Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Pambano Kuu - Contents
  • Results
  • Related
  • Featured
No results found for: "".
  • Weighted Relevancy
  • Content Sequence
  • Relevancy
  • Earliest First
  • Latest First
    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents

    Sura ya 11—Upinzani wa Wakuu wa Majimbo

    Moja ya shuhuda za kujivunia zilizowahi kutolewa kuunga mkono Matengenezo ulikuwa upinzani uliotolewa na viongozi Wakristo wa Ujerumani katika Baraza la Spires la mwaka 1529. Ujasiri, imani, na uimara wa wale watu wa Mungu ulileta uhuru wa mawazo na dhamiri kwa vizazi vilivyofuata. Upinzani wao ndio ulioliletea kanisa la matengenezo jina la Protestanti; kanuni zake ndizo “msingi halisi wa Uprotestanti.”— D'Aubigne, b. 13, ch. 6.PKSw 147.1

    Siku ya giza na ya kutisha ilikuwa imefika kwa Matengenezo. Licha ya Hukumu ya Worms, ikimtangaza Luther kuwa haramia na ikipiga marufuku kufundisha au kuamini mafundisho yake, uvumilivu wa kidini hadi wakati huo uliendelea kuwepo katika dola. Uongozi wa Mungu ulikuwa umedhibiti nguvu zilizopinga ukweli. Charles V alikuwa amejielekeza kukomesha Matengenezo, lakini mara nyingi alipoinua mkono wake kupiga alilazimishwa kugeuzia pigo pembeni. Tena na tena mara nyingi, mauaji yasiyoepukika ya watu waliothubutu kupinga Roma yalikuwa karibu kutekelezwa; lakini wakati mfupi kabla ya utekelezaji majeshi ya Uturuki yalitokea kwenye mpaka wa mashariki, au mfalme wa Ufaransa, au hata papa mwenyewe, kwa sababu ya wivu wa ukuu uliokuwa ukiongezeka wa mfalme, walifanya vita dhidi yake; na hivyo, katikati ya migogoro na vurugu za mataifa, Matengenezo yaliachwa kuimarika na kupanuka.PKSw 147.2

    Hatimaye, hata hivyo, mamlaka za upapa zilimaliza migogoro yao, ili wawe na mwelekeo mmoja dhidi ya Wanamatengenezo. Baraza Kuu lililokaa Spires katika mwaka 1526 lilitoa kwa kila jimbo uhuru kamili katika masuala ya kidini mpaka mkutano wa Baraza Kuu; lakini mara tu baada ya hatari zilizosababisha kupewa uhuru huo kupita, mfalme aliitisha Baraza la pili katika mji wa Spires mwaka 1529 kwa kusudi la kukomesha uzushi. Wakuu wa majimbo walipaswa kushawishiwa, ikiwezekana kwa njia ya amani, waungane dhidi ya Matengenezo; lakini ikiwa mbinu hizi zingeshindwa, Charles alijiandaa kutumia upanga.PKSw 147.3

    Wafuasi wa upapa walifurahi sana. Walikuja mjini Spires kwa idadi kubwa, na walionesha chuki yao wazi wazi kwa Wanamatengenezo na wote waliowaunga mkono. Alisema Melanchthon: “Sisi ni karaha na takataka za ulimwengu; lakini Kristo atawaangalia watu Wake wanyenyekevu, na atawatunza.”—Ibid., b. 13, ch. 5. Wakuu wa majimbo waliokuwa wafuasi wa injili waliohudhuria katika Baraza walikatazwa kuruhusu injili kuhubiriwa hata katika makazi yao binafsi. Lakini watu wa Spires walikuwa na kiu kwa ajili ya neno la Mungu, na, licha ya kupigwa marufuku injili, maelfu walifurika kwenye huduma zilizoendeshwa katika kanisa la elekta wa Saxony.PKSw 147.4

    Hili liliharakisha hali ya hatari. Ujumbe wa kifalme ulitangaza kwa Baraza kwamba kwa kuwa azimio lililotoa uhuru wa dhamiri lilikuwa limesababisha uasi mkuu, mfalme aliagiza lifutwe. Amri hii isiyokuwa na mantiki iliamsha hasira na hali ya tahadhari kwa Wakristo waaminio injili. Mmoja alisema: “Kristo ameangukia tena katika mikono ya Kayafa na Pilato.” Wafuasi wa Roma walianza tena kufanya fujo. Mfuasi wa papa mwenye msimamo mkali alisema: “Waturuki ni bora zaidi kuliko Walutheri; kwa kuwa Waturuki wanaadhimisha siku za funga, na Walutheri wanazivunja. Ikiwa inatupasa kuchagua kati ya Maandiko Matakatifu na makosa ya zamani ya kanisa, inatupasa kuacha Maandiko Matakatifu.” Melanchthon alisema: “Kila siku, katika mkutano uliojaa watu, Faber alikuwa anarusha jiwe jipya kwa wafuasi wa injili.”—Ibid., b. 13, ch. 5.PKSw 148.1

