Loading...
Larger font
Smaller font
Copy
Print
Contents
Pambano Kuu - Contents
  • Results
  • Related
  • Featured
No results found for: "".
  • Weighted Relevancy
  • Content Sequence
  • Relevancy
  • Earliest First
  • Latest First
    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents

    Sura ya 13—Uholanzi na Skandinavia

    Katika nchi ya Uholanzi, ukatili wa kipapa ulipata upinzani mkali tangu mapema kabisa. Miaka mia saba kabla ya wakati wa Luther, Kiongozi wa Kanisa la Roma alipingwa bila woga na maaskofu wawili, ambao, baada ya kutumwa Roma kwa kazi maalumu, waligundua tabia halisi ya “kiongozi mkuu wa kanisa”: Mungu “ameweka malkia na mwenzi Wake, kanisa, kuwa ruzuku ya kutosha na ya milele kwa ajili ya familia yake, na mahari isiyofifia wala isiyoharibika, na kumpatia taji na fimbo ya milele; ... vyote ambavyo hutenda kazi kama mtego wa mwizi. Unajiweka mwenyewe katika hekalu la Mungu; badala ya mchungaji, umekuwa mbwa mwitu kwa kondoo; ... unataka tukuamini kama askofu mkuu, lakini una tabia ya ukatili.... Wakati ulipaswa kuwa mtumishi wa watumishi, kama unavyojiita, unapambana kuwa bwana wa mabwana.... Unazidharau amri za Mungu.... Roho Mtakatifu ni mjenzi wa makanisa ulimwenguni kote.... Jiji la Mungu wetu, ambalo sisi ni raia wake, linapanuka na kuhusisha maeneo yote ya mbinguni; na ni kubwa zaidi kuliko jiji, ambalo manabii watakatifu waliliita Babeli, ambalo hujifanya kuwa la Kimungu, na hujitapa kuwa hekima yake ni ya milele; na hatimaye, ingawa bila sababu, kuwa jawahi kukosea, wala hawezi kukosea kamwe.”— Gerard Brandt, History of the Reformation in and About the Low Countries 1:6.PKSw 179.1

    Wengine waliinuka kutoka karne hadi karne wakitoa mwangwi wa upinzani huu. Na wale walimu wa awali ambao, walitembelea nchi tofauti tofauti na wakijulikana kwa majina mbalimbali, wakiwa na tabia ya wamishenari Wawaldensia, wakisambaza kila mahali ukweli wa injili, waliingia Uholanzi. Mafundisho yao yalienea haraka. Waliitafsiri Biblia ya Kiwaldensia katika lugha ya Kidachi. Walitangaza “kuwa Biblia ilikuwa na manufaa makubwa sana; haina mizaha, haina hadithi za kubuni, haina upuuzi, haina uongo, bali ina maneno ya kweli; na kwamba kweli hapa na pale kulikuwepo na mambo magumu kuyaelewa. Lakini iko hivyo ili uzuri na utamu wa yale mepesi na matakatifu ugunduliwe kirahisi.”—Ibid. 1:14. Hivyo ndivyo walivyoandika marafiki wa imani ya kale, katika karne ya kumi na mbili.PKSw 179.2

    Sasa ndipo yalipoanza mateso ya Kiroma; lakini katikati ya matita ya kuni na mateso waumini waliendelea kuongozeka, wakitangaza kwa ujasiri kuwa Biblia ndiyo mamlaka pekee isiyokosea katika dini, na kwamba “hakuna mtu anayepaswa kulazimishwa kuamini, bali anapaswa kuongolewa kwa kuhubiriwa.”—Martyn 2:87.PKSw 179.3

    Mafundisho ya Luther yalipata udongo wenye rutuba katika nchi ya Uholanzi, na watu wa kweli na waaminifu waliinuka kuihubiri injili. Kutoka moja ya majimbo ya Uholanzi alitokea Menno Simmons. Akiwa amesomeshwa na Kanisa Katoliki la Roma na kuwekwa wakfu wa upadrisho, alikuwa hajui chochote kuhusu Biblia, na hakuisoma kwa kuogopa kushawishika na kuwa mzushi. Wakati mashaka kuhusiana na fundisho kuwa mkate na mvinyo hubadilika kuwa mwili na damu halisi ya Yesu yalipomjia, aliyachukulia kama majaribu kutoka kwa Shetani, na kwa maombi na toba alipambana kuyashinda; lakini bila mafanikio. Kwa kujichanganya katika matukio ya starehe alijaribu kunyamazisha sauti ya dhamiri; lakini bila mafanikio. Baada ya muda alivutwa kujifunza Agano Jipya, na hili, pamoja na vitabu vya Luther vilimfanya aikubali imani ya matengenezo. Muda mfupi baada ya hapo alishuhudia katika kijiji jirani kukatwa kichwa cha mtu ambaye alikuwa ameuawa kwa kubatizwa mara ya pili. Jambo lililomfanya ajifunze Biblia kuhusiana na ubatizo wa watoto. Hakupata ushahidi wake katika Maandiko, lakini aliona toba na imani kila mahali kama sharti la kupokea ubatizo.PKSw 179.4

