Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Pambano Kuu - Contents
  • Results
  • Related
  • Featured
No results found for: "".
  • Weighted Relevancy
  • Content Sequence
  • Relevancy
  • Earliest First
  • Latest First
    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents

    Sura ya 32—Mitego ya Shetani

    Pambano kuu kati ya Kristo na Shetani, ambalo limekuwa likipiganwa kwa takribani miaka elfu sita, linakaribia kufungwa; na Shetani anaongeza juhudi mara mbili kuishinda kazi ya Kristo kwa niaba ya mwanadamu na kushikilia roho katika mitego yake. Kuwashikilia watu gizani na katika hali ya kutotubu hadi upatanisho wa Mwokozi uishe, na kusiwepo tena kafara kwa ajili ya dhambi, ndiyo lengo analotafuta kulifikia.PKSw 396.1

    Kunapokuwa hakuna juhudi maalumu zinazofanywa kupinga mamlaka yake, kutojali kunaposhamiri katika makanisa na katika ulimwengu, Shetani hana wasiwasi; kwa kuwa hayuko katika hatari ya kupoteza wale ambao anawashikilia mateka kama apendavyo. Tahadhari inapotolewa ili kujali mambo ya umilele, na roho zinapouliza, “Nifanye nini nipate kuokoka?” anakaa chonjo, akitafuta kupambana dhidi ya nguvu ya Kristo na kupinga mvuto wa Roho Mtakatifu.PKSw 396.2

    Maandiko yanaeleza kuwa wakati mmoja, malaika wa Mungu walipokuja kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye alikuja miongoni mwao (Ayubu 1:6), siyo kusujudu mbele ya Mfalme wa Milele, bali kutafuta fursa ya kutimiza mipango yake mibaya dhidi ya wenye haki. Kwa lengo hilo hilo, anakuwepo katikati ya watu wanapokusanyika kumwabudu Mungu. Ingawa anajificha asionekane kwa macho, anafanya kazi kwa bidii zake zote kutawala akili za watu wanaokuja kuabudu. Kama jenerali mwenye ujuzi anapanga mipango yake mapema. Anapoona mjumbe wa Mungu akichunguza Maandiko, analiona somo litakalohubiriwa kwa watu. Ndipo anatumia hila zake zote na akili zake zote kwa kutawala mazingira ili ujumbe usiwafikie wale ambao anawadanganya kuhusiana na kipengele hicho kinachoandaliwa. Yule ambaye anahitaji sana onyo hilo anaingizwa katika miamala ya shughuli zingine zinazohitaji uwepo wake, au kwa njia nyingine atazuiwa asisikie maneno ambayo yangekuwa chumvi ya uzima kwa ajili ya uzima.PKSw 396.3

    Kwa mara nyingine tena, Shetani anawaona watumishi wa Bwana wakiwa na mzigo kwa sababu ya giza la kiroho linalowafunika watu. Anasikia maombi ya dhati kwa ajili ya neema na nguvu ya Kiungu ivunje laana ya kutojali, uzembe, na uvivu. Ndipo kwa juhudi mpya anatumia werevu wake. Anawajaribu watu waendekeze uchu wa chakula au aina nyingine ya anasa, na kwa njia hiyo anatia ganzi fahamu zao washindwe kusikiliza mambo ambayo walihitaji sana kuyasikia.PKSw 396.4

    Pamoja na hayo, Shetani anajua sana kuwa wale ambao anaweza kuwaongoza wapuuze maombi na wasijali kuchunguza Maandiko, wataangushwa na mashambulizi yake. Hivyo anatengeneza kila nyenzo inayowezekana kufunga kila akili. Kumekuwepo daima kundi la watu wanaodai kuwa wataua, ambao, badala ya kufuatilia ili kuujua ukweli, hufanya dini yao kuwa utafutaji makosa katika tabia au dosari katika imani ya wale wasiokubaliana nao. Watu hao ni wasaidizi wa mkono wa kulia wa Shetani. Washitaki wa ndugu sio wachache, na daima wanajishughulisha Mungu anapokuwa kazini na watumishi Wake wanapomwabudu Mungu kwa kicho cha kweli. Wataweka rangi ya uongo katika maneno na matendo ya wale wanaoipenda na kuitii kweli. Watawakilisha watumishi wa Kristo wenye moyo wa dhati wenye bidii, wanaojikana nafsi kama watu waliodanganywa au wadanganyaji. Ni kazi yao kuwakilisha vibaya nia ya kila tendo la kweli na zuri, kueneza maneno yasiyothibitishwa, na kuchochea mashaka katika akili za watu wasiokuwa na uzoefu. Katika kila njia inayoweza kufikiriwa watatafuta kusababisha kile ambacho ni safi na cha haki kichukuliwe kama kibaya na cha uongo.PKSw 396.5