    Uvumilivu wa kidini ulipitishwa kisheria, na majimbo yaliyoamini injili yaliazimia kupinga ukiukaji wa haki zao. Luther, akiwa bado chini ya katazo lililowekwa na Amri ya Worms, alikuwa haruhusiwi kuwepo Spires; lakini nafasi yake ilikuwa imejazwa na watendakazi wenzake na wakuu ambao Mungu alikuwa amewainua kutetea kazi Yake nyakati za \ dharura hii. Mheshimiwa Frederick wa Saxony, mtetezi wa zamani wa Luther, kifo kilikuwa kimemuondoa; lakini John, Mwana wa Mfalme, kaka na mrithi wake, aliyakaribisha Matengenezo kwa furaha, na wakati akiwa rafiki wa amani, alionesha nguvu na ujasiri mwingi katika mambo yote yaliyohusiana na maslahi ya imani.PKSw 148.2

    Makasisi walidai kuwa majimbo yaliyokuwa yamekubali Matengenezo yajisalimishe kwa utawala wa Roma kimya kimya. Wanamatengenezo, kwa upande mwingine, walidai uhuru ambao ulikuwa umetolewa awali. Wasingeweza kukubali Roma iyalete chini ya utawala wake yale majimbo ambayo kwa furaha kubwa yalikuwa yamelipokea neno la Mungu.PKSw 148.3

    Kama njia ya kupata mwafaka, hatimaye ilipendekezwa kuwa mahali ambapo Matengenezo hayakuwa yamepokelewa, Hukumu ya Worms itekelezwe kikamilifu; na kuwa “katika yale majimbo ambapo watu walikuwa wameikiuka, na mahali ambapo wasingeweza kuifuata bila hatari ya uasi, walitakiwa angalau wasiingize matengenezo mapya, wasiguse vipengele vinavyobishaniwa, wasipinge sherehe za misa, wasiruhusu Mromani Katoliki ajiunge na UlutheriLuther.”—Ibid., b. 13, ch. 5. Uamuzi huu ulipitishwa na Baraza Kuu, na makasisi na maaskofu wa upapa waliridhika sana.PKSw 148.4

    Ikiwa amri hii ingetekelezwa, “Matengenezo yasingeenea ... mahali ambapo yalikuwa bado hayajulikani, wala yasingejengwa juu ya misingi imara ... mahali yalipokuwepo.”—Ibid., b. 13, ch. 5. Uhuru wa kusema ungeharimishwa. Waongofu wapya wasingeruhusiwa. Na marafiki wa Matengenezo walitakiwa kujisalimisha kwa masharti na makatazo haya mara moja. Matumaini ya ulimwengu yalionekana kana kwamba yamezimwa. “Uhuishaji wa utawala wa Roma ... ungerudisha bila shaka maovu ya zamani;” na fursa ingepatikana kirahisi kwa ajili ya “kukamilisha uangamizaji wa kazi ambayo tayari ilikuwa imeshayumbishwa sana” na hali ya kuwa na itikadi kali na migawanyiko.—Ibid., b. 13, ch. 5.PKSw 148.5

    Wakati kundi la wafuasi wa injili walipokutana ili kushauriana, kila mmoja alimwangalia mwenzake katika hali ya kuduwaa kabisa. Kutoka kwa mmoja hadi kwa mwingine swali hili lilipita: “Ni jambo gani lifanyike?” Masuala mazito yanayohusu ulimwengu yalikuwa hatarini. “Je, viongozi wa Matengenezo wajisalimishe, na wakubaliane na hukumu? Ni rahisi kiasi gani Wanamatengenezo wangeweza wakati huu wa hatari, ambayo kwa kweli ilikuwa kubwa, kujenga hoja ya kuwapeleka katika njia potovu! Visingizio vilivyoeleweka vingapi na sababu zilizokubalika ngapi ambazo wangeweza kuzitoa ili wasijisalimishe! Viongozi wa Kilutheri walipewa uhakikisho wa uhuru wa kufuata dini yao. Upendeleo huo huo walipewa pia watu wote waliokuwa chini ya utawala wao ambao, kabla ya kupitishwa uamuzi huo, walikuwa wameamini mitazamo ya kimatengenezo. Je, jambo hili isingepasa liwaridhishe? Ni hatari ngapi wangeziepuka kwa kujisalimisha! Ni hatari ngapi na migogoro mingapi ambayo upinzani wao ungewasababishia! Nani ajuaye fursa ambazo wangezipata baadaye? Hebu tuikumbatie amani; hebu tutafute tawi la mzeituni lililoinuliwa na Roma, na tufunike majeraha ya Ujerumani. Kwa hoja kama hizi, Wanamatengenezo wangeweza kufuata njia ambayo kwa hakika ingeweza, kwa muda mfupi, kuangamiza kazi yao ya matengenezo.PKSw 149.1

