Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Pambano Kuu - Contents
  • Results
  • Related
  • Featured
No results found for: "".
  • Weighted Relevancy
  • Content Sequence
  • Relevancy
  • Earliest First
  • Latest First
    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents

    Sura ya 16—Makasisi Wasafiri

    Wanamatengenezo wa Uingereza, wakati wakikataa mafundisho ya Kirumi, walibaki na mifumo mingi ya ibada ya Kirumi. Kwa hiyo, ingawa mamlaka na imani ya Kirumi ilikataliwa, siyo desturi na sherehe chache zilizoingizwa katika ibada ya Kanisa la Uingereza. Ilidaiwa kuwa mambo haya hayakuwa masuala ya dhamiri; kuwa ingawa hayakuwa yameagizwa katika Maandiko, wala kukataliwa katika Maandiko, hayakuwa muhimu, kwa hiyo hayakuwa na ubaya wowote. Uadhimishaji wa mambo hayo ulikuwa na mwelekeo wa kupunguza ufa uliotenganisha makanisa yaliyofanya matengenezo na kanisa la Rumi, na ilisisitizwa kuwa mambo yale yangewahamasisha wafuasi wa Rumi kuikubali imani ya Kiprotestanti.PKSw 220.1

    Kwa wale waliokuwa na msimamo wa kutopenda mabadiliko na wasioyumbishwa, hoja hizi zilionekana kuwa na nguvu. Lakini kulikuwepo na tabaka jingine ambalo halikuwa na mtazamo wa jinsi hiyo. Ukweli kuwa desturi hizi “zilikuwa na mwelekeo wa kupunguza tofauti kati ya Rumi na Matengenezo” (Martyn, volume 5, ukurasa wa 22), katika mtazamo wao ilikuwa hoja yenye nguvu dhidi ya kubaki nazo. Waliziona kuwa ni alama za utumwa ambao walikuwa wameachana nao na ambao wasingependa kuurudia tena. Walifikiria kuwa Mungu ameweka katika neno Lake kanuni zinazoongoza ibada Yake, na kuwa watu hawana uhuru wa kuongeza zingine zaidi ya zile zilizopo au kuzipunguza zilizopo. Mwanzo wa uasi mkuu ulikuwa katika kutafuta kuongezea mamlaka ya kanisa kwa mamlaka ya Mungu. Rumi ilianza kwa kuongeza kile ambacho Mungu hakukikataza, na iliishia katika kukataza kile ambacho Mungu alikuwa amekiagiza waziwazi.PKSw 220.2

    Wengi walikuwa na shauku ya dhati ya kuurudia usafi na usahili ambao ulikuwa sifa kuu ya kanisa la awali. Walichukulia nyingi za desturi zilizozoeleka za Kanisa la Uingereza kama kumbukumbu za ibada ya sanamu, na wasingeweza kwa sababu ya kufuata dhamiri zao kuungana katika ibada yake. Lakini kanisa, likiungwa mkono na mamlaka ya serikali, lisingengeruhusu kufanya tofauti na desturi zake. Mahudhurio katika huduma zake yalitakiwa kisheria, na mikutano kwa ajili ya ibada za kidini ilipigwa marufuku, na watu waliokiuka sheria hiyo walipaswa kufungwa gerezani, kufukuzwa nchini na kulazimika kwenda kuishi uhamishoni, na kuuawa.PKSw 220.3

    Mwanzoni mwa karne ya kumi na saba, mfalme ambaye ndiyo tu alikuwa ametawazwa katika kiti cha enzi cha Uingereza, alitangaza azma yake ya kuwafanya wafuasi wa imani ya Wasafi (Waprotestanti waliotaka mila na desturi za Kikatoliki zisiingizwe katika Kanisa la Uingereza) “ wakubaliane, au ... waharakishwe kuondoka nchini, au vinginevyo mabaya zaidi yawapate.”— George Bancroft, History of the United States of America, pt. 1, ch. 12, par. 6. Wakiwindwa, wakiteswa, na wakifungwa magerezani, Wasafi waligundua kuwa siku zijazo hazikuwa na ahadi ya kuleta hali bora zaidi, na wengi wao walishawishika kuwa ikiwa wanataka kumtumikia Mungu kulingana na msukumo wa dhamiri zao, “ Uingereza ilikuwa ikipungua siku kwa siku kuwa mahali salama pa kuishi.”—J. G. Palfrey, History of New England, ch. 3, par. 43. Baadhi waliazimia kutafuta hifadhi katika nchi ya Uholanzi. Matatizo, hasara, na vifungo viliwakuta. Makusudi yao yalizimwa, na walisalitiwa katika mikono ya maadui zao. Lakini msimamo imara usiokatishwa tamaa haimaye ulishinda, na walipata hifadhi katika pwani rafiki za Jamhuri ya Kidachi.PKSw 220.4