    Menno aliachana na Kanisa la Kiroma na kujitolea maisha yake kufundisha kweli alizozipokea. Katika nchi za Ujerumani na Uholanzi kikundi cha watu wenye itikadi kali kilijitokeza, wakihubiri mafundisho ya kipuuzi na uchochezi, wakivunja utaratibu na uzuri, na wakihamasisha fujo na kuchochea uasi dhidi ya serikali. Menno aliona matokeo mabaya ambayo kwa hakika hatimaye vuguvugu hili lilikuwa zlinaenda kusababisha na alichukua hatua madhubuti kupinga mafundisho potovu na mipango ya hila ya watu wenye itikadi kali. Walikuwepo watu wengi, hata hivyo, waliokuwa wamepotoshwa na wapotoshaji hawa, lakini walioacha mafundisho yao yasiyofaa; na walikuwepo bado waliosalia wengi wa Wakristo wa zamani, matunda ya mafundisho ya Wawaldensia. Menno alifanya kazi miongoni mwa makundi haya ya watu kwa bidii na mafanikio makubwa.PKSw 180.1

    Kwa miaka ishirini na tano alisafiri, akiwa na mkewe na watoto wao, akistahimili shida kubwa na kujinyima kwingi, na mara nyingi kwa kuhatarisha maisha yake. Alizunguka mara nyingi katika nchi ya Uholanzi na maeneo ya magharibi ya nchi ya Ujerumani, akifanya kazi zaidi miongoni mwa makundi ya watu wa chini lakini akiwa na mvuto mkubwa miongoni mwa watu wengi zaidi. Akiwa na uwezo wa asili wa kuongea kwa ufasaha, ingawa elimu yake ilikuwa ya wastani tu, alikuwa mtu mwenye uadilifu usioyumba, mwenye roho ya unyenyekevu na tabia ya upole, na mtu mkweli na mcha Mungu wa dhati, akionesha kwa mfano maishani mwake kanuni ambazo alizifundisha, na aliaminiwa na watu. Wafuasi wake walitawanywa na kuonewa. Waliumizwa zaidi kwa kushindwa na kikundi cha wenye itikadi kali cha Wamansteri. Hata hivyo watu wengi waliongolewa kutokana na kazi zake.PKSw 180.2

    Hakuna mahali ambapo mafundisho ya kimatengenezo yalipokelewa kwa furaha na watu wengi zaidi kuliko katika nchi ya Uholanzi. Ni katika nchi chache ambapo wafuasi wa matengenezo walistahimili mateso ya kutisha zaidi kuliko katika nchi ya Uholanzi. Katika nchi ya Ujerumani, Charles V alipiga marufuku Matengenezo, na alitamani kuwachoma moto wafuasi wote wa Matengenezo; lakini wakuu walikuwa kikwazo dhidi ya ukatili wake. Katika nchi ya Uholanzi, mfalme alikuwa na nguvu zaidi, na maagizo yake ya utesaji yalifuatana moja baada ya lingine kwa haraka haraka. Kusoma Biblia, kuisikiliza au kuihubiri, au hata kuizungumzia, ilikuwa ni kujitakia adhabu ya kifo cha kuchomwa moto. Kumwomba Mungu kwa siri, kukataa kuinamia sanamu, au kuimba zaburi, adhabu yake ilikuwa kifo. Hata wale ambao walikana makosa yao walihukumiwa, ikiwa walikuwa wanaume, kuuawa kwa upanga; ikiwa walikuwa wanawake, kuzikwa wakiwa hai. Maelfu ya watu yaliangamia chini ya utawala wa Charles na wa Philip II.PKSw 180.3

    Wakati mmoja familia nzima ililetwa mbele ya mahakama ya uchunguzi, wakishitakiwa kwa kutokuhudhuria misa na kuabudia nyumbani. Walipohojiwa kuhusu ibada zao za siri mtoto wao wa mwisho wa kiume alijibu: “Tunapiga magoti, na kuomba kuwa Mungu aangazie akili zetu na asamehe dhambi zetu; tunamwombea mfalme wetu, kwamba utawala wake ufanikiwe na maisha yake yawe ya furaha; tunawaombea mahakimu wetu, kwamba Mungu awalinde na awatunze.”—Wylie, b. 18, ch. 6. Baadhi ya majaji waliguswa sana, hata hivyo baba na mmoja wa watoto wake wa kiume walihukumiwa kuchomwa moto.PKSw 181.1

    Hasira ya watesaji ililingana na imani ya wafia dini. Siyo wanaume tu bali pia hata wanawake na mabinti dhaifu walionesha ujasiri usioyumba. “Wake walisimama pembeni mwa waume zao waliokuwa wakichomwa moto, na wakati wanaume walipokuwa wakiungua moto wake zao walinong'oneza maneno ya faraja, au kuwaimbia zaburi au kuwatia moyo.” “Mabinti walilala katika makaburi yao kana kwamba walikuwa wakiingia katika vyumba vyao vya kulala usiku; au walienda kwenye jukwaa la kunyongea na moto, wakiwa wamevaa nguo nzuri kabisa, kana kwamba walikuwa wanaenda kwenye harusi zao.”—Ibid., b. 18, ch. 6.PKSw 181.2

    Kama ilivyokuwa katika siku ambapo upagani ulipamba moto kuangamiza injili, damu ya Wakristo ilikuwa mbegu. (Tazama Tertullian, Apology, paragraph 50.) Mateso yalichochea ongezeko la idadi ya mashahidi kwa ajili ya ukweli. Mwaka baada ya mwaka mfalme, kwa kukasirishwa sana na msimamo usioyumba wa watu, aliongeza ukatili katika kazi yake ya utesaji; lakini bila mafanikio. Chini ya uongozi wa mheshimiwa William wa Orange Mapinguzi yalileta uhuru wa kuabudu katika nchi ya Uholanzi.PKSw 181.3

    Katika milima ya Piedmont, katika nyika za Ufaransa na pwani za Uholanzi, maendeleo ya kazi ya injili yalienda sambamba na umwagikaji wa damu ya wanafunzi. Lakini katika nchi za Kaskazini injili ilipenya kwa amani. Wanafunzi katika jiji la Wittenberg, waliporudi nyumbani kwao, walipeleka imani ya matengenezo katika nchi za Scandinavia. Machapisho ya maandishi ya Luther pia yalisambaza nuru. Watu sahili, wavumilivu wa Kaskazini waliacha ufisadi, majivuno, na ushirikina wa Roma, wakakaribisha usafi, usahili, na kweli za Biblia zinazobadilisha maisha.PKSw 181.4

    Tausen, “Mwanamatengenezo wa Denmark,” alikuwa mtoto wa kiume wa mkulima. Kijana huyu tangu awali alithibitisha kuwa na akili nyingi; alitamani sana elimu; lakini jambo hili halikuwezekana kwa sababu ya hali ya wazazi, hivyo aliingia nyumba ya watawa. Hapa, usafi wake wa maisha, pamoja na bidii na uaminifu wake, vilimfanya kupendwa na mkubwa wake. Mtihani ulionesha kuwa alikuwa na talanta ambayo kwayo siku moja angeweza kulihudumia kanisa vizuri. Iliazimiwa kuwa asomeshwe katika moja ya vyuo vikuu vya Ujerumani au Uholanzi. Mwanafunzi huyu kijana alipewa ruhusa ya kuchagua shule aliyoipenda, kwa sharti moja tu, kuwa asiende Wittenberg. Msomi wa kanisa hakupaswa kuhatarishwa kwa sumu ya uzushi. Hivyo ndivyo watawa walivyosema.PKSw 181.5

    Tausen alikwenda Cologne, mahali ambapo nyakati hizo, kama ilivyo sasa, ni moja ya ngome kubwa za Uroma. Hapa haukupita muda mrefu alianza kuchukizwa na imani zisizoeleweka za walimu. Wakati huo huo alipata maandishi ya Luther. Aliyasoma kwa mshangao na furaha, na alitamani sana kupata mafundisho binafsi kutoka kwa Mwanamatengenezo mwenyewe. Lakini ili kufanya hivyo alilazimika kumkasirisha mkubwa wake wa nyumba ya watawa na kujinyima ufadhili wa masomo yake. Muda siyo mrefu uamuzi wake ulifanywa, na haikuchukua muda alidahiliwa kama mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Wittenberg.PKSw 182.1

    Aliporudi Denmark, alirudi tena katika nyumba yake ya watawa. Hakuna mtu aliyekuwa amejua juu ya Ulutheri wake; hakufichua siri yake, lakini alijitahidi, bila kuamsha chuki za wenzake, kuwaongoza kwenye imani safi na maisha matakatifu zaidi. Alifungua Biblia, na kueleza maana yake ya kweli, na mwishowe aliwahubiri juu ya Kristo kama njia ya kuhesabiwa haki kwa mwenye dhambi na tumaini pekee la wokovu. Ghadhabu ya mkuu wa nyumba ya watawa ilikuwa kubwa sana, kwani alikuwa amejenga matumaini makubwa sana kwake kama mtetezi shujaa wa Roma. Aliondolewa katika nyumba yake ya kitawa na kupelekwa katika chumba cha peke yake chini ya usimamizi mkali.PKSw 182.2

    Katika hatua ambayo iliwaogofya sana wasimamizi wake baadhi ya watawa muda si mrefu walitangaza kuwa wameongoka na wamepokea Uprotestanti. Kupitia nondo za chumba chake Tausen alikuwa amewafundisha marafiki zake mafundisho ya kweli. Kama wale mapadri wangekuwa na stadi za kanisa za kushughulikia uzushi, sauti ya Tausen isingeweza kusikika tena kamwe; lakini badala ya kumtupa kaburini katika gerezani la ardhini, walimwondoa katika nyumba ya watawa peke yake. Sasa walikuwa hawana nguvu tena. Amri ya mfalme, ambayo ndiyo tu ilikuwa imetolewa, ilitoa ulinzi kwa walimu wa mafundisho mapya. Tausen akaanza kuhubiri. Makanisa yalifunguliwa kwa ajili yake, na watu walifurika kumsikiliza. Wengine pia walihubiri neno la Mungu. Agano Jipya, lililokuwa limetafsiriwa katika lugha ya Kidanishi, lilisambazwa sana. Juhudi za watetezi wa upapa za kutaka kushindana na kazi ya Uprotestanti ziliishia katika kuusambaza zaidi, na muda si mrefu nchi ya Denmark ilitangaza kupokea kwake imani ya matengenezo.PKSw 182.3

    Katika nchi ya Sweden, pia, vijana waliokuwa wamekunywa maji ya kisima cha Wittenberg walibeba maji ya uzima na kuwapelekea watu wa nchi yake. Viongozi wawili wa Matengenezo ya Kiswidishi, Olafu na Laurentio Petri, watoto wa kiume wa mhunzi wa Orebro, walijifunza chini ya Luther na Melanchthon, na kweli walizojifunza walizifundisha kwa bidii. Kama Mwanamatengenezo mkuu, Luther, Olafu aliwagusa watu kwa sababu ya bidii na ufasaha wake, wakati Laurentio, kama Melanchthon, alikuwa msomi, mwenye fikra nyingi, na mkimya. Wote wawili walikuwa wacha Mungu wa dhati, wenye uwezo mkubwa wa kiteolojia, na wenye ujasiri usiotetereka katika kueneza ukweli. Upinzani wa watetezi wa upapa ulikuwepo. Padri wa Kikatoliki aliwachochea watu wajinga na washirikina. Olafu Petri alishambuliwa na kundi la hao watu, na katika matukio kadhaa aliponea chupu chupu kuuawa. Hata hivyo, Wanamatengenezo hawa, walipendwa na kulindwa na mfalme.PKSw 182.4

    Chini ya utawala wa Kanisa la Roma watu walikuwa wamezamishwa katika umaskini na kushikiliwa katika ukandamizwaji. Hawakuwa na Maandiko; na wakiwa na dini ya ishara na sherehe tu, ambayo haikupeleka nuru yoyote akilini, walikuwa wakirudi katika imani za kishirikina na matendo ya kipagani ya mababu zao waabudu mizimu. Taifa liligawanyika katika makundi makundi, ambayo migogoro yao isiyoisha iliongeza matatizo ya wote. Mfalme aliazimia kuleta matengenezo katika serikali na kanisa, na aliwakaribisha wasaidizi hawa wenye uwezo katika vita dhidi ya Roma.PKSw 183.1

    Akiwa mbele ya mfalme na viongozi wa ngazi za juu wa Swideni, Olafu Petri kwa uwezo mkubwa alitetea mafundisho ya imani ya matengenezo dhidi ya mashujaa watetezi wa Uroma. Alitangaza kuwa mafundisho ya mapadri inapasa yapokelewe pale tu yanapopatana na Maandiko; kwamba mafundisho muhimu ya imani yawasilishwe katika Biblia katika namna iliyo ya wazi na sahili, ili watu wote waweze kuyaelewa. Kristo alisema, “Mafundisho Yangu siyo Yangu, bali Yake Yeye aliyenituma” (Yohana 7:16); na Paulo alitangaza kuwa kama angehubiri injili nyingine tofauti na ile aliyoipokea, angepaswa kulaaniwa (Wagalatia 1:8). “Iweje, basi,” alisema Mwanamatengenezo,“watu wengine wajipe mamlaka ya kutunga sheria zao, kwa mapenzi yao wenyewe, na kuwalazimisha wengine kuzitii kama mambo muhimu kwa ajili ya wokovu?”—Wylie, b. 10, ch. 4. Alionesha kuwa amri za kanisa hazina mamlaka ikiwa zinapingana na amri za Mungu, na alisisitiza kanuni kuu ya Kiprotestanti kuwa “Biblia na Biblia pekee” ni kanuni ya imani na matendo.PKSw 183.2

    Shindano hili, ingawa lilifanyikia katika jukwaa la siri, kwa kiasi fulani, linatuonesha“aina ya watu waliokuwa maaskari wajeshi la Wanamatengenezo. Hawakuwa watu wasiojua kusoma na kuandika, wabaguzi wa kidini, wabishi na wapiga kelele tu—walikuwa tofauti kabisa na kitu kama hicho; walikuwa watu waliokuwa wamelisoma neno la Mungu, na walijua vizuri jinsi ya kutumia silaha ambazo Biblia, kama ghala la silaha, inaweza kuzitoa. Katika suala la elimu, walikuwa mbele ya zama zao. Tunapoelekeza macho yetu katika vituo makini kama Wittenberg na Zurich, na kwa majina mashuhuri kama ya akina Luther na Melanchthon, ya Zwingli na Okolampadio, tunajikuta tukiwa tayari kuambiwa, hawa walikuwa viongozi wa hili vuguvugu, na inatupasa kwa kawaida kutarajia kwao nguvu ya ziada na maarifa mengi; lakini watu waliokuwa chini yao hawakuwa kama wao. Ndiyo, tunageukia maeneo yasiyojulikana sana kama ya Swideni, na majina madogo ya Olafu na Laurentio Petri—kutoka kwa walimu hadi kwa wanafunzi—tunakuta nini? ... Wasomi na wanateolojia; watu ambao waliuelewa kikamilifu mfumo mzima wa ukweli wa injili, na wanawaoshinda kirahisi wanafalsafa wa dhana mbalimbali na waheshimiwa wa Roma.”—Ibid., b. 10, ch. 4.PKSw 183.3

    Kama matokeo ya mdahalo huu, mfalme wa Swideni aliipokea imani ya Kiprotestanti, na siyo muda mrefu baadaye bunge lilitangaza kuunga mkono imani ya Kiprotestanti. Agano Jipya lilikuwa limetafsiriwa na Olafu Petri katika lugha ya Kiswidishi, na maelekezo ya mfalme wale ndugu wawili walitafsiri Biblia nzima. Kwa hiyo, kwa mara ya kwanza watu wa Swideni walipokea neno la Mungu katika lugha yao wenyewe. Baraza Kuu la Kitaifa liliamuru kuwa katika ufalme wote, wachungaji wafafanue Maandiko na kuwa watoto katika shule wafundishwe kuisoma Biblia.PKSw 184.1

    Pole pole lakini kwa uhakika, baraka hii ya nuru ya injili ilifukuza giza la ujinga na ushirikina. Likiwa limekombolewa kutoka katika uonevu wa Kiroma, taifa la Swideni lilipata nguvu na utukufu ambao lilikuwa halijaupata kabla ya hapo. Swideni ikawa ngome ya Uprotestanti. Karne moja baadaye, wakati wa hatari kubwa kuliko wakati mwingine wowote, nchi hii ndogo ambayo siku za nyuma lilikuwa taifa dhaifu—taifa pekee katika Bara la Ulaya lililothubutu kutoa mkono wa msaada—liliikomboa Ujerumani katika mgogoro wa kutisha wa Vita ya Miaka Thelathini. Kaskazini yote ya Bara la Ulaya ilionekana kurejeshwa tena chini ya utawala katili wa Kiroma. Majeshi ya Swideni ndiyo yaliyoiwezesha Ujerumani kugeuza mkondo wa mafanikio ya upapa, kupata uvumilivu wa kidini kwa ajili ya Waprotestanti,--Wakalvini na Walutheri,—na kurudisha uhuru wa dhamiri kwa nchi zilizokubali Matengenezo. PKSw 184.2

    Larger font
    Smaller font
    Copy
    Print
    Contents