    “Kwa furaha waliiangalia kanuni ambayo ilikuwa msingi wa mwafaka, na walitenda kwa imani. Kanuni hiyo ilikuwa ipi? Ilikuwa haki ya Roma kulazimisha na kudhibiti dhamiri na kupiga marufuku maswali huria. Lakini, Je, haikuwa haki yao wenyewe na raia zao Waprotestanti kuwa na uhuru wa kidini? Ndiyo, uhuru ulikuwepo, lakini, kama upendeleo uliowekwa katika mwafaka, na siyo kama haki yao. Lakini kwa wengine wote nje ya mwafaka, kanuni kuu ya mamlaka ilikuwa kutawala; dhamiri kutojaliwa; Roma ilikuwa jaji asiyekosea, na lazima itiiwe. Kukubaliana na mwafaka uliopendekezwa kungemaanisha kuwa uhuru wa kidini ubaki katika mji wa Saxony tu; mahali ambapo matengenezo yalikuwa yamekubaliwa na watu walio wengi; na kwa ulimwengu wa Kikristo uliosalia, kujifunza na kujiunga na imani ya matengenezo ilikuwa ni uhalifu, na ilikuwa lazima uhalifu huo adhibitiwe kwa kutupwa gerezani au kutundikwa juu ya mti wenye ncha kali. Je, waridhie kuufanya uhuru wa dhamiri kuwa haki ya watu eneo moja tu? Yaani, itangazwe kuwa Imani ya Matengenezo imepata mwongofu wa mwisho? Kwamba imepata eka yake ya mwisho ya utawala? Na kwamba mahali popote Roma ilipokuwa imeweka mizizi yake kwa wakati ule, utawala wake ubaki hivyo milele zote? Je, Wanamatengenezo wangeweza kujitetea kuwa hawana hatia ya damu ya wale mamia kwa maelfu ambao, kwa utekelezaji wa mwafaka huo, ingewapasa kupoteza maisha yao katika nchi za upapa? Hii ingekuwa kusaliti, katika saa ile muhimu, kazi ya injili na uhuru wa ulimwengu wa Kikristo.”—Wylie, b. 9, ch. 15. Ingekuwa heri kwao “kutoa kafara kila kitu, hata majimbo yao, miji yao, taji zao, na maisha yao.”—D'Aubigne, b. 13, ch. 5.PKSw 149.2

    “Tukatae amri hii,” walisema wakuu wa majimbo. “Katika masuala ya dhamiri kanuni ya wengi wape haina nguvu.” Manaibu walisema: “Ni amri ya mwaka 1526 ambayo imewezesha kuwepo kwa amani katika himaya: kuiondoa amri hiyo kungeijaza Ujerumani kwa misuguano na migawanyiko. Mahakama haina mamlaka ya kufanya kitu cho chote zaidi ya kutunza uhuru wa dini mpaka Baraza Kuu likutane.”—Ibid., b. 13, ch. 5. Kulinda uhuru wa dhamiri ni wajibu wa dola, na huu ndiyo mpaka wake katika masuala ya dini. Kila serikali yo yote ya kidunia inayojaribu kutunga au kutekeleza sheria za kidini kwa kutumia mamlaka za kiraia inavunja kanuni ambayo Wakristo wainjilisti wameipambania kwa gharama kubwa.PKSw 150.1

    Wafuasi wa papa waliazimia kuangusha kile walichokiita “ukaidi usio na hofu.” Walianza kwa kusababisha migawanyiko miongoni mwa watu waliounga mkono Matengenezo na kuwatisha wote ambao walikuwa bado hawajatangaza hadharani kuunga mkono Matengenezo. Wawakilishi wa miji huru hatimaye waliitwa mbele ya Baraza Kuu na walitakiwa kutangaza ikiwa walikuwa tayari kukubaliana na mapendekezo ya mwafaka. Waliomba wapewe muda, lakini hawakupewa muda. Walipojaribiwa, karibu nusu yao walichagua kuwa upande wa Wanamatengenezo. Waliokataa kukiuka uhuru wa dhamiri na haki ya uamuzi wa mtu binafsi walijua hakika kuwa msimamo wao ungewafanya wakosolewe, walaumiwe, na wateswe. Mjumbe mmoja alisema: “Inatupasa ama tulikane neno la Mungu, au—tuchomwe moto.”— Ibid., b. 13, ch. 5.PKSw 150.2

    Mfalme Ferdinand, mwakilishi wa mfalme mkuu kwenye Baraza Kuu, aliona kuwa amri hiyo ingesababisha migawanyiko mikubwa ikiwa wakuu wa majimbo hawatashawishiwa kuikubali na kuisimamia. Kwa hiyo alijaribu sanaa ya ushawishi, waikijua vema kuwa kutumia nguvu kwa watu wale kungewafanya wazidi kusimamia uamuzi wao. Ferdinand “ aliwaomba wakuu waikubali amri, akiwathibitishia kuwa mfalme mkuu angewafurahia sana.” Lakini watu hawa waaminifu walikiri mamlaka iliyokuwa juu ya watawala wa kidunia, na walijibu kwa utulivu: “Tutamtii mfalme mkuu katika kila jambo linaloweza kuchangia katika kudumisha amani na heshima ya Mungu.”— Ibid., b. 13, ch. 5.PKSw 150.3

    Mbele ya Baraza Kuu mfalme alitangaza hatimaye kwa elekta na marafiki zake kuwa amri “ilikuwa inakwenda kuandikwa katika muundo wa tamko la kifalme,” na kwamba “njia pekee iliyobaki kwao ilikuwa kujisalimisha kwa walio wengi.” Baada ya kusema hayo, aliondoka na kuuacha mkutano, bila kuwapa Wanamatengenezo fursa ya kujadili au kujibu. “Hata hivyo walituma wajumbe kwenda kumsihi mfalme arudi.” Jibu lake kwa malalamiko yao lilikuwa:“Ni jambo lililokwisha kuamriwa; kujisalimisha ndiyo tu kumebaki.”— Ibid., b. 13, ch. 5.PKSw 151.1

    Kikosi cha mfalme kilishawishika kuwa viongozi wakuu wa Kikristo walikuwa wameshaazimia kuyaweka Maandiko Matakatifu juu ya mafundisho na matakwa ya kibinadamu; na walijua kuwa mahali popote ilipokubalika hivyo, upapa hatimaye ulishindwa. Lakini, kama ilivyokuwa kwa maelfu ya watu tangu wakati wao, walioangalia “mambo yanayoonekana,” walijidanganya kuwa upande wa mfalme na papa ulikuwa na nguvu, na kuwa upande wa Wanamatengenezo ulikuwa dhaifu. Ikiwa Wanamatengenezo wangetegemea msaada wa kibinadamu peke yake, wangekuwa dhaifu kama wafuasi wa papa walivyodhania. Lakini ingawa walikuwa wachache katika idadi, na hawakupatana na Roma, walikuwa na chanzo cha nguvu zao. Walipata nguvu “ambayo haikutokana na taarifa ya Mahakama, bali iliyotokana na neno la Mungu, siyo iliyotoka kwa mfalme mkuu Charles, bali iliyotoka kwa Yesu Kristo, Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana.”— Ibid., b. 13, ch. 6.PKSw 151.2

    Mfalme Ferdinand alipokataa kuheshimu imani na dhamiri zao, wakuu wa majimbo ya Kikristo waliamua wasijali kutokuwepo kwake, bali walete Upinzani wao kwenye baraza la taifa bila kuchelewa. Hivyo basi, tamko rasmi, liliandaliwa na kuwasilishwa kwa Baraza:PKSw 151.3

    “Tunapinga kwa hati hii, mbele ya Mungu, Muumbaji wetu pekee, Mtunzaji, Mkombozi, na Mwokozi, na ambaye siku moja atakuwa Mhukumu wetu, hali kadhalika mbele ya watu wote na viumbe wote, kwamba sisi, kwa ajili yetu na kwa ajii ya watu, hatuikubali wala kuitii kwa namna yo yote ile amri iliyopendekezwa, na jambo lolote lile ambalo ni kinyume na Mungu, na neno Lake takatifu, na haki yetu ya dhamiri, na wokovu wa roho zetu.”PKSw 151.4

    “Nini! Tunathibitisha amri hii! Tunasema kuwa Mwenyezi Mungu anapomwita mtu ashiriki ujuzi Wake, hata hivyo, mtu huyu hawezi kupokea ujuzi wa Mungu!” “Hakuna fundisho la hakika isipokuwa lile ambalo linapatana na neno la Mungu.... Mungu anakataza.... Maandiko Matakatifu yanapaswa kuelezwa kwa kutumia aya zingine na zinazoeleweka kwa uwazi zaidi; ... Kitabu hiki Kitakatifu, miongoni mwa mambo muhimu kwa ajili ya Mkristo, ni rahisi kueleweka, na kimekusudiwa kusambaratisha giza. Tumedhamiria, kwa neema ya Mungu, kudumisha usafi na kuhubiri neno Lake pekee, kama lilivyo katika vitabu vya kibiblia vya Agano la Kale na Agano Jipya, bila kuongeza kitu chochote humo ambacho ni kinyume chake. Neno hili ndiyo ukweli pekee; ni kanuni ya hakika ya mafundisho yote na maisha yote, na hawezi kamwe kutuangusha au kutudanganya. Anayejenga juu ya msingi huu atasimama dhidi ya nguvu zote za kuzimu, wakati majivuno yote ya kibinadamu yanapopangwa dhidi ya neno la Mungu yataanguka mbele ya uso wa Mungu.”PKSw 151.5

    “Kwa sababu hiyo tunakataa nira iliyowekwa juu yetu.” “Wakati huo huo tunatarajia kuwa mfalme mkuu atatutendea kama kiongozi Mkristo anayempenda Mungu zaidi kuliko kitu kingine chochote; na tunawaahidi kuwapa, yeye pamoja na ninyi waheshimiwa wenye neema, upendo na utii wetu wote ambao ni haki na wajibu wetu halali.”—Ibid., b. 13, ch. 6.PKSw 152.1

    Mguso wa kushangaza ulihisika kwenye Baraza Kuu. Wengi wao walipatwa na mshangao na tahadhari kwa sababu ya ujasiri wa wapinzani. Mustakabali wao ulionekana kuwa wenye dhoruba na usio na uhakika. Migawanyiko, migogoro, na umwagaji damu vilionekana kutoepukika. Lakini Wanamatengenezo, baada ya kuhakikishiwa haki ya msimamo wao, na kuutegemea mkono wa Yeye Mwenye nguvu zote, walikuwa “wamejaa ujasiri na uthabiti.”PKSw 152.2