    Katika kukimbia kwao Wasafi waliacha nyumba zao, mali zao, na miundombinu yao ya maisha ya kila siku. Walikuwa wageni katika nchi ya kigeni, miongoni mwa watu wa lugha na mila tofauti. Walilazimika kujifunza kazi ambazo ni mpya na ambazo hawakuzizoea ili kupata mkate wao. Watu wa umri wa kati, waliokuwa wametumia maisha yao katika kulima udongo, iliwapasa sasa kujifunza kazi za ufundi. Lakini waliikubali hali hiyo kwa furaha na hawakupoteza muda kwa kukaa kivivu au kulalamika. Pamoja na kuwa walibanwa na umasikini, walimshukuru Mungu kwa mibaraka ambayo bado waliipata na walipata furaha katika ushirika wao wa kiroho usio na usumbufu wowote. “ Walijua walikuwa wasafiri, na hawakuangalia sana mambo hayo, bali waliinua macho yao mbinguni, nchi yao nzuri, na roho zao zilitulizwa.”—Bancroft, pt. 1, ch. 12, par. 15.PKSw 221.1

    Katikati ya ukimbizi na ugumu, upendo na imani yao viliimarika. Walizitumainia ahadi za Bwana, na Bwana hakuwapungukia wakati wa uhitaji. Malaika wa Bwana walikuwa kando yao, wakiwatia moyo na kuwategemeza. Na mkono wa Mungu ulipoonekana kuwaelekeza wavuke ng'ambo ya bahari, katika nchi ambayo wangeweza kuunda serikali yao wenyewe, na kuwaachia watoto wao urithi wa thamani wa uhuru wa dini, walisonga mbele, bila hofu, katika njia waliyoongozwa na Mungu kuipitia.PKSw 221.2

    Mungu aliruhusu majaribu yawajie watu Wake kuwaandaa kwa ajili ya utekelezaji wa kusudi Lake la neema kwa ajili yao. Kanisa lilikuwa limeshushwa chini, ili liinuliwe juu. Mungu alikuwa karibu kuonesha nguvu Zake kwa ajili ya kanisa, ili kuuonesha ulimwengu ushahidi mwingine kuwa Yeye hawezi kuwatupa watu wanaomtumaini.PKSw 221.3

    Mungu aliongoza matukio na kuifanya hasira ya Shetani na mipango ya watu waovu itangaze utukufu Wake na kuwaleta watu Wake hadi mahali palipo na usalama. Mateso na ukimbizi vilifungua njia ya kuelekea kwenye uhuru.PKSw 221.4

    Walipolazimishwa kwa mara ya kwanza kujitenga na Kanisa la Uingereza, Wasafi waliungana pamoja kwa kiapo makini, kama watu wa Bwana walio huru, “kutembea pamoja katika njia Zake zote ambazo Mungu alikuwa amewafunulia au ambazo angewafunulia.”—J. Brown, The Pilgrim Fathers, uk. 74. Hapa kulikuwa na roho ya kweli ya matengenezo, kanuni ya msingi ya Uprotestanti. Ilikuwa kwa ajili ya kusudi hili ambapo Wasafiri waliondoka Uholanzi na kwenda kutafuta makazi katika Ulimwengu Mpya. John Robinson, mchungaji wao, ambaye kwa uongozi wa Mungu alizuiwa asiambatane nao, katika hotuba yake ya kuwaaga wakimbizi alisema:PKSw 221.5

    “Ndugu zangu, sasa tunakaribia kuachana, na Bwana anajua ikiwa nitaishi na kuona nyuso zenu tena au la. Lakini iwe Bwana atawezesha tuonane au ataona ni vema tusionane tena, ninawaagiza mbele za Mungu na malaika Zake waliobarikiwa mnifuate kwa kiwango kile tu ambacho nimemfuata Kristo. Ikiwa Mungu atawafunulia jambo jingine lo lote kwa njia Yake yo yote ile, muwe tayari kulipokea kama vile ambavyo mngepokea ukweli wowote unaotokana na huduma yangu; kwa kuwa nina hakika Bwana anao ukweli na nuru zaidi inayopaswa kugunduliwa katika neno Lake takatifu.”—Martyn 5:70.PKSw 222.1

    “Kwa upande wangu, siwezi kuonesha masikitiko yangu kiasi cha kutosha kwa ajili ya hali ya makanisa yaliyofanya matengenezo, ambao wamefika kikomo katika dini, na hawaendi tena zaidi ya mafundisho ya matengezo yao waliyonayo sasa. Walutheri hawawezi kuvutwa kwenda mbele zaidi ya kile Luther alichokiona; ... na wafuasi wa Clavin, unaona, wanashikilia sana pale walipoachwa na yule mtu wa Mungu, ambaye hata hivyo hakuona mambo yote. Huu ni msiba unaopaswa kuombolezewa; kwa kuwa ingawa walikuwa taa zilizowaka na kuangaza katika wakati wao, lakini hawakupenya na kuingia katika mashauri yote ya neno la Mungu, lakini kama ikiwa wangekuwa hai sasa, wangekuwa tayari kupokea nuru zaidi kama walivyopokea ile ya kwanza.”—D. Neal, History of the Puritans 1:269.PKSw 222.2

    “Kumbukeni agano la kanisa lenu, ambapo mmekubali kutembea katika njia zote za Bwana, ambazo mmejulishwa au ambazo mtajulishwa. Kumbukeni ahadi na agano lenu kwa Mungu na kwa kila mmoja kwa mwenzake, kupokea nuru yo yote na ukweli wowote mtakaojulishwa kutokana na neno Lake lililoandikwa; lakini hata hilo nalo lisikilizeni, ninawasihi sana, mtakachokipokea kama ukweli, mkilinganishe na kukipima na Maandiko mengine ya ukweli kabla ya kukikubali; kwa kuwa haiwezekani kwa ulimwengu wa Kikristo uliotoka hivi karibuni katika giza nene la mpingakristo, lipokee ujuzi mkamilifu wa ukweli wa neno la Mungu kwa mara moja.”—Martyn, vol. 5, pp. 70, 71.PKSw 222.3

    Ilikuwa shauku kwa ajili ya uhuru wa dhamiri iliyowasukuma Wasafiri kustahimili hatari za safari ndefu ya kuvuka ng'ambo ya bahari, kustahimili ugumu na hatari za jangwa, na mbaraka wa Mungu kujenga, kwenye pwani ya Amerika, msingi wa taifa lenye nguvu nyingi sana. Pamoja na kuwa walikuwa watu waaminifu na watu wanaomcha Mungu, Wasafiri bado walikuwa hawajaelewa kanuni kuu ya uhuru wa dini. Uhuru ambao walitoa kafara kubwa sana kuupata, hawakuwa radhi kuwapa wengine. “Wachache sana, hata miongoni mwa watu wenye fikira pevu na waadilifu wa karne ya kumi na saba, waliokuwa na hata wazo dogo la hiyo kanuni kuu, fundisho la Agano Jipya, linalomkiri Mungu kama mhukumu pekee wa imani ya mwanadamu.”—Ibid. 5:297. Fundisho kuwa Mungu amelipatia kanisa haki ya kutawala dhamiri, kufasili na kuadhibu uzushi, ni moja ya makosa yenye mizizi mirefu ya upapa. Wakati ambapo Wanamatengenezo walikataa imani za Kirumi, haimaanishi hawakuwa na roho ya kukosa uvumilivu kabisa. Giza nene ambalo, kwa zama nyingi za utawala wake, lilifunika ulimwengu wote wa Kikristo, lilikuwa bado halijaondoka kabisa. Alisema mmoja wa wachungaji mashuhuri katika koloni la Ghuba ya Massachussetts: “Kuvumiliana ndiko kulikoufanya ulimwengu uwe kinyume na Kristo; na kanisa halijawahi kupata madhara yo yote kwa kuwaadhibu wazushi.”— Ibid., vol. 5, uk. 335. Kanuni ilitungwa na wakoloni kuwa washiriki wa kanisa peke yao ndio wawe na sauti katika serikali ya kiraia. Aina fulani ya kanisa la serikali lilianzishwa, watu wote wakitakiwa kuchanga pesa kwa ajili ya kutegemeza wachungaji, na mahakimu wakipewa mamlaka ya kudhibiti uzushi. Kwa njia hiyo nguvu ya serikali ikawa katika mikono ya kanisa. Haukupita muda mrefu kabla hatua hizi hazijaleta matokeo yasiyoepukika—mateso.PKSw 222.4

    Miaka kumi na moja baada ya kuanzisha koloni la kwanza, Roger Williams alikuja katika Ulimwengu Mpya. Kama walivyokuwa Wasafiri wa awali alikuja kwa lengo la kupata uhuru wa dini; lakini, tofauti na wao, aliona—kile ambacho wachache sana wakati wake walikuwa wamekiona— kuwa uhuru huu ulikuwa haki isiyoachanika ya watu wote, bila kujali ni watu wa imani gani. Alikuwa mtafutaji wa dhati wa ukweli, na Robinson akishikilia kuwa ilikuwa jambo lisilowezekana kuwa nuru yote ilikuwa bado haijapokelewa kutoka katika neno la Mungu. Williams “alikuwa mtu wa kwanza katika Ulimwengu mpya wa Ukristo kuanzisha serikali ya kiraia kwa kuzingatia fundisho la uhuru wa dhamiri, usawa wa mawazo mbele ya sheria.”—Bancroft, pt. 1, ch. 15, par. 16. Alisema kuwa ilikuwa wajibu wa hakimu kudhibiti uhalifu, lakini siyo kutawala dhamiri. “Umma au mahakimu wanaweza kuamua,” alisema, “nini wajibu wa mtu kwa mtu; lakini wanapojaribu kueleza wajibu wa mtu kwa Mungu, wanatoka nje ya mstari, na haiwezekani kukawa na usalama; kwa sababu ni wazi kuwa ikiwa hakimu anayo mamlaka, anaweza kuamrisha seti moja ya maoni au imani leo na mwingine akatangaza zingine kesho; kama ambavyo imefanyika katika nchi ya Uingereza na wafalme na malkia, na mapapa na mabaraza mbalimbali katika Kanisa la Roma; kiasi kwamba imani zingekuwa mlima wa machafuko.”—Martyn, vol. 5, uk. 340.PKSw 223.1

    Kushiriki ibada za kanisa rasmi la serikali ilikuwa lazima na usiposhiriki adhabu yake ilikuwa faini au kifungo. “Williams aliikataa hiyo sheria; sheria mbaya kuliko zote za Uingereza ilikuwa ile iliyowalazimisha watu kuhudhuria katika kanisa la parokia. Alichukulia tendo la kuwalazimisha watu kuungana na watu wa imani tofauti, kuwa ukiukaji wa wazi wa haki za asili; kuwakokota watu wasio na dini na wasiopenda kuabudu, ilionekana kama kuhitaji unafiki.... ‘Hakuna mtu yeyote anayepaswa kulazimishwa kuabudu, au,’ aliongezea, ‘kuendelea kuabudu, kinyume na mapenzi yao.’ ‘Nini!’ wapinzani walisema kwa mshangao, ‘si mtenda kazi anastahili ujira kwa ajili ya kazi yake?’ ‘Ndiyo,’ alijibu, ‘kutoka kwa wale waliomwajiri.'”— Bancroft, pt. 1, ch. 15, par. 2.PKSw 223.2

    Roger Williams aliheshimiwa na kupendwa kama mchungaji mwaminifu, mtu mwenye vipawa ambavyo havipatikani kwa watu wengi, mwenye uadilifu usiopinda na ukarimu wa kweli; hata hivyo upinzani wake usiotetereka dhidi ya haki ya mahakimu ya kuwa na mamlaka juu ya kanisa, na madai yake kwa ajili ya uhuru wa dini, havikuweza kuvumiliwa. Matumizi ya fundisho hili jipya, ilisisitizwa sana, “yangedhoofisha dola ya msingi na serikali ya nchi.”— Ibid., pt. 1, ch. 15, par. 10. Alihukumiwa kufukuzwa katika makoloni, na, hatimaye, kuepuka kukamatwa, alilazimika kukimbia, katikati ya baridi na dhoruba ya wakati wa baridi, akatokomea katika msitu ulioshikamana.PKSw 224.1

    “Kwa majuma kumi na nne,” alisema, “Niliteseka sana katika msimu mbaya, sikujua mkate au kitanda ni nini.” Lakini “kunguru walinilisha nyikani,” na mti wenye uwazi ulikuwa ndiyo makazi yangu.—Martyn, vol. 5, uk. 349, 350. Hivyo aliendelea na ukimbizi wake wenye maumivu makali katikati ya theluji na msitu usiokuwa na njia, mpaka alipopata hifadhi kwa kabila la Wahindi ambao walimwamini na kumpenda alipowafundisha ukweli wa injili.PKSw 224.2

    Akifika hatimaye, baada ya miezi mingi ya mabadiliko na mizunguko, kwenye fukwe za Ghuba ya Narragansett, alijenga msingi wa dola ya kwanza ya siku hizi ambayo kwa maana halisi ilitambua haki ya uhuru wa dini. Kanuni ya msingi ya koloni la Roger Williams ilikuwa “kila mtu anatakiwa kuwa na uhuru wa kumwabudu Mungu kulingana na nuru ya dhamiri yake mwenyewe.”—Ibid., vol. 5, uk. 354. Jimbo lake dogo hilo, la Rhode Island, lilikuja kuwa hifadhi ya watu walioonewa, na liliongezeka na kufanikiwa mpaka kanuni zake za msingi—za uhuru wa kiraia na wa kidini—zikawa mawe makuu ya pembeni ya Jamhuri ya Amerika.PKSw 224.3

    Katika ile hati kuu ambayo waasisi wa taifa la Marekani waliitangaza kuwa muswada wao wa haki—Tamko la Uhuru—walitangaza: “Tunachukulia kuwa kweli hizi zina ushahidi ulio wazi, kuwa wanadamu wote wameumbwa wakiwa sawa; kwamba wamepewa na Muumbaji wao haki kadhaa zisizoachika; kwamba miongoni mwa hizi haki ni uhai, uhuru, na utafutaji wa furaha.” Na Katiba inatoa uhakikisho, katika maana iliyo wazi, wa uhuru wa dhamiri: “Hakuna kigezo cha kidini kitakachotakiwa kama sifa ya kufanya kazi katika ofisi au dhamana ya umma yo yote katika nchi ya Marekani.” “Bunge la Kongresi halitatunga sheria yo yote inayohusika na uanzishaji wa dini, au kupiga marufuku watu kujihusisha na dini.”PKSw 224.4

    “Waandishi wa Katiba waliitambua kanuni ya milele kuwa uhusiano wa mtu na Mungu wake uko juu ya sheria yo yote ya kibinadamu, na haki zake za dhamiri haziachiki. Mantiki haikuwa ya lazima katika kuelewa uwepo wa huu ukweli; tunatambua uwepo wake katika vifua vyetu. Ni utambuzi huu ambao, katika kushindana kwake na sheria za kibinadamu, umesababisha vifo vya mashahidi wengi kwa njia ya mateso na ndimi za moto. Walihisi kuwa wajibu wao kwa Mungu ulikuwa juu ya maagizo ya wanadamu, na kuwa mwanadamu hakupaswa kuwa na mamlaka juu ya dhamiri zao. Ni kanuni tunayozaliwa nayo ambayo hakuna kitu cho chote kinaweza kuiondoa.”—Congressional documents (U.S.A.), serial No. 200, document No. 271.PKSw 225.1

    Habari zilipoenea katika nchi za Ulaya, kuhusu nchi ambayo kila mtu ana uhuru wa kufurahia matunda ya kazi yake na kutii imani ya dhamiri yake mwenyewe, maelfu walifurika kwenye fukwe na Ulimwengu Mpya. Makoloni yaliongezeka kwa kasi kubwa. “Massachusetts, kwa sheria maalumu, ilitoa ukaribisho na msaada wa bure, kwa gharama za serikali, kwa Wakristo wa taifa lolote ambao wangeruka hadi ng'ambo ya Atlantiki ‘kuepuka vita au njaa, au uonevu wa watesaji wao.’ Kwa njia hiyo wakimbizi na watu waliodharauliwa, kwa mujibu wa sheria, walifanywa kuwa wageni wa dola.”—Martyn, vol. 5, p. 417. Kwa miaka ishirini tangu ujio wa watu wa kwanza kule Plymouth, maelfu kwa maelfu ya Wasafiri walikuja kuishi New England.PKSw 225.2

    Kukidhi lengo lililowaleta, “waliridhika kupata mapato kidogo ya kukidhi kwa kiwango cha chini cha maisha ya kujinyima sana na kufanya kazi za kutoa jasho. Hawakuhitaji chochote kutoka katika ardhi zaidi ya mapato yanayolingana na kazi yao. Hakuna njozi ya dhahabu iliyoonesha utukufu wa uongo kwenye njia yao.... Waliridhishwa na maendeleo ya pole pole lakini yanayosonga mbele ya umoja wao wa kijamii. Walistahimili kwa uvumilivu umaskini wa nyikani, wakimwagilia mti wa uhuru kwa machozi yao, na kwa jasho la nyuso zao, mpaka ulipostawi kikamilifu katika nchi.”PKSw 225.3

    Biblia ilichukuliwa kuwa msingi wa imani yao, chanzo cha hekima, na mwongozo wa uhuru wao. Kanuni zake zilifundishwa kwa bidii katika nyumba, shuleni, na kanisani, na matunda yake yalionekana wazi wazi kwa njia katika kubana matumizi, uwezo mkubwa wa akili, usafi, na kiasi. Mtu angeweza kwa miaka mingi kuishi katika makazi ya Wasafi, “na asione mlevi, au asisikie kiapo, au asikutane na mtu ombaomba.”—Bancroft, pt. 1, ch. 19, par. 25. Ilioneshwa kuwa kanuni za Biblia ni ulinzi wa hakika wa ukuu wa taifa. Makoloni yaliyokuwa dhaifu na yaliyotawanyika huko na huko yalikua na kuunda shirikisho la majimbo yenye nguvu, na ulimwengu ulishikwa na butwaa ulipoona amani na mafanikio ya “kanisa lisilokuwa na papa, na dola isiyokuwa na mfalme.”PKSw 225.4

    Lakini idadi kubwa ya watu waliendelea kufurika katika fukwe za Amerika, wakisukumwa na mamhitaji mengine tofauti kabisa na ya wale Wasafiri wa kwanza. Ingawa imani ya awali na usafi wa kwanza viliendelea kuwa na mvuto mpana na nguvu inayoumba mwenendo, lakini mvuto wake uliendelea kupungua zaidi na zaidi kwa kadiri idadi ilivyoongezeka ya watu waliokuja kutafuta manufaa ya kidunia.PKSw 226.1

    Kanuni iliyofuatwa na wakoloni wa awali, ya kuruhusu washiriki wa kanisa tu kupiga kura au kushika ofisi katika serikali ya kiraia, ilileta matokeo mabaya. Hatua hii ilikuwa imechukuliwa kama njia ya kuhifadhi usafi wa dola, lakini ilisababisha ufisadi ndani ya kanisa. Kuwa na dini kulipofanywa kigezo cha kuwa na haki ya kupiga kura na kushika ofisi katika serikali ya kiraia, watu wengi, kwa kusukumwa na hitaji la mafanikio ya kiduni, walijiunga na kanisa bila badiliko la moyo. Hivyo makanisa yalijikuta yamejaa, kwa kiwango kikubwa, watu wasioongoka; na hata miongoni mwa wachungaji walikuwemo siyo tu wale walioshikilia mafundisho yenye makosa, bali pia waliokuwa hawana uzoefu wowote wa nguvu ya Roho Mtakatifu inayoumba upya. Kwa hiyo ilidhihirisha kwa mara nyingine tena matokeo mabaya, yanayoonekana mara nyingi katika historia ya kanisa tangu tangu siku za Konstantini hadi leo, ya kujaribu kujenga kanisa kwa msaada wa dola, wa kuomba nguvu za kidunia katika kutegemeza injili Yake Yeye aliyesema: “Ufalme wangu siyo wa ulimwengu huu” (Yohana 18:36). Muungano wa kanisa la dola, hata kama ungekuwa mdogo sana, wakati unaweza kuonekana kuuleta ulimwengu karibu na kanisa, unaweza katika kiuhalisia kulileta kanisa karibu na ulimwengu.PKSw 226.2

    Kanuni kuu ambayo ilihubiriwa sana na Robinson na Roger Williams, kuwa ukweli ni endelevu, kuwa inawapasa Wakrtisto kuwa tayari kuikubali nuru yote ambayo inaweza kuangaza kutoka katika neno takatifu la Mungu, haikuonwa na watoto na wajukuu wao. Kanisa la Kiprotestanti la Amerika,— na wale wa Ulaya pia,—waliopendelewa sana kwa kupokea mibaraka ya Matengenezo, walishindwa kuendelea mbele katika njia ya matengenezo. Ingawa watu waaminifu wachache waliinuka, wakati mmoja hadi mwingine, wakatangaza ukweli mpya na kufunua makosa yaliyoshikiliwa kwa muda mrefu, wengi wao, sawa na Wayahudi wa wakati wa Kristo au wafuasi wa upapa wa wakati wa Lutha, waliridhika kuamini kama baba zao walivyoamini na waliridhika kuishi kama baba zao walivyoishi. Kwa hiyo dini kwa mara nyingine tena iliporomoka na kurudi katika hali ya mfumo tu; na makosa na ushirikina ambavyo vilipaswa kuachwa kabisa kama kanisa lingeendelea kutembea katika nuru ya neno la Mungu, vilitunzwa na kustawishwa. Hivyo roho iliyovuviwa na Matengenezo ilipotea, mpaka ikanonekana kwamba kulikuwa na hitaji kubwa la matengenezo katika Makanisa ya Kiprotestanti kama ilivyokuwa katika Kanisa la Roma wakati wa Lutha. Kulikuwa na hali ya kidunia na usingizi mkubwa wa kiroho, aina ile ile ya kuheshimu maoni ya watu, na kuweka nadharia za kibinadamu badala ya mafundisho ya neno la Mungu.PKSw 226.3

    Usambazaji mkubwa wa Biblia katika sehemu ya mwanzo mwa karne ya kumi na tisa, na kwa njia hiyo, nuru kubwa iliyoangazia ulimwengu, haukufuatwa na ukuaji wa maarifa ya ukweli uliofunuliwa, au maisha yaliyobadilishwa na dini. Shetani hakuweza, kama ilivyokuwa katika zama za awali, kuficha neno la Mungu mbali na watu; ilikuwa imewekwa karibu na watu wote na kila mtu angeweza kulipata; lakini ili aweze kutekeleza lengo lake, aliwaongoza wengi kuithamini kidogo sana. Watu walipuuza kuchunguza Maandiko, na kwa njia hiyo waliendelea kukubali tafsiri potovu, na waliendelea kushikilia mafundisho ambayo hayakuwa na msingi katika Biblia.PKSw 227.1

    Baada ya kuona kushindwa kwa juhudi zake za kufutlia mbali ukweli kwa njia ya mateso, Shetani kwa mara nyingine tena alichagua kutumia njia ya ulegezaji masharti ambayo ilisababisha uasi mkuu na uundwaji wa Kanisa la Roma. Aliwashawishi Wakristo waungane wenyewe kwa wenyewe, sasa siyo na upagani, bali na wale ambao, kwa kujiingiza sana katika mambo ya ulimwengu huu, walikuwa wameshakwenda mbali kiasi kwamba walishakuwa waabudu sanamu kweli kweli sawa na wale walioabudu sanamu za kuchonga. Na matokeo ya muungano huu yalikuwa mabaya kama ilivyokuwa katika zama za nyuma; kiburi na ubadhirifu vilijitokeza chini la vazi la dini, na makanisa yalianza kuwa na ufisadi ndani yake. Shetani aliendelea kupotosha mafundisho ya Biblia, na mila na desturi ambazo zingeharibu mamilioni ya watu zilikuwa zikiweka mizizi mirefu. Kanisa lilikuwa likishikilia na kutetea tamaduni hizi, badala ya kushindana kwa ajili “imani ambayo kwanza ilitolewa kwa watakatifu.” Kwa njia hiyo kanuni ambazo Wanamatengenezo walizikuza na kuteseka kwazo zilidhalilishwa. PKSw 227.2

    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents