Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Pambano Kuu - Contents
  • Results
  • Related
  • Featured
No results found for: "".
  • Weighted Relevancy
  • Content Sequence
  • Relevancy
  • Earliest First
  • Latest First
    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents

    Sura ya 33—Udanganyifu Mkuu wa Kwanza

    Tangu mwanzoni kabisa mwa historia ya mwanadamu, Shetani alianza juhudi zake za kudanganya jamii yetu. Yule aliyechochea uasi mbinguni alitamani kuwaleta wakazi wa dunia waungane naye katika vita yake dhidi ya serikali ya Mungu, na ukweli huu ulikuwa ushuhuda wa daima dhidi ya dai alilolitoa Shetani mbinguni, kuwa sheria ya Mungu ni kandamizi na iko kinyume na maslahi ya viumbe Wake. Na zaidi ya hapo, kijicho cha Shetani kiliamshwa alipoona makazi mazuri yaliyoandaliwa kwa ajili ya wawili hao wasiokuwa na dhambi. Alidhamiria kusababisha anguko lao, halafu, baada ya kuwatenganisha na Mungu na kuwaleta chini ya mamlaka yake, angeimiliki dunia na hapa ndipo angesimika ufalme wake akipingana na Yeye Aliye Juu.PKSw 406.1

    Ikiwa Shetani angejifunua katika tabia yake halisi, angepingwa mara moja, kwa kuwa Adamu na Hawa walikuwa wameshaonywa dhidi ya adui huyo wa hatari; lakini alifanya kazi gizani, akificha kusudi lake, ili atekeleze lengo lake kwa ufanisi zaidi. Akitumia nyoka kama mwili wake, kiumbe ambaye wakati ule alikuwa wa kuvutia katika mwonekano wake, alizungumza na Hawa: “Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani?” (Mwanzo 3:1). Ikiwa Hawa angejizuia asiingie katika mahojiano na mjaribu, angekuwa salama; lakini alijiingiza katika mazungumzo na Ibilisi na akawa mhanga wa hila zake. Hivi ndivyo ambavyo bado wengi wanashindwa. Wanatilia mashaka na kuhoji matakwa ya Mungu; na badala ya kutii amri za Mungu, wanapokea nadharia za kibinadamu, ambazo kimsingi zinaficha mitego ya Shetani.PKSw 406.2

    “Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa. Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya” (Aya ya 2-5). Shetani alitangaza kuwa wangekuwa kama Mungu, wakiwa na hekima kubwa zaidi kuliko kabla na wakiwa na uwezo wa kuishi maisha ya hali ya juu zaidi. Hawa alishindwa na jaribu; na kwa ushawishi wa Hawa, Adamu aliongozwa kutenda dhambi. Walikubali maneno ya nyoka, kuwa Mungu hakumaanisha kile alichosema; walimtilia shaka Muumba wao na walidhani kuwa Mungu aliminya uhuru wao na kuwa wangeweza kupata hekima kubwa zaidi na kuinuliwa juu kwa kukiuka sheria Yake.PKSw 406.3

    Lakini Adamu, baada ya dhambi yake, aligundua kitu gani kuhusu maana ya maneno, “Siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika”? Je, aligundua kuwa maneno haya yalimaanisha, kama Shetani alivyomwongoza kuamini, kuwa angeingizwa katika maisha ya hali ya juu? Kama kweli ilikuwa hivyo basi maana yake kulikuwa na faida kubwa iliyopatikana kwa kutenda dhambi, na Shetani alithibitika kuwa mfadhili wa jamii ya wanadamu. Lakini Adamu hakugundua kuwa hii ndiyo ilikuwa maana ya hukumu ya Mungu. Mungu alitangaza kuwa kama adhabu ya dhambi yake, mwanadamu angerudi mavumbini alikotolewa:“Kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi” (Aya ya 19). Maneno ya Shetani, “mtafumbuliwa macho,” yalithibitika kuwa ya kweli katika maana hii pekee: Baada ya Adamu na Hawa kumwasi Mungu, macho yao yalifumbuliwa waone upumbavu wao; hawakujua uovu, na walionja matunda machungu ya kutenda dhambi.PKSw 406.4

    Katikati ya Edeni ulikuwepo mti wa uzima, ambao matunda yake yalikuwa na uwezo wa kuendeleza uhai. Ikiwa Adamu angedumu kuwa mtii kwa Mungu, angeendelea kuwa huru kuuendea mti huu na angeishi milele zote. Lakini alipotenda dhambi, alikatazwa asiuendee mti wa uzima, na alikabiliwa na kifo. Hukumu ya Mungu, “Maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi,” huzungumzia kutoweka kabisa kwa uzima.PKSw 407.1

    Hali ya kutokufa, ambayo mwanadamu aliahidiwa kwa sharti la utii, iliondolewa kwa sababu ya kutenda dhambi. Adamu asingeweza kurithisha kwa watoto wake kile ambacho yeye mwenyewe hakuwa nacho; na kulikuwa hakuna tumaini kwa jamii iliyoanguka dhambini ikiwa Mungu, kwa njia ya kafara ya Mwana Wake, asingerudisha hali ya kutokufa katika uwezekano wa kuipata. Wakati ambapo “mauti iliwafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi,” Kristo alimebatilisha mauti, na “kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili” (Warumi 5:12; 2 Timotheo 1:10). Ni kwa njia ya Kristo pekee hali ya kutokufa inaweza kupatikana. Yesu alisema: “Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima” (Yohana 3:36). Kila mtu anaweza kupata mbaraka huu wa thamani kubwa ikiwa atatimiza masharti. Wote “ambao kwa saburi katika kutenda mema wanatafuta utukufu na heshima na kutokuharibika,” watapokea “uzima wa milele” (Warumi 2:7).PKSw 407.2

    Mdanganyaji mkuu pekee ndiye aliyemwahidi Adamu uzima katika uasi. Na tangazo la nyoka kwa Hawa katika Bustani ya Edeni— “Hakika hamtakufa”—lilikuwa hubiri la kwanza lililowahi kuhubiriwa juu ya hali ya kutokufa kwa roho. Hata hivyo, tangazo hili, likiwa limejengwa juu ya mamlaka ya Shetani pekee, linahubiriwa katika mimbari za ulimwengu wa Ukristo na kupokelewa na watu wengi kwa utayari ule ule wa wazazi wetu wa kwanza. Hukumu ya Mungu, “Roho itendayo dhambi, ndiyo itakayokufa” (Ezekieli 18:20), inatafsiriwa kumaanisha: Roho itendayo dhambi, siyo itakayokufa, bali ndiyo itakayoishi milele. Ni jambo linaloshangaza kuona jinsi wanadamu wanavyoweza kupumbazwa kiasi cha kuamini maneno ya Shetani na kukataa kuamini maneno ya Mungu.PKSw 407.3