    “Kanuni zilizomo katika Upinzani huu unaosherehekewa ... ndiyo maudhui hasa ya Uprotestanti. Sasa Upinzani huu hupinga dhuluma mbili dhidi ya mwanadamu katika masuala ya imani: dhuluma ya kwanza ni uingiliaji wa mahakama za kiraia, na dhuluma ya pili ni mamlaka ya kiimla ya kanisa. Badala ya dhuluma hizi, Uprotestanti huweka nguvu ya dhamiri juu kuliko hakimu, na mamlaka ya neno la Mungu juu kuliko kanisa linaloonekana. Katika nafasi ya kwanza, inakataa mamlaka ya kiraia katika mambo ya Kimungu, na husema na manabii na mitume, ‘Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.’ Mbele ya mfalme mkuu Charles wa Tano, unaiinua taji ya Yesu Kristo. Lakini unaenda mbele zaidi ya hapo: unaweka kanuni kuwa mafundisho yote ya kibinadamu yanapaswa kuwa chini ya udhibiti wa neno la Mungu.”—Ibid., b. 13, ch. 6. Wapinzani walikuwa wamethibitisha haki yao ya kusema kwa uhuru waliyoyaamini kuhusu ukweli. Siyo tu kuwa wangeamini na kutii, bali pia wangefundisha kile ambacho neno la Mungu linasema, na walipinga haki ya kasisi au hakimu kuingilia. Upinzani wa Spires ulikuwa ushuhuda mkubwa dhidi ya kukosa uvumilivu wa kidini, na dai la haki za binadamu wote kumwabudu Mungu kulingana na matakwa ya dhamiri zao wenyewe.PKSw 152.3

    Tayari tangazo lilikuwa limetolewa. Lilikuwa limeandikwa katika kumbukumbu za maelfu ya watu na lilikuwa limeandikwa katika vitabu vya mbinguni, mahali ambapo juhudi za mwanadamu zisingeweza kulifuta. Ujerumani yote iliyokuwa imeipokea injili ilipokea tamko la Uprotestanti kama tamko lao la imani. Kila mahali watu waliona tamko hili kama ahadi ya enzi bora zaidi. Mmoja wa wakuu aliwaambia Waprotestanti wa Spires: “Mwenyezi Mungu, ambaye amewapa neema ya kukiri kwa nguvu, kwa uhuru, na bila hofu, awatunze katika uimara wa Kikristo mpaka siku ya umilele.”—Ibid., b. 13, ch. 6.PKSw 152.4

    Kama Matengenezo, baada ya kupata kiasi fulani cha mafanikio, ungekubali kupitisha muda ili wapendwe na ulimwengu, ungekosa uaminifu kwa Mungu na kwa matengenezo yenyewe, na ungejihakikishia kifo chake yenyewe. Uzoefu wa hawa waheshimiwa Wanamatengenezo ni somo kwa ajili ya zama zote zilizofuata. Namna ya Shetani ya kufanya kazi dhidi ya Mungu na neno Lake haijabadilika; bado yuko kinyume na Maandiko kufanywa mwongozo wa maisha kama ilivyokuwa katika karne ya kumi na sita. Katika wakati wetu kuna kuacha sana mafundisho na kanuni za Maandiko kuna hitaji la kurudi kwenye kanuni kuu za Uprotestanti—Biblia, na Biblia pekee, kama kanuni ya imani na wajibu. Shetani bado anafanya kazi kwa kila njia anayoweza kuitumia kuharibu uhuru wa dhamiri. Nguvu ya upinzani dhidi ya Ukristo ambayo waprotestanti wa Spires waliikataa, sasa kwa nguvu mpya inatafuta kurudisha utawala iliyoupoteza. Utii imara kwa neno la Mungu sawa na ule uliooneshwa wakati wa migogoro ya Matengenezo ndiyo tumaini pekee la matengenezo leo.PKSw 153.1

    Kulitokea ishara za hatari kwa Waprotestanti; kulikuwepo ishara, pia, kuwa mkono wa Mungu ulikuwa umenyoshwa kuwalinda waaminifu. Ilikuwa ni wakati huu “Melanchthon alipompitisha katika mitaa ya Spires kuelekea Rhine rafiki yake Simon Grynaeus, akimshurutisha avuke mto. Grynaeus alishangaa sana kwa tukio hilo. ‘Mtu mmoja mzee sana, lakini ambaye sikumjua,’ alisema Melanchthon, ‘alitokea mbele yangu na kusema, Ndani ya dakika mbili, maofisa watatumwa na Ferdinand kumkamata Grynaeus.’”PKSw 153.2

    Wakati wa mchana, Grynaeus alikuwa amesemwa vibaya katika hubiri lililotolewa na Faber, daktari msomi mfuasi wa papa; na alipofunga hubiri alimshutumu Grynaeus kwa kutetea “makosa fulani yanayochukiza.” “Faber alituliza hasira yake, lakini mara moja alikwenda kwa mfalme, ambapo alipata amri dhidi ya profesa msumbufu wa Heidelberg. Melanchthon hakuwa na shaka kuwa Mungu alimwokoa rafiki yake kwa kumtuma mmoja wa malaika Zake watakatifu kumwonya mapema dhidi ya hatari iliyomkabili rafiki yake.PKSw 153.3

    “Akiwa ametulia kwenye kingo za Mto Rhine, alisubiri mpaka maji ya mto yalipokuwa yamemwokoa Grynaeus dhidi ya watesaji. ‘Hatimaye,’ alipiga kelele Melanchthon, alipomwona upande wa pili wa mto, ‘hatimaye ametenganishwa na taya katili za watu walio na kiu ya damu isiyo na hatia.’ Aliporudi nyumbani kwake, Melanchthon alipewa taarifa kuwa maofisa waliokuwa wakimtafuta Grynaeus walikuwa wamepekua kila mahali kwenye nyumba yake toka juu hadi chini.”—Ibid., b. 13, ch. 6.PKSw 153.4

    Ilikuwa sasa matengenezo yaletwe mbele ya viongozi wakuu wa dunia. Viongozi wa uinjilisti walikuwa wamekataliwa fursa ya kusikilizwa na Mfalme Ferdinandi; lakini walikuwa wapewe fursa ya kuwasilisha hoja zao mbele ya mfalme mkuu na waheshimiwa waliokusanyika wa kanisa na dola. Katika mwaka uliofuata Upinzani wa Spires, ili kunyamazisha migawanyiko iliyosumbua dola, Charles V, aliitisha kikao cha Baraza Kuu katika mji wa Augsburg, ambapo alitangaza kusudi lake la kuongoza kikao hicho yeye mwenyewe binafsi. Pale viongozi wa Uprotestanti waliitwa.PKSw 154.1

    Hatari kubwa zilitishia Matengenezo; lakini watetezi wake walimtumaini Mungu awasaidie katika kazi yao, na waliahidi kuwa imara katika kuunga mkono injili. Elekta wa Saxony alisihiwa na wajumbe wake wa baraza asihudhurie lile Baraza Kuu. Walisema, Mfalme alihitajika awe pamoja na wakuu kwenye lile Baraza ili awaingize katika mtego. “Je, siyo hatari kabisa kwenda na kujifungia mwenyewe ndani ya kuta za jiji pamoja na adui mwenye nguvu?” Lakini wengine walieleza kwa uungwana, “Hebu wakuu wa majimbo tujiheshimu kwa ujasiri, na kazi ya Mungu itaokolewa.” “Mungu ni mwaminifu; Hatatutupa,” alisema Luther.—Ibid., b. 14, ch. 2. Elekta aliondoka, akiwa na msafara wake, kuelekea Augsburg. Wote walielewa hatari zilizomkabili, na wengi walienda huko wakiwa na nyuso zenye huzuni na mioyo iliyojaa mashaka. Lakini Luther, ambaye aliwafuata mpaka Coburg, alifufua imani yao iliyokuwa karibu kupotea kwa kuimba wimbo, ulioandikwa katika safari ile, “Mungu ni ngome yetu imara.” Hofu nyingi zilizoleta mashaka ziliondoka, mioyo mingi mizito iliburudishwa, kwa sauti ya wimbo unaovuvia.PKSw 154.2

    Wakuu waliopokea matengenezo waliazimia kuandika tamko la pamoja la maoni yao kwa mpangilio mzuri, likiwa na uthibitisho kutoka katika Maandiko, na kuliwasilisha kwa Baraza; na kazi ya uandishi wake alipewa Luther, Melanchthon, na wenzao. Ungamo hili lilikubaliwa na Waprotestanti kama ufafanuzi wa imani yao, na walikusanyika kuweka majina yao kwenye hati hii muhimu. Ulikuwa wakati muhimu lakini wa kujaribiwa sana. Wanamatengenezo walitamani kazi yao isiingiliwe na masuala ya kisiasa; walihisi kuwa Matengenezo hayakupaswa kutumia mvuto mwingine zaidi ya ule unaotoka katika neno la Mungu. Wakati wakuu wa Ukristo walipotaka kuendelea kutia sahihi Ungamo, Melanchthon aliingilia kati, na kusema: “Ni kazi ya wanateolojia na wachungaji kupendekeza mambo haya; hebu tuache mambo mengine mikononi mwa mamlaka za wakuu wa dunia.” “Haiwezekani, hata kidogo,” alijibu John wa Saxony, “kunitenga. Nimeazimia kufanya kilicho sahihi, wala sijali taji yangu. Shauku yangu ni kumkiri Bwana. Kofia yangu na vazi langu la uongozi wa jimbo havina thamani sana kwangu sawa na msalaba wa Yesu Kristo.” Baada ya kusema hayo, aliandika jina lake. Mwingine miongoni mwa wakuu wa majimbo alisema alipokuwa akishika kalamu: “Ikiwa heshima ya Bwana wangu Yesu Ktisto inahitaji jambo hili, niko tayari ... kuacha mali zangu na maisha yangu nyuma.” “Ni heri niache raia wangu na majimbo yangu, kuiacha nchi ya baba zangu, na fimbo ya mkononi,” aliendelea, “kuliko nipokee fundisho jingine tofauti na Ungamo hili.”—Ibid., b. 14, ch. 6. Hiyo ndiyo iliyokuwa imani na ujasiri wa watu wa Mungu.PKSw 154.3

    Wakati mwafaka ulifika wa kwenda mbele ya mfalme mkuu. Charles V, akiwa ameketi kwenye kiti cha enzi, akiwa amezungukwa na maelekta na wakuu, akiwasikiliza Wanamatengenezo wa Kiprotestanti. Ungamo la imani yao lilisomwa. Katika mkutano huo mkubwa kweli za injili ziliwekwa wazi, na makosa ya kanisa la papa yalianikwa wazi wazi. Ndiyo siku hiyo ilitangazwa “siku kuu zaidi kuliko zote za Matengenezo, na siku yenye utukufu mwingi zaidi kuliko zote katika historia ya Ukristo na wanadamu.”—Ibid., b. 14, ch. 7.PKSw 155.1

    Lakini miaka michache ilikuwa imepita tangu mtawa wa Wittenberg aliposimama peke yake katika jiji la Worms mbele ya baraza la kitaifa. Sasa mahali pake walisimama viongozi wenye heshima kubwa na nguvu nyingi katika ufalme. Luther alikataliwa kuja Augsburg, lakini alikuwepo kwa njia ya maneno na maombi yake. “Nina furaha sana,” aliandika, “kuishi hadi saa hii, ambapo Kristo ameinuliwa hadharani na waumini mashuhuri kama hao, na katika mkutano mkubwa kama huo.”—Ibid., b. 14, ch. 7. Kwa njia hiyo yakatimizwa Maandiko yanayosema: “Nitazinena shuhuda zako ... mbele ya wafalme” (Zaburi 119:46).PKSw 155.2

    Nyakati za Paulo injili ambayo kwayo alifungwa gerezani ilifikishwa hivyo hivyo mbele ya wakuu na waheshimiwa wa jiji la kifalme. Kwa hiyo katika tukio hili, yale ambayo mfalme alipiga marufuku yasihubiriwe mimbarani yalihubiriwa katika nyumba ya mfalme; yale ambayo yalifikiriwa kuwa yasingefaa kusikilizwa na watumishi yalisikilizwa kwa mshangao na mabwana na malodi wa himaya ya kifalme. Wafalme na watu mashuhuri walikuwa wasikilizaji, wana wa wafalme walikuwa wahubiri, na hubiri lilikuwa ukweli wa Mungu. “Tangu enzi za mitume,” anasema mwandishi, “hakujakuwepo kazi kubwa zaidi au ungamo kubwa zaidi kuliko hilo.”—D'Aubigne, b. 14, ch. 7.PKSw 155.3

    “Yote ambayo yamesemwa na Walutheri ni ya kweli; hatuwezi kuyakana,” alisema askofu wa kipapa. “Unaweza kweli kupata hoja nzuri za kukanusha ungamo lililofanywa na elekta na wenzake?” mwingine alimwuliza Dkt. Eck. “Kwa maandishi ya mitume na manabii—hapana!” lilikuwa jibu; “lakini kwa maandishi ya mababa na mabaraza—ndiyo!” “Ninaelewa,” alisema mwuliza swali. “Walutheri, kwa mujibu wa maelezo yako, wapo katika Maandiko, na sisi tuko nje.”—Ibid., b. 14, ch. 8.PKSw 155.4

    Baadhi ya wakuu wa majimbo wa Ujerumani waliongoka na kujiunga na imani ya matengenezo. Mfalme mkuu mwenyewe alitangaza kuwa mafundisho ya imani ya Kiprotestanti yalikuwa ya kweli. Tamko lilitafsiriwa katika lugha nyingi na kusambazwa katika nchi zote za Ulaya, na limekubaliwa na mamilioni ya watu katika vizazi vilivyofuata kama muhtasari wa imani yao.PKSw 156.1

    Watumishi wa Mungu waaminifu hawakufanya kazi peke yao. Wakati mamlaka na nguvu na roho wachafu katika anga walipoungana pamoja dhidi yao, Bwana hakuwaacha watu Wake. Kama macho yao yangefumbuliwa, wangeweza kuona ushahidi wa ajabu wa uwepo na msaada wa Mungu kama ule uliotolewa kwa nabii wa zamani. Wakati mtumishi wa Elisha alipomwonesha bwana wake jeshi la adui lililokuwa limewazunguka na kukataa kabisa fursa zote za kuponyoka, nabii aliomba: “Ee Bwana, nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona” (2 Wafalme 6:17). Na, kumbe, mlima ulikuwa umejaa magari na farasi za moto, jeshi la mbinguni lililokuwa limepangwa kumlinda mtu wa Mungu. Hivyo ndivyo malaika walivyowalinda watendakazi katika kazi ya Matengenezo.PKSw 156.2

    Moja ya kanuni zilizoshikiliwa sana na Luther ilikuwa kwamba kusiwepo na namna yo yote ya haja ya kuomba mamlaka ya kidunia iunge mkono Matengenezo, na kusiwepo na haja yo yote ya kuomba jeshi kulinda Matengenezo. Alifurahi kuwa injili ilipokelewa na wakuu wa himaya; lakini walipopendekeza kuungana ili kuunda umoja wa kujihami, alisema kuwa “fundisho la injili linapaswa kulindwa na Mungu pekee.... Kwa kadiri mwanadamu alivyoingilia katika kazi, ndivyo Mungu angejihusisha zaidi katika kuilinda. Tahadhari zote za kisiasa zilizopendekezwa, kwa maoni yake, zilitokana na hofu zisizo na msingi na mashaka yanayotokana na dhambi.”— D'Aubigne, London ed., b. 10, ch. 14.PKSw 156.3

    Wakati adui walipoungana ili kuangamiza imani ya matengenezo, na maelfu ya mapanga yalipoonekana kuwa yanakaribiwa kuvutwa kutoka katika ala zake dhidi ya matengenezo, Luther aliandika: “Shetani anaonesha ghadhabu yake; maaskofu waovu wanakula njama; na tunatishiwa vita. Himizeni watu kupambana kwa kishujaa mbele ya kiti cha enzi cha Bwana, kwa imani na maombi, ili kwamba maadui, kwa kunyamazishwa na Roho wa Mungu, watulizwe kwa amani. Hitaji letu kuu, kazi yetu kuu, ni maombi; hebu watu wajue kuwa wanakabiliwa na ncha ya upanga na ghadhabu ya Shetani, na hebu waombe.”—D'Aubigne, b. 10, ch. 14.PKSw 156.4

    Tena, tarehe nyingine ya baadaye, akizungumzia muungano uliokuwa ukifikiriwa na viongozi wa majimbo yaliyofanya matengenezo, Luther alisema kuwa silaha pekee iliyopaswa kutumiwa katika vita hii ilipaswa kuwa “upanga wa Roho.” Alimwandikia elekta wa Saxony: “Hatuwezi kwa dhamiri zetu kuidhinisha muungano uliopendekezwa. Ingekuwa bora tufe mara kumi kuliko kuiona injili yetu inasababisha tone moja la damu linamwagika. Sehemu yetu ni kuwa kama mwanakondoo aendaye machinjioni. Msalaba wa Kristo lazima ubebwe. Hebu mheshimiwa kiongozi usiogope. Tutafanya mengi zaidi kwa maombi yetu kuliko maadui zetu watakavyofanya kwa majivuno yao. Jambo muhimu pekee ni kuwa mikono yenu isiwe na madoa ya damu ya ndugu zenu. Ikiwa mfalme anahitaji kutupeleka katika mahakama zake, tuko tayari kwenda. Huwezi kuilinda imani yetu: kila mmoja anapaswa kuamini kwa kuwa tayari kuhatarisha maisha yake mwenyewe.”—Ibid., b. 14, ch. 1.PKSw 156.5

    Kutoka katika chumba cha siri cha maombi ndiko ilipotoka nguvu iliyoutetemesha ulimwengu katika Matengenezo Makuu. Pale, kwa utulivu mtakatifu, watumishi wa Bwana walisimika miguu yao juu ya mwamba wa ahadi Zake. Wakati wa mapambano pale Augsburg, Luther “hakupitisha siku bila kutumia angalau saa tatu katika maombi, na zilikuwa saa zilizochaguliwa kutoka miongoni mwa zile zilizofaa zaidi kwa ajili ya kujifunza.” Katika faragha ya chumba chake, alisikika akimimina roho yake mbele za Mungu katika maneno “yaliyojaa sifa, hofu, na tumaini, sawa na mtu aliyeongea na rafiki yake.” “Ninajua kuwa Wewe ni Baba yetu na Mungu wetu,” alisema, “na kwamba Wewe utawatawanya watesi wa watoto Wako; kwa kuwa Wewe Mwenyewe upo hatarini pamoja nasi. Jambo hili ni Lako, na ni kwa sababu ya msukumo Wako sisi tumeweka mikono yetu juu yake. Tutetee, basi, Ee Baba!”—Ibid., b. 14, ch. 6.PKSw 157.1

    Kwa Melanchthon, ambaye alikuwa amevunjika moyo kwa sababu ya mzigo wa wasiwasi na hofu, aliandika: “Neema na amani katika Kristo— ninasema, na siyo katika ulimwengu. Amina. Ninachukia kwa chuki kali sana kwa sababu ya hiyo hali yako ya wasiwasi inayokutafuna. Ikiwa kazi hii siyo ya haki, achana nayo; ikiwa kazi hii ni ya haki, kwa nini tusiziamini ahadi Zake Yeye Ambaye ametuamuru tusinzie bila hofu? ... Kristo hatatupungukia katika kazi ya haki na ukweli. Yu hai, Anatawala; ni hofu gani, tena, tunaweza kuwa nayo?”—Ibid., b. 14, ch. 6.PKSw 157.2

    Mungu alisikia vilio vya watumishi Wake. Aliwapa wakuu wa majimbo na wachungaji neema na ujasiri wa kusimama kwa ajili ya ukweli dhidi ya watawala wa giza la ulimwengu huu. Alisema Bwana: “Tazama, naweka katika Sayuni jiwe kuu la pembeni, teule, lenye heshima, Na kila amwaminiye hatatahayarika” (1 Petro 2:6). Wanamatengenezo Waprotestanti walijenga juu ya Kristo, na malango ya kuzimu yasingeweza kuwashinda.PKSw 157.3

    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents