Majuma machache baada ya Luther kuzaliwa kwenye kibanda cha mchimba madini kule Saksoni, Ulric Zwingli naye alizaliwa katika kijumba kidogo cha mchunga ng’ombe katikati ya milima ya Alps. Akiwa amelelewa katika mandhari ya hali ya asili na ya kuvutia, akili yake ilikuwa imevutiwa mapema na ukuu wa Mungu. Kando ya bibi yake alisikiliza visa vichache vya thamani vya Biblia alivyovikusanya huku na huko kutoka kwa watu mashuhuri na mapokeo ya kanisa. TK 112.1
Alipokuwa na umri wa miaka kumi na mitatu alikwenda Bem, mji uliokuwa na wasomi wengi na wenye kuheshimika nchini Uswisi. Hata hivyo, ilizuka hatari mahali hapa. Juhudi za makusudi zilifanywa na watawa kumshawishi ajiunge na nyumba nao. Na kwa uwezo wa Mungu baba yake alipata habari za mipango hiyo ya watawa. Aligundua kuwa ufanisi wa maisha yajayo ya mtoto wake ulikuwa hatarini, kwa hiyo alimwamuru arudi nyumbani. TK 112.2
Agizo lilitekelezwa, lakini kijana hakuridhika kuishi kwa muda mrefu kwenye bonde alikozaliwa, baada ya muda mfupi alirudi masomoni, huku kwa vipindi fulani akienda na wenzake kule Basel. Hapa ndipo Zwingli aliposikia kwa mara ya kwanza neema ya bure kwenye Injili ya Mungu. Alipokuwa akijifunza Kiyunani na Kiebrania hukoWittembach aliongozwa kwenye Maandiko Matakatifu, na hivyo ndivyo miali ya nuru ya mbinguni ilivyoingia katika mioyo ya wanafunzi aliokuwa anawafundisha. Alidai kuwa kifo cha Kristo ni fidia pekee kwa mwenye dhambi. Kwa Zwingli, maneno haya yalikuwa mwali wa kwanza wa nuru iliyotangulia mapambazuko. TK 112.3
Muda mfupi baadaye, Zwingli aliitwa kutoka Basel kwenda kwenye kazi yake ya kudumu. Kazi yake ya kwanza ilikuwa katika parokia iliyokuwa kwenye eneo la milima mirefu. Akiwa amewekwa wakfu kama kasisi, “alijitoa kwa moyo wake wote kuutafuta ukweli wa Mungu.” 95Wylie, bk. 8, ch.5. TK 112.4
Kwa kadri alivyoyachunguza Maandiko, ndivyo ilivyodhihirika kwa usahihi tofauti kati ya ukweli na uasi wa Kanisa la Roma. Alijisalimisha kwenye Biblia kama Neno la Mungu, linalojitosheleza peke yake, na kanuni isiyokosea. Aliona kuwa Biblia ni lazima ijifafanue yenyewe. Alitafuta kila msaada kupata uelewa sahihi na maana yake, na alikaribisha msaada wa Roho Mtakatifu. “Nilianza kumwomba Mungu anipatie nuru yake,” baadaye aliandika, “na kwangu, Maandiko yakaanza kueleweka kwa urahisi.” 96Ibid., bk. 8, ch. 6. TK 113.1
Mafundisho ya imani aliyokuwa akiyafundisha Zwingli hayakutoka kwa Luther. Yalikuwa ni mafundisho ya Kristo. Mwanamatengenezo huyu wa Uswisi alisema, “Ikiwa Luther anamhubiri Kristo anafanya kile ambacho mimi pia ninafanya....Hakuna neno lolote nililoliandika kwenda kwake, wala neno aliloliandika yeye kuja kwangu. Lakini kwa nini?...Ili ionekane namna Roho wa Mungu anavyofanya kazi, kwa kuwa sisi sote, bila kuwa tumekutana kwa vyovyote vile, tunafundisha maagizo ya Kristo kwa namna moja.” 97D’Aubigne, bk. 8, ch. 9. Mwaka 1516 Zwingli alialikwa kuhubiri kwenye nyumba ya watawa kule Einsiedeln. Kama Mwanamatengenezo, angeleta mvuto ambao ungeonekana hadi ng’ambo ya mipaka ya nchi yake aliyozaliwa huko Alps. TK 113.2
Kati ya vivutio vikubwa vilivyokuwa kule Einsiedeln, ilikuwa ni sanamu ya Bikira, iliyosemekana kuwa na nguvu za kutenda miujiza. Juu ya lango la kuingilia kwenye nyumba ya watawa yalikuwepo maandishi yaliyosema, “Ondoleo la dhambi zote linaweza kupatikana hapa.” 98Ibid., 8, ch. 5. Makundi ya watu yalikuja kwenye hekalu la Bikira kutoka sehemu zote za Uswisi, na hata wengine walitokea Ufaransa na Ujerumani. Zwingli alitumia fursa hiyo kutangaza uhuru kupitia Injili kwa watumwa hawa wa imani za mapokeo potovu. TK 113.3
Alisema, “Msidhani kuwa Mungu yumo ndani ya hekalu hili kuliko sehemu nyingine alizoziumba...Je, kazi zisizo na faida, safari ndefu za kwenda kuhiji, sadaka, sanamu, kumwomba msaada Bikira au watakatifu kunaweza kuwapatia neema ya Mungu?...itamfaa nini mtu kanzu inayong’aa, kichwa chenye upara, vazi refu na pana linalofunika mwili wote, ama makubadhi yaliyopambwa kwa dhahabu?” Alisema, “Ni Kristo, aliyetolewa msalabani mara moja, ni kafara na mhanga, ambaye alitosha kuziondoa dhambi zote za waaminio milele zote.” 99Ibid. TK 113.4
Kwa wengi ilikuwa ni masikitiko makubwa kuambiwa kwamba safari yao yenye kuchosha ilikuwa bure. Msamaha unaotolewa bure kwa njia ya Kristo hawakuufahamu. Walikuwa wameridhika na namna Kanisa la Roma lilivyowafundisha. Ilikuwa ni rahisi kutumainia wokovu wao kutoka kwa makasisi na Papa kuliko kutafuta usafi wa moyo. TK 114.1
Lakini kundi jingine lilipokea kwa furaha habari za wokovu kwa njia ya Kristo, na kwa imani waliipokea damu ya Mwokozi kwa ajili ya upatanisho. Hawa walirudi nyumbani kuwafunulia wengine nuru ya thamani waliyokuwa wameipokea. Hivyo ndivyo ukweli ulivyosambazwa kutoka mji mmoja kwenda mji mwingine na idadi ya mahujaji kwenda kwenye hekalu la Bikira ilipungua sana. Kulikuwa na kushuka chini kwa sadaka kwa kiwango kikubwa, na kusababisha kushuka kwa mshahara wa Zwingli uliopatikana kutoka kwenye sadaka hizo. Jambo hili lilimfurahisha sana Zwingli kuona nguvu za mapokeo potuvu zikivunjika. Ukweli uliendelea kukita mizizi katika mioyo ya watu. TK 114.2