    Ikiwa mwanadamu baada ya anguko angeruhusiwa kuuendea mti wa uzima, angeishi milele, na hivyo mwenye dhambi angekuwa na hali ya kutokufa. Lakini makerubi na upanga wa moto vililinda “njia ya mti wa uzima” (Mwanzo 3:24), na hakuna hata mtu mmoja wa familia ya Adamu amewahi kuruhusiwa kupita kizuizi kile na kula matunda yanayotoa uzima. Kwa hiyo hakuna mwenye dhambi ambaye hafi.PKSw 408.1

    Lakini baada ya Anguko, Shetani aliwaagiza malaika zake kufanya juhudi maalumu za kupandikiza imani ya hali ya kutokufa kwa mwanadamu; na baada ya kuwashawishi watu kupokea kosa hili, iliwapasa kuwaongoza kuhitimisha kuwa mwenye dhambi angeweza kuishi katika mateso ya milele. Sasa mfalme wa giza, akifanya kazi kwa njia ya mawakala wake, anamwakilisha Mungu kama jitu katili linalolipiza kisasi, akitangaza kuwa Mungu anawatupa jehanamu wale wote wasiompendeza, na kuwafanya wahisi ghadhabu Yake; na kuwa wakati wakiteseka kwa uchungu usioelezeka na wakihangaika katika ndimi za moto za milele, Muumbaji wao anawatazama na kuridhika.PKSw 408.2

    Kwa hiyo adui mkuu anamvika kwa sifa zake mwenyewe Muumbaji na Mruzuku wa wanadamu. Ukatili ni wa kishetani. Mungu ni pendo; na vyote alivyoviumba vilikuwa vyema, vitakatifu, na vya kupendeza, mpaka dhambi ilipoingizwa kwa njia ya mwasi mkuu wa kwanza. Shetani mwenyewe ni adui anayemjaribu mwanadamu atende dhambi, na ndipo anamwangamiza akiweza; na akifaulu kumwangusha mhanga wake, anafurahia uharibifu anaokuwa amefaulu kuufanya. Akiruhusiwa, anaweza kufutilia mbali jamii yote ya wanadamu katika wavu wake. Isingekuwa kwa ajili ya kuingilia kwa nguvu za Mungu, hakuna mwanadamu ye yote hata mmoja angepona.PKSw 408.3

    Shetani anatafuta kuwashinda watu leo, kama alivyowashinda wazazi wetu wa kwanza, kwa kutikisa imani yao kwa Muumba wao na kuwaongoza kutilia shaka hekima ya serikali Yake na haki ya sheria Yake. Shetani na vibaraka wake wanamwakilisha Mungu kana kwamba Mungu ni mbaya zaidi kuliko wao, ili kuhalalisha uovu na uasi wao. Mdanganyaji mkuu anajitahidi kuhamisha ukatili wa kutisha wa tabia yake na kuuweka juu ya Baba yetu wa mbinguni, ili atengeneze mazingira ya yeye kuonekana kuwa ndiye aliyekosewa alipofukuzwa mbinguni kwa sababu asingekubali kujisalimisha chini ya mtawala dhalimu kama huyo. Anawasilisha mbele ya ulimwengu uhuru ambao wangeweza kuufurahia chini ya utawala wake mwepesi, kinyume na utumwa wa kulazimishwa wa amri kali za Yehova. Kwa njia hiyo anafanikiwa kudanganya watu na kuwafanya wasimtii Mungu.PKSw 408.4

    Ni kero kubwa kiasi gani kwa mhemko wa upendo na rehema, na hata kwa uelewa wetu wa haki, kuna fundisho kuwa waovu waliokufa wanateswa kwa moto wa kiberiti katika jehanamu inayowaka moto milele zote; kuwa kwa ajili ya dhambi za maisha mafupi ya duniani inawapasa kupata mateso wakati wote ambao Mungu atadumu kuwepo. Lakini fundisho hilo limekuwa likifundishwa mahali pengi na bado ni moja ya mafundisho ya imani za msingi za ulimwengu wa Kikristo. Alisema daktari msomi wa theolojia: “Mwonekano wa mateso ya jehanamu utaongeza furaha ya watakatifu milele zote. Wakati wengine walio na asili kama ya kwao na waliozaliwa chini ya mazingira yaliyo sawa na ya kwao, wakitupwa katika taabu ile, na wao wakiwa wameheshimiwa sana, italeta maana ya kwa nini wao wawe na furaha.” Mwingine alitumia maneno haya: “Wakati amri ya kukataliwa ikitekelezwa milele na milele kwa walengwa wa ghadhabu, moshi wa maumivu yao utakuwa ukipanda mbele ya macho ya walengwa wa rehema, ambao, badala ya kushiriki mateso ya hawa waliokataliwa, wao watakuwa wakisema, Amina, Aleluya! Msifuni Bwana!”PKSw 409.1

    Ni wapi, katika kurasa za neno la Mungu, unaweza kupata fundisho hili? Je, waliokombolewa wakiwa mbinguni watapoteza kabisa mhemko wa huruma na kujali, na hata hisia za umoja wa ubinadamu? Je, hisia zitaondolewa na badala yake waliokombolewa watakuwa na hali ya kutojali kwa ukakamavu au ukatili wa mshenzi? Hapana, hapana; hili sio fundisho la Kitabu cha Mungu. Watu wanaowasilisha mawazo yaliyoelezwa katika dondoo zilizotolewa hapo juu wanaweza kuwa watu wenye elimu na hata watu waaminifu, lakini wamepotoshwa na uongo wa Shetani. Anawaongoza kutafsiri vibaya kauli nzito za Maandiko, akiipa lugha rangi ya uchungu na ubaya ambao ni wake yeye mwenyewe, lakini siyo wa Muumbaji wetu. “Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sikufurahii kufa kwake mtu mwovu; bali aghairi mtu mwovu, na kuiacha njia yake mbaya, akaishi. Ghairini, ghairini, mkaache njia zenu mbaya; mbona mnataka kufa, Enyi nyumba ya Israeli?” (Ezekieli 33:11).PKSw 409.2

    Je, Mungu angepata nini, ikiwa tungekubali kuwa Anafurahia kuona mateso yasiyokoma; kuwa anaburudishwa na vilio na kelele na maneno ya laana ya viumbe wake aliowashikilia katika moto wa jehanamu? Je, inawezekana kuwa sauti hizi mbaya zikawa muziki mzuri katika sikio la Upendo wa Milele? Kuna hoja inatolewa kuwa adhabu ya maumivu yasiyokoma kwa waovu itaonesha chuki ya Mungu kwa dhambi kama uovu unaoharibu amani na utaratibu wa ulimwengu. Aha! kufuru ya kutisha! Kana kwamba chuki ya Mungu dhidi ya dhambi ndiyo sababu mateso yanaendelezwa. Kwani, kulingana na mafundisho ya wanatheolojia hawa, kuendelezwa kwa mateso bila tumaini la rehema kunawafanya wahanga maskini wawe na hasira zaidi, na kwa kadiri wanavyomwaga nje hasira zao kwa laana na kufuru, wanaongeza mzigo wao wa hatia milele na milele. Utukufu wa Mungu hauongezwi kwa njia hiyo ya kuongeza mzigo wa dhambi daima milele na milele.PKSw 409.3

    Ni nje ya uwezo wa akili ya mwanadamu kukadiria uovu ambao umefanywa kwa njia ya fundisho la uongo la mateso ya adhabu ya milele. Dini ya Biblia, ikiwa imejaa upendo na wema, na ikiwa imesheheni huruma tele, inatiwa giza kwa ushirikina na kuvikwa hofu kuu. Tunapotafakari kiasi cha rangi za uongo ambazo Shetani ameipaka tabia ya Mungu, tunaweza kushangaa kama kweli Muumbaji wetu mwenye rehema anaheshimiwa, anahofiwa, na hata anachukiwa? Mawazo ya kutisha kuhusu Mungu ambayo yamesambazwa ulimwenguni kote kutokana na mafundisho yanayotolewa katika mimbari yamewafanya maelfu, ndiyo, mamilioni, wawe na mashaka na Mungu, na wengine wawe makafiri kabisa.PKSw 410.1

    Nadharia ya mateso ya adhabu ya milele ni moja ya mafundisho ya uongo yanayotengeneza mvinyo ya machukizo ya Babeli, ambayo anawanywesha watu wa mataifa yote (Ufunuo 14:8; 17:2). Ukweli kuwa watumishi wa Kristo walilipokea fundisho hili la uongo na kulihubiri kutoka katika meza takatifu ni siri ya ajabu. Walilipokea kutoka Roma, kama walivyopokea sabato ya uongo. Ni kweli, limefundishwa na watu wanaoheshimiwa sana na watu walio wema kabisa; lakini nuru kuhusu somo hili ilikuwa haijawafikia kama ilivyotufikia sisi. Waliwajibika tu kwa ile nuru iliyomulika katika wakati wao; sisi tunawajibika kwa ajili ya nuru inayomulika katika wakati wetu. Ikiwa tutaacha ushuhuda wa neno la Mungu, na kupokea mafundisho ya uongo kwa sababu baba zetu waliyafundisha, tunanaswa katika hukumu iliyotangazwa juu ya Babeli; tunakunywa mvinyo ya machukizo ya Babeli.PKSw 410.2

    Tabaka kubwa la wale ambao fundisho la mateso ya adhabu ya milele halileti maana kwao wanasukumwa upande mwingine wa kosa hilo lililo kinyume cha lile la kwanza. Wanaona kuwa Maandiko yanamwakilisha Mungu kama mwenye uhai mwenye upendo na huruma, na hawawezi kuamini kuwa atawatupa viumbe Wake katika jehanamu inayowaka moto milele. Lakini kushikilia kuwa roho kwa asili haifi, hawaoni njia nyingine isipokuwa kuhitimisha kuwa wanadamu wote hatimaye wataokoka. Wengi wanachukulia vitisho vya Biblia kama vile vimepangwa kuwatisha tu watu wawe watiifu, na siyo kweli kuwa vitatimizwa. Hivyo basi, mwenye dhambi anaweza kuishi katika anasa za kibinafsi, huku akipuuza matakwa ya Mungu, na bado atarajie hatimaye kupokelewa na kukubaliwa Naye. Fundisho hilo, ambalo hudaiwa kujengwa juu ya rehema za Mungu, lakini likipuuza uwepo wa haki ya Mungu, huufurahisha moyo wa mwanadamu asiye na Mungu na unawaimarisha watu waovu katika uovu wao.PKSw 410.3

    Kuonesha jinsi wanaoamini katika wokovu wa watu wote wanavyopotosha Maandiko ili kuhalalisha imani zao potofu zinazoangamiza roho, inatupasa kutaja tu kauli zao wenyewe. Wakati wa mazishi ya kijana mwanaume asiyekuwa na dini, aliyekuwa amekufa kwa ghafla kwa sababu ya ajali, mchungaji anayeamini katika wokovu wa watu wote alichagua kama aya yake kuu kauli ya Maandiko inayomhusu Daudi: “Kwa kuwa ametulizwa kwa habari ya Amnoni, kwa maana amekufa” (2 Samweli 13:39).PKSw 410.4

    “Ninaulizwa mara kwa mara,” mhubiri alisema, “kuhusu hatima ya wale wanaoondoka duniani wakiwa wenye dhambi, wanaokufa, pengine, wakiwa wamelewa, wanaokufa wakiwa na madoa mekundu ya uhalifu wa kijinai bila kuoshwa na kuondolewa kwenye majoho yao, au wanaokufa kama alivyokufa kijana huyu, bila kukiri wakati wowote au kupata uzoefu wo wote ule wa kidini. Tunaridhishwa na Maandiko; jibu lao linatatua tatizo kubwa sana. Amnoni alikuwa mwenye dhambi kuliko kawaida; hakuwa na muda wa kutubu; alikuwa amelewa pombe, na akiwa amelewa aliuawa. Daudi alikuwa nabii; na hivyo basi, ni lazima alikuwa na uwezo wa kujua ikiwa hatima ya Amnoni ingekuwa nzuri au mbaya katika ulimwengu ujao. Maelezo kutoka katika moyo wa Daudi yalikuwa na ujumbe gani? ‘Mfalme Daudi akatamani kutoka kumwendea Absalomu kwa kuwa ametulizwa kwa habari ya Amnoni, kwa maana amekufa’ (Aya ya 39).”PKSw 411.1

    “Na ni fundisho gani tunalipata kutokana na lugha hii? Sio kuwa mateso yasiyokoma hayakuwa sehemu ya imani yake ya kidini? Kwa hiyo tunaelewa; na hapa tunagundua hoja ya ushindi inayounga mkono nadharia yenye ukarimu, inayofurahisha zaidi, yenye nuru kubwa zaidi ya hatima ya usafi na amani kwa watu wote. Daudi alifarijika alipoona mwanawe amekufa. Kwa nini afarijike? Kwa sababu ya jicho la kiunabii aliweza kuona mbele katika wakati ujao wenye utukufu na akaona kuwa mwanawe akiwa ameepushwa na majaribu yote, akiwa ameachiwa kutoka katika utumwa na akiwa ameoshwa uchafu wote wa dhambi, na baada ya kutakaswa kiasi cha kutosha na kupewa nuru ya kutosha, aliruhusiwa kuingia katika mkutano wa roho zilizokwisha kupaa na zinazofurahia. Faraja pekee ilikuwa, kwa kuondolewa katika hali ya sasa ya dhambi na mateso, mwanawe mpendwa alikuwa amekwenda mahali ambapo pumzi za juu za Roho Mtakatifu zingemulika nuru juu ya roho yake yenye giza, ambapo akili yake ingefunguliwa ili kupokea hekima ya mbinguni na furaha tamu ya upendo usio na kikomo, na hivyo kupata asili iliyotakaswa na kufurahia pumziko pamoja na jamii yote ya warithi wa mbinguni.PKSw 411.2

    “Katika mawazo haya ingekuwa vema tueleweke kuwa, tunaamini kuwa wokovu wa mbinguni hautegemei kitu cho chote ambacho tunaweza kukifanya katika maisha haya; wala juu ya badiliko la sasa la moyo, wala imani ya sasa, au kukiri kwa sasa kuwa una dini.”PKSw 411.3

    Hivyo, mtu anayedai kuwa ni mtumishi wa Kristo, anakariri uongo uliosemwa na nyoka katika bustani ya Edeni: “Hakika hamtakufa.” “Siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu.” Anadai kuwa, watu wenye dhambi kupindukia—mwuaji, mwizi, na mzinzi—baada ya kifo, wataandaliwa kuingia katika furaha ya milele.PKSw 411.4

    Na ni kutokana na nini huyu mpotoshaji wa Maandiko anapata hitimisho lake? Kutoka sentensi moja inayoeleza kujisalimisha kwa Daudi kwa uongozi wa Mungu. Roho yake ilitamani “kutoka kumwendea Absalomu kwa kuwa ametulizwa kwa habari ya Amnoni, kwa maana amekufa.” Baada ya makali ya uchungu wake kupozwa kwa kadiri muda ulivyozidi kusonga mbele, mawazo yake yalihama kutoka kwa mtoto aliyekwisha kufa yakaelekea kwa mwanawe aliye hai, akiwa amejiachia na kujisalimisha kwa Mungu kwa sababu ya hofu ya adhabu ya haki ya Amnoni kwa sababu ya uhalifu wake mwenyewe. Na huu ndiyo ushahidi kuwa Amnoni, mbakaji wa dada yake na mlevi wa pombe, mara baada ya kifo chake alichukuliwa hadi katika makao ya amani, pale akatakaswa na kuandaliwa kwenda kuishi na malaika wasiokuwa na dhambi! Hadithi ya kufurahisha kweli, inayopendeza moyo usio na Roho wa Mungu! Hili ni fundisho la Shetani mwenyewe, na linamsaidia katika kazi yake kwa ufanisi mkubwa. Je, tushangae, kwa fundisho kama hilo, uovu ukizidi kuongezeka?PKSw 412.1

    Njia iliyofuatwa na huyu mwalimu mmoja wa uongo ni mfano wa njia zinazofuatwa na wengine wengi. Maneno machache ya Maandiko yanatenganishwa na muktadha, ambao mara nyingi ungeonesha maana yake kuwa kinyume kabisa na tafsiri inayotolewa kwa maneno hayo; na aya hizo zilizokatwa katwa zinapotoshwa na kutumiwa kama uthibitisho wa mafundisho ambayo hayana msingi katika neno la Mungu. Ushuhuda uliotolewa kuwa Amnoni mlevi yuko mbinguni ni tafsiri inayopingana moja kwa moja na kauli za wazi na chanya za Maandiko kuwa hakuna mlevi atakayeurithi ufalme wa Mungu (1 Wakorintho 6:10). Ndivyo hivyo wenye mashaka, wasioamini, na wenye kushuku hugeuza ukweli kuwa uongo. Na watu wengi wamedanganywa kwa uongo wao na kubembelezwa hadi wanasinzia katika kitanda cha usalama wa kimwili.PKSw 412.2

    Kama ingekuwa ni kweli kuwa roho za wanadamu wote hupita moja kwa moja na kuingia mbinguni wakati wa saa ya kufa, basi wote tungetamani kufa kuliko kuishi. Wengi wameongozwa na imani hii kukatisha maisha yao. Wanapozidiwa na matatizo, mashaka, na kukatishwa tamaa, inaonekana kuwa jambo rahisi kukata uzi mwepesi wa maisha na kupaa kwenda katika amani ya ulimwengu wa milele.PKSw 412.3

    Mungu ametoa katika neno Lake ushahidi wa kutosha kuwa atawaadhibu wavunjaji wa sheria. Wale wanaojifariji kwa kujidanganya kuwa Yeye ni mwenye rehema nyingi sana kiasi kwamba hawezi kutekeleza haki kwa mwenye dhambi, hebu na watazame msalaba wa Kalwari. Kifo cha Mwana wa Mungu asiyekuwa na doa kinathibitisha kuwa “mshahara wa dhambi ni mauti,” kuwa kila uvunjaji wa sheria ya Mungu lazima upokee adhabu yake ya haki. Kristo alifanyika dhambi kwa ajili ya mwanadamu. Alibeba hatia ya dhambi, na alivumilia kufichwa kwa uso wa Baba Yake, mpaka moyo Wake ukavunjika na uhai Wake kutoka. Kafara yote hii ilifanywa ili mwenye dhambi akombolewe. Kulikuwa hakuna njia nyingine ambayo ingewezesha mwanadamu aokolewe kutoka katika adhabu ya dhambi. Na kila mtu anayekataa kuwa mshirika wa upatanisho uliopatikana kwa gharama kubwa kama hiyo atalazimika kubeba katika nafsi yake mwenyewe hatia na adhabu ya uasi wake.PKSw 412.4

    Hebu tuangalie kile ambacho Biblia inafundisha kuhusu watu wasiomcha Mungu na wasiotubu, ambao, mtetezi wa wokovu kwa wote bila kujali hali yao ya kiroho, anasema watakwenda mbinguni kukaa pamoja na malaika watakatifu, wenye furaha.PKSw 413.1

    “Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure” (Ufunuo 21:6). Ahadi hii ni kwa wale tu wenye kiu. Ni wale tu walio na hitaji la maji ya uzima, na wanayatafuta kwa gharama ya vitu vyote vingine, ndio watakaopewa. “Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu” (Aya ya 7). Hapa, pia, masharti yameelezwa wazi. Ili kurithi vitu vyote, inatupasa kuipinga na kuishinda dhambi.PKSw 413.2

    Bwana anatangaza kupitia kwa nabii Isaya: “Waambieni wenye haki ya kuwa watakuwa heri, kwa maana watakula matunda ya matendo yao.” “Ole wake mtu mbaya; shari itakuwa kwake, kwa maana atapewa ijara ya mikono yake” (Isaya 3:10, 11). “Ajapokuwa mwenye dhambi amefanya maovu mara mia,” anasema mwenye hekima, “akazidisha siku zake; lakini hata hivyo najua hakika ya kwamba itakuwa heri kwao wamchao Mungu, wenye kicho mbele zake; walakini haitakuwa heri kwa mwovu” (Mhubiri 8:12, 13). Na Paulo anashuhudia kuwa mwenye dhambi anajiwekea “akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira na ufunuo wa hukumu ya haki ya Mungu, atakayemlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake;” “dhiki na shida juu ya kila nafsi ya mwanadamu atendaye uovu” (Warumi 2:5, 6, 9).PKSw 413.3

    “Hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu” (Waefeso 5:5). “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao” (Waebrania 12:14). “Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake. Huko nje wako mbwa, na wachawi, na wazinzi, na wauaji, na hao waabuduo sanamu, na kila mtu apendaye uongo na kuufanya” (Ufunuo 22:14, 15).PKSw 413.4

    Mungu ametoa tamko kwa wanadamu kuhusu tabia Yake na mbinu Yake ya kushughulikia dhambi. “Bwana akapita mbele yake, akatangaza, Bwana, Bwana, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli; mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi; wala si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe” “Wakosaji wataangamizwa pamoja, Wasio haki mwisho wao wataharibiwa” (Zaburi 145:20; 37:38). Uwezo na mamlaka ya serikali ya Mungu vitatumika kukomesha uasi; lakini udhihirisho wote wa adhabu ya haki utapatana kikamilifu na tabia ya Mungu ambaye ni mwenye rehema, mvumilivu, na mkarimu.PKSw 413.5

    Mungu halazimishi nia au uamuzi wa mtu ye yote. Yeye hafurahii utii usiotumia akili. Anatamani kuwa viumbe wa mikono Yake wampende kwa sababu anastahili kupendwa. Angependa kuwaona wakimtii kwa sababu wametambua kwa kutumia akili zao wenyewe kuwa Mungu ni mwenye hekima, haki, na ukarimu. Na wote walio na utambuzi sahihi wa sifa hizi watampenda kwa sababu wanavutwa Kwake kwa kuvutiwa na sifa Zake.PKSw 414.1

    Kanuni za ukarimu, rehema, na upendo, zilizofundishwa na Mwokozi wetu akazionesha kwa vitendo na, ni nakala ya mapenzi na tabia ya Mungu. Kristo alisema kuwa hakufundisha chochote kile isipokuwa kile tu alichokipokea kutoka kwa Baba Yake. Kanuni za serikali ya Mungu zinapatana kikamilifu na kanuni ya Mwokozi, “Wapendeni adui zenu.” Mungu anatekeleza hukumu juu ya waovu kwa manufaa ya ulimwengu wote, na hata kwa wale ambao hukumu inatekelezwa juu yao. Angeweza kuwafanya wawe na furaha ikiwa angeweza kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria za serikali Yake na haki ya tabia Yake. Anawazungushia viashiria vya upendo Wake, anawapa fursa ya kuijua sheria Yake, na anawafuatilia kwa kuwapa fursa ya rehema Yake; lakini wanadhihaki upendo Wake, wanahesabu sheria Yake kuwa si kitu, na wanatupilia mbali rehema Yake. Wakati daima wakipokea zawadi Zake, wanamkosea heshima Mtoaji; wanamchukia Mungu kwa sababu wanajua anachukia dhambi zao. Bwana anavumilia sana ukengeufu wao; lakini saa ya uamzi itafika hatimaye, wakati mustakabali wao utakapoamriwa. Je, atawakamata hawa waasi na kuwafunga kwa mnyororo upande Wake? Je, atawalazimisha kufanya mapenzi Yake?PKSw 414.2

    Wale ambao wamemchagua Shetani kuwa kiongozi wao na wanatawaliwa na nguvu yake hawako tayari kuingia katika uwepo wa Mungu. Kiburi, uongo, anasa, ukatili, vimejengeka katika tabia zao. Je, wanaweza kuingia mbinguni na kuishi milele na wale ambao waliwadhihaki na waliwachukia duniani? Ukweli kamwe hautakubalika kwa mtu muongo; unyenyekevu hautamridhisha mtu mwenye kujiinua na mwenye kiburi; utakatifu haukubaliki kwa mtu aliye fisadi; upendo usio na upendeleo haumvutii mtu mchoyo. Mbingu itakuwa na chanzo gani cha furaha kwa watu ambao mawazo yao yote yanatafuta mambo ya kidunia na maslahi ya kichoyo?PKSw 414.3

    Ikiwa wale ambao maisha yao yametumiwa katika uasi dhidi ya Mungu wangepelekwa kwa ghafla mbinguni na kushuhudia hali ya juu na takatifu ya ukamilifu ambao daima uko pale,—kila roho ikiwa imejazwa kwa upendo, na kila uso uking'ara kwa furaha, muziki wa kufurahisha wenye sauti tamu ukiinuka juu kwa heshima ya Mungu na Mwanakondoo, na miale ya nuru ikimwagwa juu ya waliokombolewa kutoka katika uso Wake Yeye aketiye juu ya kiti cha enzi,—je, wale ambao mioyo yao imejaa chuki dhidi ya Mungu, na dhidi ya ukweli na utakatifu wangeweza kuchanganyika na mkutano huo wa mbinguni na kujiunga nao kuimba nyimbo za sifa? Je, wangeweza kustahimili utukufu wa Mungu na wa Mwanakondoo? Hapana, hapana; miaka ya rehema ilitolewa kwao, ili waweze kujenga tabia za mbinguni; lakini hawakufundisha akili kupenda utakatifu; hawakujifunza lugha ya mbinguni, na sasa muda wao wa kujifunza umeshapita. Maisha ya uasi dhidi ya Mungu hayawapi sifa ya kuishi mbinguni. Usafi wake, utakatifu wake, na amani yake vingekuwa mateso kwao; utukufu wa Mungu ungekuwa moto ulao kwao. Wangetamani kukimbia kutoka mahali pale patakatifu. Wangekuwa tayari kukaribisha kifo, ili wafichwe wasiuone uso Wake Yeye aliyekufa ili awakomboe. Hatima ya waovu inaamriwa na uchaguzi wao wenyewe. Kutokwenda mbinguni kwa waovu ni hiari yao wenyewe, na ni haki na rehema ya Mungu.PKSw 415.1