    Lakini hakuna anayepaswa kudanganywa kuhusiana na watu hao. Inaweza kujulikana kuwa wao ni watoto wa nani, ni mfano wa nani wanafuata, na wanafanya kazi ya nani. “Mtawatambua kwa matunda yao” (Mathayo 7:16). Kazi yao inafanana na ile ya Shetani, mzushi mwenye sumu, “mshitaki wa ndugu zetu” (Ufunuo 12:10).PKSw 397.1

    Mdanganyaji mkuu ana mawakala wengi walio tayari kuwasilisha kila aina ya kosa ili kunasa roho—uongo ulioandaliwa kufaa kwa kila mazingira na uwezo wa wale ambao anataka kuwaangamiza. Ni mpango wake kuleta kanisani watu wasio na moyo wa dhati, wasioumbwa upya, watakaochochea mashaka na kutokuamini, na kuwa kikwazo kwa wale wote wanaotamani kuiona kazi ya Mungu ikisonga mbele na wao kusonga mbele pamoja nayo. Wengi wasiokuwa na imani ya kweli kwa Mungu au kwa neno Lake wanakubaliana na baadhi ya kanuni za ukweli na wanapitishwa kama Wakristo, na hivyo wanawezeshwa kuingiza makosa yao kama mafundisho ya Maandiko.PKSw 397.2

    Msimamo kuwa haidhuru watu wanaamini kitu gani ni moja ya imani za uongo za Shetani ambazo zinampa mafanikio makubwa sana. Anajua kuwa ukweli, ukipokelewa kwa kuupenda, unaitakasa roho ya mpokeaji; hivyo, anatafuta daima kuweka nadharia potovu, hadithi za uongo, injili nyingine badala ya ukweli wa neno la Mungu. Tangu mwanzo, watumishi wa Mungu wameshindana na walimu wa uongo, siyo tu kama watu wakatili, bali kama wapandikizaji wa mafundisho ya uongo yaliyokuwa hatari kwa uhai wa roho. Eliya, Yeremia, Paulo, kwa uthabiti na bila woga waliwapinga wale waliokuwa wakiwageuza watu waliache neno la Mungu. Ule uhuru unaochukulia imani sahihi ya kidini kuwa sio muhimu haukupata kibali cha hawa watetezi watakatifu wa ukweli.PKSw 397.3

    Tafsiri za Maandiko zisizo dhahiri na za kufikirika, na nadharia nyingi zinazopingana kuhusu imani za dini, zinazopatikana katika ulimwengu wa Kikristo ni kazi za adui yetu mkuu kuchanganya akili ili watu wasitambue ukweli. Na misuguano na migawanyiko iliyomo miongoni mwa makanisa ya Kikristo inasababishwa kwa kiwango kikubwa na desturi zilizopo za kutumia vibaya Maandiko kuunga mkono nadharia zinazopendwa. Badala ya kujifunza kwa uangalifu neno la Mungu kwa unyenyekevu wa moyo ili kujua mapenzi Yake, wengi wanatafuta kugundua kitu kisichokuwa cha kawaida au kipya.PKSw 398.1

    Ili kuhalalisha mafundisho yao yenye makosa na mtendo yao yasiyokuwa ya kikristo, baadhi wanachukua aya za Maandiko zikiwa zimetengwa na muktadha, pengine wakinukuu nusu ya aya moja kuthibitisha hoja yao, wakati sehemu iliyobaki ingeonesha maana iliyo kinyume kabisa. Kwa werevu wa nyoka, wanajibanza nyuma ya kauli zisizokuwa na uhusiano, zilizobuniwa kukidhi tamaa zao za kimwili. Kwa njia hiyo, watu wengi kwa uchaguzi wao wanapotosha neno la Mungu. Wengine, wanaofikiria sana juu ya mambo ya kuwazika tu, yasiyo halisi, wanachukua misemo na mifano ya Maandiko Matakatifu, wanaitafsiri kuhalalisha ubunifu wao, huku wakijali kidogo sana kanuni kuwa ushuhuda wa Maandiko hujitafsiri wenyewe, na ndipo huwasilisha mawazo yao yasiyo na msingi kama mafundisho ya Biblia.PKSw 398.2

    Wakati wowote, kujifunza Maandiko kunapofanyika bila roho ya maombi, unyenyekevu, na kufundishika, aya za wazi na rahisi kabisa pamoja na zile ngumu kabisa zitaeleweka tofauti na maana yake ya kweli. Viongozi wa upapa wanachagua sehemu za Maandiko zinazokidhi vizuri zaidi kusudi lao, wanazitafsiri wanavyopenda wenyewe, na ndipo huwasilisha tafsiri hizi kwa watu, huku wakiwanyima fursa ya kujifunza Biblia na kuelewa ukweli mtakatifu wao wenyewe. Biblia nzima inapaswa kutolewa kwa watu kama inavyosomeka. Ingekuwa bora zaidi kwao wasipate kabisa mafundisho ya Biblia kuliko kupata mafundisho ya Maandiko yaliyowakilishwa vibaya kwa kiwango hicho.PKSw 398.3

    Biblia ilikusudiwa iwe mwongozo kwa wale wote wanaopenda kuyajua mapenzi ya Muumbaji wao. Mungu aliwapa wanadamu neno la kweli la unabii; malaika na hata Kristo Mwenyewe walikuja kumfahamisha Danieli na Yohana mambo ambayo hayana budi kuja upesi. Yale mambo muhimu yanayohusu wokovu wetu hayakuachwa sirini. Hayakufunuliwa katika namna ambayo inamtatanisha na kumpoteza mtafutaji wa dhati wa ukweli. Bwana alisema kupitia kwa nabii Habakuki: “Bwana akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi ..., ili aisomaye apate kuisoma kama maji” (Habakuki 2:2). Neno la Mungu liko wazi kwa wote wanaolisoma kwa moyo wa maombi. Kila mtu aliye mwaminifu na wa kweli atapokea nuru ya ukweli. “Nuru imemzukia mwenye haki” (Zaburi 97:11). Na hakuna kanisa linaweza kukua katika utakatifu isipokuwa washiriki wake wanautafuta ukweli kwa dhati kama kutafuta hazina iliyositirika.PKSw 398.4

    Kwa makelele ya “Uhuru”, watu wanapofushwa wasione mbinu za adui yao, wakati yeye anafanya kazi wakati wote bila kuchoka afanikishe lengo lake. Baada ya kufanikiwa kuondoa Biblia na badala yake akaingiza fikra za kibinadamu, sheria ya Mungu imewekwa pembeni, na makanisa yako chini ya utumwa wa dhambi wakati wanadai kuwa wako huru.PKSw 399.1

    Kwa wengi, utafiti wa kisayansi umekuwa laana. Mungu ameruhusu mafuriko ya nuru yamwagwe ulimwenguni kwa njia ya ugunduzi wa sayansi na sanaa; lakini hata watu wenye uwezo mkubwa wa akili, wasipoongozwa na neno la Mungu katika utafiti wao, wanachanganyikiwa katika jitihada zao za kuchunguza mahusiano ya sayansi na ufunuo.PKSw 399.2

    Ujuzi wa mwanadamu wa mambo ya kimwili na ya kiroho ni mdogo na siyo kamili; matokeo yake wengi hawawezi kupatanisha mawazo yao ya sayansi na kauli za Maandiko. Wengi wanapokea nadharia na mambo ya kufikirika yasiyo halisi kama ukweli wa kisayansi, na wanafikiri kuwa neno la Mungu linapaswa kupimwa kwa mafundisho ya “elimu iitwayo elimu kwa uongo” (1 Timotheo 6:20). Muumbaji na kazi Zake vipo nje ya ufahamu wao; na kwa kuwa hawawezi kueleza mambo haya kwa sheria za asili, historia ya Biblia inachukuliwa kama taarifa isiyoweza kutumainiwa. Wanaotilia mashaka ukweli wa kumbukumbu za Agano la Kale na Agano Jipya mara nyingi wanaenda hatua nyingine mbele na wanatilia mashaka uwepo wa Mungu na wanadai kuwa vitu vya asili vina nguvu isiyo na mipaka. Wakiwa wameachia nanga yao, wanaachwa wagonge miamba ya ukafiri.PKSw 399.3

    Kwa njia hiyo wengi wanajikwaa katika imani na wanadanganywa na Ibilisi. Wanadamu wanajaribu kuwa na hekima zaidi kuliko Muumba wao; falsafa ya kibinadamu imejaribu kuchunguza na kueleza siri ambazo hazitafunuliwa kamwe milele zote. Ikiwa wanadamu wangeridhika kuchunguza na kuelewa yale ambayo Mungu ameyafunua juu Yake Mwenyewe na makusudi Yake, wangeona mandhari ya utukufu, nguvu, na mamlaka ya Yehova kiasi kwamba wangegundua udogo wao na wangeridhishwa na yale ambayo yamefunuliwa kwa ajili yao na kwa ajili ya watoto wao.PKSw 399.4

    Ni udanganyifu wa Shetani unaofanywa kwa ustadi wa hali ya juu kuwafanya watu watumie sana akili zao kuchunguza na kujaribu kueleza yale ambayo Mungu hajayafunua na ambayo Mungu hakusudii yaeleweke. Ilikuwa kwa sababu hiyo Lusifa alipoteza nafasi yake mbinguni. Alitokea kutoridhika kwa sababu siri zote za makusudi ya Mungu hazikufunuliwa kwake, na alijikuta akipuuza yale ambayo yalikuwa yemefunuliwa kuhusiana na kazi yake katika cheo chake cha juu alichokuwa amepewa. Kwa kuchochea hali ya kutoridhika huko katika mioyo ya malaika waliokuwa chini ya uongozi wake, alisababisha anguko lao. Sasa anatafuta kujaza roho ile ile katika akili za watu ili na wao wapuuze amri za Mungu zinazoeleweka moja kwa moja.PKSw 399.5

    Watu ambao hawapendi kupokea ukweli wa Biblia ulio wazi, unaochoma daima wanatafuta hadithi zinazofurahisha ili kunyamazisha dhamiri zao. Kwa kadiri mafundisho yanayotolewa yasivyokuwa ya kiroho sana, yasivyodai kujikana nafsi, na yasivyodai kujinyenyekesha, ndivyo yanavyopendwa na watu zaidi na yanavyopokelewa kwa wepesi zaidi. Watu hawa wanashusha uwezo wao wa kiakili ili kutimiza tamaa zao za mwili. Wakiwa na hekima nyingi katika kiburi chao kiasi cha kufikia hatua ya kuacha kuchunguza Maandiko kwa unyenyekevu wa moyo na maombi ya dhati ili wapate uongozi wa Kimungu, hawana ngao ya kuwakinga dhidi ya udanganyifu. Shetani yuko tayari kukidhi shauku ya moyo, na anagawa uongo wake badala ya ukweli. Hivyo ndivyo upapa ulivyopata mamlaka yake juu ya akili za watu; na kwa kuukataa ukweli kwa sababu unahusisha msalaba, Waprotestanti wanafuata njia ile ile. Wote wanaopuuza neno la Mungu ili wajifunze njia nyepesi na sera, ili wasiwe tofauti na watu wa ulimwengu, wataachwa wapokee uongo wa kutisha badala ya ukweli wa kidini. Kila aina ya uongo itapokelewa na watu ambao kwa kuchagua wao wenyewe wanaukataa ukweli wa neno la Mungu. Mtu anayetazama kwa hofu uongo wa aina moja atapokea uongo wa aina nyingine kwa urahisi. Mtume Paulo, akizungumzia juu ya tabaka la watu ambao “hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa,” anasema: “Kwa hiyo Mungu awaletea nguvu ya upotevu, wauamini uongo; ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu” (2 Wathesalonike 2:10-12). Kwa onyo hili lililoko mbele yetu, inatupasa tuwe makini kuhusiana na fundisho tunalolipokea.PKSw 400.1

    Miongoni mwa mawakala wanaofanikiwa sana wa mdanganyaji mkuu ni mafundisho na maajabu yanayodanganya ya imani ya kuwasiliana na watu waliokufa. Akijigeuza na kuwa kama malaika wa nuru, Shetani anatandaza wavu wake mahali asipotarajiwa sana. Ikiwa watu wangejifunza Kitabu cha Mungu kwa maombi ya dhati wangeweza kulijua hili, wasingeachwa gizani na wasingepokea mafundisho ya uongo. Lakini kwa kuwa wameukataa ukweli wanajikuta wakiwa mawindo ya udanganyifu.PKSw 400.2

    Uongo mwingine wa hatari ni fundisho linalokana na uungu wa Kristo, likidai kuwa hajawahi kuwepo hata kidogo kabla ya ujio Wake duniani. Nadharia hii inapokelewa kwa furaha na tabaka kubwa la watu wanaodai kuiamini Biblia; lakini inapingana na kauli za wazi kabisa za Mwokozi wetu juu ya uhusiano Wake na Baba, tabia Yake ya Kiungu, na uwepo Wake kabla ya ujio Wake duniani. Fundisho hili haliwezi kutetewa bila kupotosha Maandiko. Siyo tu kuwa linashusha uelewa wa mwanadamu wa kazi ya ukombozi, lakini pia linafanya watu wasiiamini Biblia ipasavyo kama ufunuo kutoka kwa Mungu. Wakati kutokuiamini Biblia kunalifanya fundisho la kuukana uungu wa Yesu liwe la hatari zaidi, kunalifanya pia lisiweze kupingwa kwa urahisi. Watu wakikataa ushuhuda wa Maandiko yaliyovuviwa kuhusu uungu wa Kristo, ni kazi bure kubishana nao juu ya mada hii; kwa sababu hakuna hoja, hata kama ina nguvu kiasi gani, inayoweza kuwashawishi. “Mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni” (1 Wakorintho 2:14). Hakuna mtu ye yote yule ambaye anashikilia kosa hili anayeweza kuwa na uelewa wa kweli wa tabia au utume wa Kristo, au wa mpango mkuu wa ukombozi wa mwanadamu.PKSw 400.3

    Na bado kuna kosa jingine lenye hila na ubaya mwingi linaloenea haraka, imani kuwa Shetani hayupo na siyo kiumbe mwenye nafsi; kuwa jina la Shetani linatumika tu kumaanisha mawazo na tamaa mbaya za watu.PKSw 401.1

    Fundisho linalohubiriwa mahali pengi kutoka katika mimbari maarufu, kuwa ujio wa pili wa Kristo ni ujio Wake kwa kila mtu wakati wa kifo chake, ni zana ya kuhamisha akili za watu zisifikirie ujio Wake binafsi katika mawingu ya mbinguni. Kwa miaka mingi, Shetani amekuwa akisema, “Tazama, yumo katika vyumba vya siri” (Mathayo 24:23-26); na roho nyingi zimepotea kwa kuukubali uongo huu.PKSw 401.2

    Tena, kuna hekima ya kidunia inayofundisha kuwa maombi sio muhimu. Wanasayasi wanadai kuwa hakuna jibu halisi kwa maombi; kwamba hili lingekuwa kukiuka sheria, muujiza, na kuwa miujiza haipo. Sayari zote, wanasema, zinatawaliwa na sheria zisizobadilika, na Mungu Mwenyewe hafanyi cho chote kinyume na sheria hizi. Hivyo wanamwakilisha Mungu kuwa anabanwa na sheria Zake Mwenyewe—kana kwamba utendaji wa sheria za Kimungu ungeweza kuondoa uhuru wa Kiungu. Fundisho hilo linapingana na ushuhuda wa Maandiko. Je, miujiza haikufanywa na Kristo na mitume Wake? Mwokozi Yule yule mwenye huruma yuko hai leo, na yuko tayari kusikia maombi ya imani kama alivyofanya alipoonekana kwa macho akitembea miongoni mwa watu. Vitu vya asili vinashirikiana na vitu vilivyo juu ya vitu vya asili. Ni sehemu ya mpango wa Mungu kutupatia, kama jibu kwa ombi la imani, kile ambacho asingetupatia ikiwa tusingemwomba.PKSw 401.3

    Kuna idadi kubwa ya mafundisho yenye makosa na mawazo ya kufikirika yanayozidi kushamiri miongoni mwa makanisa ya ulimwengu wa Kikristo. Ni vigumu kukadiria matokeo mabaya ya kuondoa moja ya viwango vilivyowekwa na neno la Mungu. Ni watu wachache wanaodiriki kufanya hivyo wanaoachia kukataa fundisho moja tu la ukweli. Walio wengi huendelea kuweka pembeni kanuni moja ya ukweli baada ya nyingine, hadi wanafikia kuwa makafiri kamili.PKSw 402.1

    Makosa katika teolojia inayokubaliwa na wengi yamesababisha watu wengi kuwa na mashaka ambapo kama isingekuwa kwa sababu hiyo wangeyaamini Maandiko. Ni vigumu kwa mtu kukubali mafundisho ambayo hukiuka maadili ya haki, rehema, na ukarimu; na kwa kuwa mambo haya huwakilishwa kama mafundisho ya Biblia, mtu anakataa kuyapokea kama neno la Mungu.PKSw 402.2

    Na hili ndilo lengo ambalo Shetani anatafuta kulitimiza. Hakuna jambo jingine analolitamani zaidi kuliko kuua imani kwa Mungu na kwa neno Lake. Shetani ni kiongozi mkuu wa jeshi kubwa la watu wenye mashaka, na anafanya kazi kwa nguvu zake zote kuwadanganya watu na kuwaleta upande wake. Kuwa na mashaka kumekuwa mtindo wa maisha. Kuna tabaka kubwa la watu ambao kwao neno la Mungu linatazamwa kwa mashaka kwa sababu ile ile kama ilivyokuwa kwa Mwasisi wake—kwa sababu linakemea na kuhukumu dhambi. Wale ambao hawako tayari kutii matakwa yake wanajaribu kushinda mamlaka yake. Wanasoma Biblia, au wanasikiliza mafundisho yake yanapowasilishwa kutoka katika dawati takatifu, kwa kusudi tu la kutafuta makosa katika Maandiko au katika hubiri. Siyo watu wachache wakuwa makafiri ili kuhalalisha au kupata udhuru wa kukimbia wajibu wao. Wengine wanashika kanuni za kutoamini kwa sababu ya kiburi na uvivu. Wanapenda raha, ili wajitambulishe kwa kufanya jambo lolote la kuwaletea heshima, ambalo linahitaji juhudi na kujikana nafsi, wanadhamiria kujipatia umaarufu kwa kukosoa Biblia wakifikiri kuwa kwa kufanya hivyo wataonekana ni wenye hekima. Kuna mengi ambayo akili yenye mipaka, ambayo haijaangaziwa kwa hekima ya Kiungu, haina uwezo wa kuyaelewa; na hivyo wanapata kisingizio cha kukosoa. Kuna wengi ambao huonekana kufikiri kuwa ni sifa njema kusimama upande wa kutokuamini, mashaka, na ukafiri. Lakini chini ya mwonekano wa uwazi wao itagundulika kuwa watu kama hao wanachochewa na kujiamini na kiburi. Wengi wanafurahia kupata jambo fulani katika Maandiko la kutatanisha akili za wengine. Baadhi mwanzoni wanakosoa na kutoa hoja upande usio sahihi, kwa sababu tu wanapenda ubishi. Hawatambui kuwa kwa njia hiyo wanajinasisha wenyewe katika mtego wa mwindaji. Lakini baada ya kueleza wazi kutokuamini kwao, wanahisi wanapaswa kutetea msimamo wao. Hivyo wanaungana na wasiomcha Mungu na kujifungia wenyewe malango ya Paradiso.PKSw 402.3

    Mungu ametoa katika neno Lake ushahidi wa kutosha wa tabia yake ya Kiungu. Ukweli mkuu ambao unahusu ukombozi wetu umewasilishwa kwa uwazi. Kwa msaada wa Roho Mtakatifu, ambao umeahidiwa kwa wale wote wanaoutafuta kwa dhati, kila mtu anaweza kuelewa ukweli huu yeye mwenyewe. Mungu amewapa watu msingi imara ambao juu yake wanaweza kusimika imani yao.PKSw 403.1

    Lakini akili za watu zenye kikomo haziwezi kuelewa kikamilifu mipango na makusudi ya Yeye Asiye na Kikomo. Hatuwezi kamwe kumwona Mungu kwa kuchunguza. Hatupaswi kujaribu kutumia mikono yetu yenye kiburi kufungua pazia ambalo nyuma yake ameficha ukuu Wake. Mtume anapiga kelele kwa mshangao: “Hukumu zake hazichunguziki, wala njia zake hazitafutikani!” (Warumi 11:33). Tunaweza tu kuelewa jinsi anavyoshughulika na sisi, na nia inayomsukuma kufanya hivyo, ili tuweze kutambua upendo usio na mipaka na rehema zilizoshikamana na nguvu isiyokuwa na mipaka. Baba yetu aliyeko mbinguni anapanga kila jambo kwa hekima na haki, na hatupaswi kutoridhishwa na kutokuwa na imani Naye, bali tumsujudie na tujisalimishe Kwake kwa kicho. Atatufunulia makusudi Yake mengi ambayo ni kwa ajili ya ustawi wetu tukiyajua, na zaidi ya hayo inatupasa kuutumainia Mkono ambao una nguvu zisizo na mpaka, Moyo uliojaa upendo.PKSw 403.2

    Wakati Mungu ametoa ushahidi wa kutosha kwa ajili ya imani yetu, kamwe hataondoa visingizio vyote ya kutokuamini. Watu wote wanaotafuta ndoana za kuning'iniza mashaka yao watazipata. Na wale wanaokataa kukubali na kutii neno la Mungu mpaka kila kikwazo kimeondolewa, na kusiwe kabisa na fursa ya kuwa na mashaka, hawatakuja nuruni.PKSw 403.3

    Kutokumwamini Mungu ni tunda la asili ya moyo usioumbwa upya, moyo ulio na uadui na Mungu. Lakini imani inavuviwa na Roho Mtakatifu, na itastawi ikipaliliwa. Hakuna mtu anayeweza kuwa na imani bila juhudi za makusudi. Kukosa imani kunakuzwa kwa kuchochewa na kuhimizwa; na ikiwa watu, badala ya kutafakari juu ya ushahidi uliotolewa na Mungu kujenga imani yao, wanajielekeza katika kuhoji na kulaumu, wataona mashaka yao yakiendelea kuwa makubwa zaidi.PKSw 403.4

    Lakini wale wanaotilia mashaka ahadi za Mungu na wanakosa imani katika hakika ya neema Yake wanamkosea Mungu heshima; na mvuto wao, badala ya kuwavuta wengine kwa Kristo, unakuwa na mwelekeo wa kuwasukumia mbali Naye. Wao ni miti isiyozaa matunda, inayoeneza matawi yake meusi mbali na katika maeneo mengi, ikizuia mwanga wa jua usiifikie mimea mingine, na kuifanya isinyae na kufa chini ya kivuli chenye baridi. Kazi ya maisha ya watu hawa huonekana kama ushuhuda wa kudumu dhidi yao. Wanapanda mbegu za mashaka na kutoamini ambazo zitatoa mavuno hatimaye.PKSw 403.5

    Kuna njia moja tu ya kufuata kwa wale wanaotamani kwa dhati kuondokana na mashaka. Badala ya kuhoji na kulalamikia yale wasiyoyaelewa, hebu wao wapokee nuru ambayo tayari inawaangazia, na watapokea nuru kubwa zaidi. Hebu wao watimize wajibu wao uliowekwa wazi kwa ufahamu wao, nao watawezeshwa kuelewa na kutekeleza yale ambayo kwa sasa wanayatilia mashaka.PKSw 404.1

    Shetani anaweza kuwasilisha kitu bandia kinachofanana sana na ukweli kiasi cha kuwadanganya watu walio tayari kudanganywa, wanaotamani kukwepa kujikana na kujitoa kafara kunakotakiwa na ukweli wa neno la Mungu; lakini haiwezekani kwake kumshikilia chini ya mamlaka yake mtu ambaye anatamani kwa uaminifu, na kwa gharama yo yote, kuujua ukweli. Kristo ni kweli na ni “Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu” (Yohana 1:9). Roho wa kweli ametumwa kuwaongoza watu katika ukweli wote. Na kwa mamlaka ya Mwana wa Mungu imetangazwa: “Tafuteni, nanyi mtaona.” “Mtu akipenda kuyatenda mapenzi yake, atajua habari ya yale mafunzo” (Mathayo 7:7; Yohana 7:17).PKSw 404.2

    Wafuasi wa Kristo wanajua kidogo sana kuhusu njama ambazo Shetani na majeshi yake wanazipanga dhidi yao. Lakini Yeye aketiye mbinguni juu atazigeuza njama hizi kutekeleza mipango Yake ya kina. Bwana huruhusu watu Wake wapitishwe katika tanuru la moto wa majaribu, siyo kwa sababu anafurahia maudhi na mateso yao, lakini kwa sababu mchakato huu ni muhimu kwa ajili ya ushindi wao. Mungu asingeweza, daima kwa utukufu Wake Mwenyewe, kuwakinga dhidi ya majaribu; kwa kuwa kusudi la msingi la majaribu ni kuwaandaa kupinga vishawishi vyote vya uovu.PKSw 404.3

    Sio watu wabaya wala mashetani wanaoweza kuzuia kazi ya Mungu, au kufungia uwepo Wake dhidi ya watu Wake, ikiwa watakuwa watiifu, wenye mioyo iliyopondeka, waliotubu na kuachana na dhambi zao, na kwa imani wanadai ahadi Zake. Kila jaribu, kila nguvu ya upinzani, ikiwa ya wazi au ya siri, inaweza kupingwa kwa mafanikio, “Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi” (Zekaria 4:6).PKSw 404.4

    “Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake husikiliza maombi yao;.... Naye ni nani atakayewadhuru, mkiwa wenye juhudi katika mema?” (1 Petro 3:12, 13). Balaamu aliposhawishiwa kwa ahadi ya zawadi, alifanya uchawi dhidi ya Israeli, na kwa kumtolea Bwana kafara alitaka kutamka laana juu ya watu Wake, Roho wa Mungu alikataa uovu aliotamani kuutamka, na Balaamu alilazimishwa kusema: “Nimlaanije, yeye ambaye Mungu hakumlaani? Nimshutumuje, yeye ambaye Bwana hakumshutumu?““Na nife kifo chake mwenye haki, Na mwisho wangu uwe mfano wa mwisho wake!” Baada ya kafara kutolewa tena, nabii asiyemcha Mungu alitangaza: “Tazama, nimepewa amri kubariki, Yeye amebariki, nami siwezi kulitangua. Hakutazama uovu katika Yakobo, Wala hakuona ukaidi katika Israeli. Bwana, Mungu wake, yu pamoja naye, Na sauti kuu ya mfalme i katikati yao.” “Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo, Wala hapana uganga juu ya Israeli. Sasa habari za Yakobo na Israeli zitasemwa, Ni mambo gani aliyoyatenda Mungu!” Pamoja na hizo madhabahu zilizojengwa kwa mara ya tatu, na kwa mara nyingine tena Balaamu alijaribu kutamka laana. Lakini kutoka katika midomo isiyopenda, Roho wa Mungu alitangaza mafanikio ya wateule Wake, na alikemea upumbavu na ubaya wa maadui zao: “Na abarikiwe kila akubarikiye, Na alaaniwe kila akulaaniye” (Hesabu 23:8, 10, 20, 21, 23; 24:9).PKSw 404.5

    Watu wa Israeli walikuwa watiifu kwa Mungu kwa wakati huu; na kwa kadiri walivyodumu kuitii sheria Yake, hakuna nguvu duniani au kuzimuni ambayo ingeweza kuwashinda. Lakini laana ya Balaamu aliyokatazwa kuitamka dhidi ya watu wa Mungu, hatimaye alifaulu kuileta juu yao kwa kuwashawishi na kuwafanya watende dhambi. Walipokiuka amri za Mungu, walijitenga Naye, nao waliachwa wakutane na nguvu ya mwangamizaji.PKSw 405.1

    Shetani anajua vizuri kuwa roho dhaifu kabisa kuliko zote inayokaa ndani ya Kristo ina nguvu nyingi zaidi kuliko majeshi yote ya giza, na kuwa, kama angejifunua wazi wazi, angekabiliwa na kushindwa. Hivyo anajitahidi kuwavuta askari wa msalaba watoke katika ngome yao imara, wakati yeye pamoja na majeshi yake wakiwavizia, wakiwa tayari kuwaangamiza wale wote wanaokwenda katika eneo lake. Kumtegemea Mungu kwa moyo mnyenyekevu, na kumtii Mungu kikamilifu ndiyo njia pekee ya usalama wetu.PKSw 405.2

    Hakuna mtu ambaye yuko salama kwa siku moja au saa moja bila maombi. Muhimu kuliko yote, inatupasa kumlilia Bwana kwa ajili ya hekima ya kulielewa neno Lake. Humo zimefunuliwa hila za mjaribu na njia ambazo kwazo anaweza kupingwa kwa ufanisi. Shetani ni mjuzi wa kudondoa Maandiko, akiweka tafsiri yake ya mafungu, ambayo kwayo anatumaini kuwa anaweza kutukwaza. Inatupasa kujifunza Biblia kwa unyenyekevu wa moyo, bila kusahau hitaji letu la kumtegemea Mungu. Wakati ambapo inatupasa daima kuwa macho dhidi ya mbinu za Shetani, inatupasa kuomba daima: “Usitutie majaribuni.”PKSw 405.3

    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents