka na kukimbilia mlimani, Luther alikuwa ameondolewa katika kupata misaada na kusifiwa na wanadamu. Na kwa namna hiyo alikuwa amenusuriwa dhidi ya kiburi na kujiamini ambako mara nyingi husababishwa na mafanikio. TK 111.1
Wakati watu wanapofurahia uhuru unaoletwa kwao kwa njia ya ukweli, Shetani hutafuta kupindisha fikra na upendo wao kutoka kwa Mungu na kuuhamishia kwa mawakala wa kibinadamu, kumpatia heshima mtumishi na kumpuuza Yeye anayeongoza matukio ya ulinzi na utunzaji. Mara nyingi, viongozi wa kidini wanapotukuzwa, huongozwa katika kujitumainia wenyewe. Watu huelekezwa kuwatazama wao kama mwongozo wao badala ya Neno la Mungu. Mungu atayalinda Matengenezo kutoka katika hatari hii. Macho ya wanadamu yalikuwa yameelekezwa kwa Luther kama mfasili wa ukweli; aliondolewa ili macho yote yaweze kuelekezwa kwa Mwumbaji wa milele wa ukweli. TK 111.2