    Kama maji ya Gharika ya Nuhu, moto wa siku kuu ya mwisho hutangaza hukumu kuwa waovu hawaponyeki. Hawana mwelekeo wa kujisalimisha kwa mamlaka ya Mungu. Nia yao ilitumika kuasi; na maisha yao yanapokoma, tayari wameshachelewa kugeuza mwelekeo wa mawazo yao katika upande wa kinyume chake, wamechelewa kuacha makosa na kuwa watiifu, kuacha chuki na kuwa na upendo.PKSw 415.2

    Katika kuhifadhi maisha ya Kaini mwuaji, Mungu alitoa mfano kwa ulimwengu kile ambacho kingekuwa matokeo ya kumruhusu mwenye dhambi aendelee kuishi maisha ya uovu usiodhibitiwa. Kwa njia ya mvuto wa mafundisho ya Kaini na ya mfano wake, umati mkubwa wa uzao wake uliongozwa kuishi maisha ya dhambi, hadi “maovu ya mwanadamu yakawa makubwa duniani” na “kila kusudi analowaza moyoni mwake likawa baya tu sikuzote” “dunia ikaharibika mbele za Mungu, dunia ikajaa dhuluma” (Mwanzo 6:5, 11).PKSw 415.3

    Kwa kuuhurumia ulimwengu, Mungu alifutilia mbali wakazi wa dunia waovu wa wakati wa Nuhu. Kwa rehema Zake, Mungu aliwaangamiza wakazi wa Sodoma. Kwa njia ya nguvu ya uongo wa Shetani, watendaji wa uovu huungwa mkono na kuvutia watu, na kwa njia hiyo daima wanawaongoza wengine kufanya uasi. Ilikuwa hivyo katika siku za Kaini na ilikuwa hivyo katika siku za Nuhu, na ilikuwa hivyo katika siku za Ibrahimu na Lutu; na iko hivyo wakati wetu. Ni kwa sababu ya rehema kwa ajili ya ulimwengu Mungu atawaangamiza, hatimaye, wote wanaotupilia mbali neema Yake.PKSw 415.4

    “Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu” (Warumi 6:23). Wakati uzima ni urithi wa wenye haki, mauti ni mshahara wa waovu. Musa aliwatangazia Waisraeli: “nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya” (Kumbukumbu 30:15). Mauti inayozungumziwa katika maandiko haya siyo ile aliyotangaziwa Adamu, kwa kuwa wanadamu wote wanapata adhabu ya kosa lake. Hii ni “mauti ya pili” ambayo ni kinyume na uzima wa milele.PKSw 416.1

    Kufuatia dhambi ya Adamu, mauti ilirithishwa hadi kwa jamii yote ya wanadamu. Wote kwa pamoja wanaenda kaburini. Na kupitia fursa ya mpango wa wokovu, wote wataletwa kutoka katika makaburi yao. “Kutakuwa na ufufuo wa wafu, wenye haki na wasio haki pia;” “kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa” (Matendo 24:15; 1 Wakorintho 15:22). Lakini tofauti imewekwa kati ya matabaka haya mawili ya watu wanaofufuliwa. “Watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu” (Yohana 5:28, 29). Wale ambao watakuwa “wamehesabiwa kustahili” kufufuliwa kwa ajili ya uzima wanaitwa “heri na watakatifu.” “Juu ya hao mauti ya pili haina nguvu” (Ufunuo 20:6). Lakini wale ambao, kwa njia ya msamaha na imani, hawakupata msamaha, itawapasa kupata adhabu ya dhambi yao—“mshahara wa dhambi.” Wanapata adhabu inayotofautiana katika urefu wa muda na uzito wake, “kwa kadiri ya matendo yao,” lakini hatimaye wakiishia katika mauti ya pili. Kwa kuwa haiwezekani kwa Mungu, kulingana na matakwa ya haki na rehema Yake, kumwokoa mwenye dhambi na dhambi zake, Mungu hampi maisha ambayo dhambi zake zimempokonya na ambayo amethibitika kutostahili kuwa nayo. Mwandishi aliyevuviwa anasema: “Maana bado kitambo kidogo asiye haki hatakuwapo, Utapaangalia mahali pake wala hatakuwapo.” Na mwingine anatangaza: “Nao watakuwa kana kwamba hawakuwa kamwe” (Zaburi 37:10; Obadia 16). Wakiwa na aibu, wanazama katika upotevu usio na matumaini, wa milele.PKSw 416.2

    Huo ndio utakuwa mwisho wa dhambi, pamoja na tabu na uharibifu uliotokana nayo. Anasema mtunga zaburi: “Umewakemea mataifa; Na kumwangamiza mdhalimu; Umelifuta jina lao milele na milele; Adui wamekoma na kuachwa ukiwa milele” (Zaburi 9:5, 6). Yohana, katika Ufunuo, akitazama mbele hadi katika maisha ya umilele, anasikia wimbo wa ulimwengu wote wa sifa bila kuharibiwa na noti moja iliyo nje ya mwafaka. Kila kiumbe mbinguni na duniani alisikika akimtukuza Mungu (Ufunuo 5:13). Hakutakuwa na roho hata moja iliyopotea itakayomkufuru Mungu ikihangaika katika maumivu ya moto usiokoma; hakuna wenye uhai masikini katika jehanamu watakaochanganya vilio vyao na nyimbo za waliokombolewa.PKSw 416.3

    Juu ya kosa la msingi la hali ya asili ya kutokufa, limejengwa fundisho la ufahamu katika hali ya kifo—fundisho ambalo, sawa na mateso katika moto wa milele, liko kinyume na mafundisho ya Maandiko, kinyume na uelewa wenye mantiki, na kinyume na hisia zetu za ubinadamu. Kwa mujibu wa imani iliyoenea mahali pengi, waliokombolewa mbinguni wanajua yote yanayotokea duniani na hususani maisha ya marafiki zao ambao wamewaacha nyuma. Lakini ni kwa jinsi gani hili linaweza kuwa chanzo cha furaha kwa watu waliokufa kujua taabu za walio hai, kushuhudia dhambi zilizotendwa na wapendwa wao, na kuwaona wakikabiliana na huzuni, kukatishwa tamaa, na maumivu ya maisha? Ni kwa kiasi gani amani ya mbinguni ingefurahiwa na wale ambao walikuwa wakiwazunguka marafiki zao waliowaacha duniani? Na ni kwa kiasi gani inakera imani kuwa mara tu pumzi inapoondoka mwilini roho ya mtu asiyetubu inapelekwa moja kwa moja jehanamu! Na ni kiasi gani cha maumivu kinawapata wanaowaona marafiki zao wakienda makaburini bila maandalizi, kuingia katika mateso na dhambi ya milele! Wengi wamepata hali kuchanganyikiwa kwa sababu ya wazo hili linalosumbua akili.PKSw 417.1

    Maandiko yanasema nini kuhusu mambo haya? Daudi anatangaza kuwa mwanadamu hana fahamu mautini. “Pumzi yake hutoka, huurudia udongo wake, Siku hiyo mawazo yake yapotea” (Zaburi 146:4). Sulemani anatoa ushuhuda huo huo: “Walio hai wanajua ya kwamba watakufa; lakini wafu hawajui neno lo lote.” “Mapenzi yao na machukio yao, na husuda yao, imepotea yote pamoja; wala hawana sehemu tena katika jambo lo lote lililofanyika chini ya jua.” “kwa kuwa hakuna kazi, wala shauri, wala maarifa, wala hekima, huko kuzimu uendako wewe” (Muhubiri 9:5, 6, 10).PKSw 417.2

    Wakati, kama jibu kwa sala yake, maisha ya Hezekia yalirefushwa kwa miaka kumi na tano, mfalme mwenye shukrani alimwimbia Mungu wimbo wa sifa kwa ajili ya rehema Yake kuu. Katika wimbo huu anaeleza sababu kwa nini anafurahia hivyo: “Kuzimu hakuwezi kukusifu; mauti haiwezi kukuadhimisha; Wale washukao shimoni hawawezi kuitarajia kweli yako. Aliye hai, naam, aliye hai, ndiye atakayekusifu, kama mimi leo” (Isaya 38:18, 19). Theolojia inayofundishwa na watu mengi hueleza kuwa wenye haki waliokufa wako mbinguni, wakiwa wameingia katika raha na wakimsifu Mungu kwa ulimi ulio na hali ya kutokufa; lakini Hezekia hakuona mustakabali wenye utukufu kama huo mautini. Maneno yake yanapatana na ushuhuda wa mtunga zaburi: “Mautini hapana kumbukumbu lako; Katika kuzimu ni nani atakayekushukuru?““Sio wafu wamsifuo Bwana, Wala wo wote washukao kwenye kimya” (Zaburi 6:5; 115:17).PKSw 417.3

    Petro katika Siku ya Pentekoste alieleza kuwa mzee Daudi “alifariki akazikwa, na kaburi lake liko kwetu hata leo.” “Maana Daudi hakupanda mbinguni” (Matendo 2:29, 34). Ukweli kuwa Daudi yuko kaburini mpaka wakati wa ufufuo huthibitisha kuwa wenye haki hawaendi mbinguni wakati wanapokufa. Ni kwa njia ya ufufuo pekee, na kwa njia ya ukweli kuwa Kristo alifufuka, ambapo Daudi anaweza hatimaye kuketi mkono wa kuume wa Mungu.PKSw 417.4

    Na Paulo alisema: “Maana kama wafu hawafufuliwi, Kristo naye hakufufuka. Na kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu. Na hapo wao nao waliolala katika Kristo wamepotea” (1 Wakorintho 15:16-18). Ikiwa kwa miaka elfu nne wenye haki walikuwa wanakwenda moja kwa moja mbinguni wakati wa kufa, Paulo angesemaje kuwa ikiwa hakuna ufufuo, “wao nao waliolala katika Kristo wamepotea”? Ufufuo usingekuwa wa muhimu.PKSw 418.1

    Mfia dini Tyndale, akizungumzia hali ya wafu, alisema: “Ninakiri wazi wazi, siamini kuwa tayari wako katika utukufu kamili ambao Kristo anao, au walionao malaika wateule wa Mungu. Wala sio fundisho mojawapo la imani yangu; kwani ikiwa ingekuwa hivyo, bila shaka kuhubiri ufufuo wa mwili kungekuwa jambo lisilo na maana yoyote ile.”—William Tyndale, Preface to New Testament (ed. 1534). Reprinted in British Reformers—Tindal, Frith, Barnes, page 349.PKSw 418.2

    Ni ukweli usiokanushika kuwa tumaini la mbaraka wa kutokufa wakati wa kufa limesababisha watu wengi kupuuzia fundisho la Biblia kuhusu ufufuo. Mwelekeo huu ulitolewa maelezo na Dkt Adam Clarke, akisema: “Fundisho la ufufuo linaonekana kuwa lilikuwa muhimu zaidi kwa Wakristo wa awali kuliko ilivyo hivi sasa! Hili limetokeaje? Mitume walikuwa wakilisisitizia, na wakiwahamasisha wafuasi wa Mungu kuwa na bidii, utii, na furaha kupitia fundisho hilo. Lakini warithi wao wa siku hizi kwa nadra sana hulitaja! Mitume walihubiri hivyo, na Wakristo wa awali waliamini hivyo; kadhalika sisi tukihubiri hivyo, wasikilizaji wetu wataamini hivyo. Hakuna fundisho katika injili ambalo limepewa mkazo mkubwa zaidi kama hili; na hakuna fundisho katika mfumo wa sasa wa mahubiri ambalo limepuuzwa zaidi kuliko hili!”—Commentary, remarks on 1 Corinthians 15, paragraph 3.PKSw 418.3

    Jambo hili limeendelea kuwepo mpaka ukweli wenye utukufu wa ufufuo umefunikwa na umepotea machoni pa ulimwengu wa Kikristo. Kwa hiyo mwandishi mashuhuri wa kidini, akifafanua maneno ya Paulo katika 1 Wathesalonike 4:13-18, anasema: “Kwa makusudi ya matumizi ya kila siku, fundisho la hali iliyobarikiwa ya kutokufa ya wenye haki inachukua, kwa ajili yetu, nafasi ya fundisho lo lote lenye mashaka la ujio wa pili wa Bwana. Wakati wa kufa kwetu Bwana anakuja kutuchukua. Hilo ndilo tunalopaswa kulingojea na kukesha kwa ajili yake. Waliokufa tayari wameshaingia katika utukufu. Hawasubiri tarumbeta kwa ajili ya hukumu na kubarikiwa.”PKSw 418.4

    Lakini muda mfupi kabla ya kuwaacha wanafunzi Wake, Yesu hakuwaambia kuwa wangekwenda Kwake mara moja.” Naenda kuwaandalia mahali,” Yesu alisema. “Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu” (Yohana 14:2, 3). Na Paulo anatueleza, kwa kina zaidi, kuwa “Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele.” Na anaongeza: “Farijianeni kwa maneno hayo” (1 Wathesalonike 4:16-18). Tofauti kubwa iliyoje kati ya maneno haya ya faraja na maneno ya mchungaji anayeamini kuwa wokovu ni kwa wote bila kujali hali zao za kiroho ambaye maneno yake yalinukuliwa katika kurasa zilizotangulia! Huyu wa pili aliwafariji marafiki zake waliofiwa kwa kuwapa uhakika kuwa, hata kama aliyekufa angekuwa mwenye dhambi nyingi kiasi gani, alipotoa pumzi yake ya mwisho ya maisha angepokelewa na kuishi miongoni mwa malaika. Paulo anawaelekeza ndugu zake mbele kwa wakati ujao wa ujio wa Bwana wakati vifungo vya kaburi vitakapovunjwa, na “waliokufa katika Kristo” watakapofufuliwa ili waishi milele.PKSw 418.5

    Kabla mtu ye yote hajaingia katika majumba ya waliobarikiwa, kesi zao lazima zipelelezwe, na tabia zao na matendo yao lazima yapitishwe mbele ya Mungu kwa ajili ya uchunguzi. Wote ni lazima wahukumiwe kulingana na mambo yaliyoandikwa katika vitabu na wapewe malipo sawasawa na kazi zao zilivyokuwa. Hukumu hii haifanyiki wakati wa kufa. Zingatia maneno ya Paulo: “Kwa maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu” (Matendo 17:31). Hapa mtume alisema wazi wazi kuwa muda mahsusi, wakati ule ukiwa ni wa baadaye, ulikuwa umepangwa kwa ajili ya hukumu ya ulimwengu.PKSw 419.1

    Yuda anazungumzia wakati huo huo: “Na malaika wasioilinda enzi yao wenyewe, lakini wakayaacha makao yao yaliyowahusu, amewaweka katika vifungo vya milele chini ya giza kwa hukumu ya siku ile kuu.” Na, tena, Yuda ananukuu maneno ya Henoko: “Angalia, Bwana alikuja na watakatifu wake, maelfu maelfu, ili afanye hukumu juu ya watu wote” (Yuda 6, 14, 15). Yohana anatangaza kuwa aliwaona “wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; ... na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu” (Ufunuo 20:12).PKSw 419.2

    Lakini waliokufa tayari wanafurahia raha ya mbinguni au wanahangaika katika ndimi za moto wa jehanamu, hukumu ya wakati ujao ni ya nini tena? Mafundisho ya neno la Mungu kuhusu vipengele hivi muhimu ni ya wazi na wala hayapingani; yanaweza kueleweka kwa akili za kawaida. Lakini ni akili gani iliyo makini inaweza kuona ama hekima au haki katika nadharia iliyopo sasa? Je, wenye haki, baada ya upelelezi wa kesi zao wakati wa hukumu yao, watapokea maneno ya pongezi, “Vema, mtumwa mwema na mwaminifu: ... ingia katika furaha ya Bwana wako,” wakati watakuwa wameishi mbele Yake, pengine kwa zama nyingi? Je, waovu wanaitwa kutoka mahali pa maumivu yao motoni wapokee hukumu kutoka kwa Jaji Mkuu wa dunia yote: “Ondokeni kwangu, ninyi mliolaaniwa, nendeni katika moto wa milele”? (Mathayo 25:21, 41). Aha, dhihaka kubwa! Ukosoaji wa aibu wa hekima na haki ya Mungu!PKSw 419.3

    Nadharia ya hali ya kutokufa kwa roho ilikuwa moja ya mafundisho ya uongo ya Roma, yaliyotoka katika upagani. Martin Lutha aliweka fundisho hili miongoni mwa “hekaya za kutisha zilizokuwa sehemu ya rundo la barua zenye mamlaka ya kipapa.”—E. Petavel, The Problem of Immortality, ukurasa 255. Akitoa ufafanuzi wa maneno ya Sulemani katika Mhubiri, wafu hawajui neno lolote, Mwanamatengenezo anasema: “Mahali pengine panapothibitisha kuwa wafu hawana... hisia. Anasema, kule hakuna wajibu, hakuna sayansi, hakuna maarifa, hakuna hekima. Sulemani anatoa hitimisho kuwa waliokufa wamelala usingizi, na hawana hisia zozote. Kwa kuwa wafu wamelala pale, bila kuhesabu siku wala miaka, lakini watakapoamshwa, wataonekana kama wamelala muda usiozidi hata dakika moja.”—Martin Luther, Exposition of Solomon’s Booke Called Ecclesiastes, ukurasa 152. Kabla haijakatika kamba ya fedha; Au kuvunjwa bakuli la dhahabu; Au mtungi kuvunjika kisimani; Au gurudumu kuvunjika birikani;PKSw 420.1

    Hakuna mahali popote katika Maandiko ambapo tunapata kauli kuwa wenye haki wanakwenda mahali pa zawadi yao au kuwa waovu wanakwenda mahali pa adhabu yao wakati wa kufa. Wazee na manabii hawakuacha uhakika wa aina hiyo. Kristo na mitume Wake hawakutoa dokezo lolote kuhusiana na hilo. Biblia inafundisha wazi kuwa wafu hawaendi mara moja mbinguni. Wanaoneshwa kuwa wamelala usingizi mpaka wakati wa ufufuo (1 (Wathesalonike 4:14; Ayubu 14:10-12). Siku ile kamba ya fedha inapokatika na bakuli la dhahabu kuvunjwa (Mhubiri 12:6), mawazo ya mtu hupotea. Wanaokwenda chini kaburini wapo katika ukimya. Hawajui jambo lolote linalotendeka chini ya jua (Ayubu 14:21). Pumziko lenye baraka kwa wenye haki waliochoka! Wakati, uwe mrefu au mfupi, ni kufumba na kufumbua tu kwao. Wanalala usingizi; wataamshwa na tarumbeta ya Mungu ili wapokee hali ya kutokufa yenye utukufu. “Maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa. Basi huu uharibikao utakapovaa kutokuharibika, na huu wa kufa utakapovaa kutokufa, hapo ndipo litakapokuwa lile neno lililoandikwa, Mauti imemezwa kwa kushinda” (1 Wakorintho 15:52-54). Wanapoamshwa kutoka katika usingizi wao mzito wanaanza kufikiri kuanzia pale walipoishia. Hisia ya mwisho ilikuwa ya maumivu ya kifo; wazo la mwisho, kuwa walikuwa wakianguka chini ya nguvu ya kaburi. Wanapoamka kutoka kaburini, wazo la furaha la kwanza litasikika kama mwangi wa kelele za ushindi: “Ku wapi, Ewe mauti, kushinda kwako? U wapi, Ewe mauti, uchungu wako?” (Aya ya 55). PKSw 420.2

    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents